Tulya anashindwa kuvumilia na kugeuza macho yake kumwangalia lakini sio kama awali safari hii Nzagamba hakuondoa macho yake usoni kwa Tulya na macho yao yanakutana na kuanza kutazamana Kila mtu akiwa na lake akilini.
Wanarudi kwenye mkeka pale Tulya anapopaliwa na chakula kwani nacho kilipotea njia kilipofika njia panda.
" uko sawa?" anauliza Bibi Sumbo akichukua kipeo Cha maji na kumpatia.
" kunywa" Tulya anakipokea na kunywa maji kidogo.
" hapo unajisikiaje?" safari hii Nzagamba ndie aliyemuuliza na kumfanya Tulya amtupie jicho la makosa ya nani lakini bado aliitikia kwa kichwa kuashiria yuko sawa.
"makosa yangu kuanzia leo kama Nzagamba yupo muwe mnaniwekea chakula nile peke yangu,nisiwanyime Raha wanandoa wapya" anaongea Bibi Sumbo na kumfanya Tulya akohoe kwa mara nyingine uso wake ukijaa aibu,Hali iliyomfanya Nzagamba kutabasamu kuona upande wa pili wa Tulya wenye aibu.
" hapana mama,kwa nini useme hivyo?" anaongea Tulya akiendelea kukohoa kidogo lakini sio kama awali.
" hapana,nimeshaamua nitakuwa nakula mwenyewe huko ndani kwangu uhuru ni wenu " anasisitiza Bibi Sumbo na kumfanya Tulya aanze kuangaza kama Kuna shimo karibu na hapo akajichimbie.Anageuka na kumwangalia Nzagamba aseme kitu lakini anamuona ndio kwanza anazidi kupeleka viazi mdomoni kama ndio kibarua chake asubuhi hii.
Bibi Sumbo aliyekuwa ameyaona mabadilishano ya macho ya mwanae tangu Tulya alipofika na kibuyu moyo wake ungekuwa nje ungeonyesha namna tabasamu la moyo mpana lilivyo.Akijua kuwa mambo yakiendekea hivi atapata habari nzuri hivi karibuni na nyumba yake itachangamka endapo mambo yataendelea hivi.
" karibu" wanamsikia Nzagamba na wote wanageuka kuangalia mlangoni na kumwona Sinde anaingia " Sinde" Tulya anaita nakumkaribisha." karibu"
"asante, shikamoo" anamsalimia Bibi Sumbo akikaa kwenye mkeka " Marahaba mwanangu hujambo" "sijambo,habari ya asubuhi" anawasalimia Nzagamba na Tulya " nzuri" wote wanaitikia kwa pamoja " karibu tule" Tulya anaongezea kimoyomoyo akishukuru ujuo wa Sinde kumtoa katika kindumbwe ndumbwe kilichokuwepo.
" mama kanituma nije kukwambia kesho umpitie asubuhi na mapema usichelewe" Sinde anaongea kilichomleta baada ya kumaliza kula. " mnaenda wapi?" Nzagamba anauliza akimwangalia mkewe " kuchukua udongo" Tulya anamjibu akikusanya vyombo.Nzagamba anaitikia kwa kichwa kumaanisha ameelewa moyoni akijisikia vibaya angekuwa anajiweza mkewe asingekuwa anahangaika.
" Sasa utakuwa unafanyia kazi wapi?nyumba zenyewe ziko mbili tu na sebule sio kubwa ya kutosha kuweka vitu vyako" anaongea Bibi Sumbo akiwa na wasiwasi.
" usiwe na wasiwasi mama,kwa sasa nitakuwa sitengenezi vyungu vingi,sebule yangu itatosha kuhifadhia" anamtoa wasiwasi.
" hapana, naelewa ukiwa unafanya kazi inahitaji utulivu na eneo utakalo kuwa na uhuru Nina uhakika huko sebuleni kwako utajibana tu"
" nitaenda kukata miti nimtengenezee uwaa huko nyuma nadhani patamfaa" anaongea Nzagamba na wote wanageuka kumwangalia kama hawaamini.Tulya anashukuru sana kuwa mumewe anatoa ushirikiano.
" hivyo itakuwa vyema,itabidi uanze mara moja Ili uwahi kukamilisha" Bibi Sumbo anamwambia kijana wake na Nzagamba anakubaliana naye.
"Mimi naondoka" Sinde anaaga " unaharaka ya nini,subiri uongee kidogo mpaka mchana,unisindikize na mtoni" Tulya anamzuia." si umetoka mtoni asubuhi hii?" Bibi Sumbo anamuuliza " ndio,nataka nikachote maji moja kwa moja Ili kesho nikiondoka usisumbuke" anamjibu mama mkwe wake." usiwe na wasi wasi wewe pumzika,kuchota vibuyu viwili vitatu havitaniua mama mkwe wako bado hajazeeka kihivyo" anajitetea Bibi Sumbo.
" najua hilo mama,sitaki tu kukaa nyumbani bila kazi siku itakuwa ndefu sana,nisubiri hapo Sinde nakuja" anaongea na kuingia ndani kwake Nzagamba nae anamfuata.
Ndani Tulya anataka kutoka anakutana na Nzagamba aliyesimama katikati ya mlango wa kutoka chumbani,Tulya anamwangalia kwa maswali " unachakusema?" anamuuliza akimwangalia usoni.
Nzagamba anakuna kidogo chake kama mtu anayetafuta kitu cha kusema na baada ya ukimya mfupi anaongea " kwani ni lazima ufanye hivi?" anamuuliza
" kufanya nini?" Tulya nae anamuuliza asijue anazungumzia nini
" kufinyanga vyungu"
" ndio,kwani hutaki?"
" hapana sio hivyo,namaanisha kama unafanya hivi kwa majukumu ya familia usijali Mimi ninaweza kuwahudumia wewe pamoja na mama vizuri tu" anaongea na Tulya kumwangalia kwa tabasamu lenye uhakika na kusema " najua,hutatuacha tulale njaa"
" Sasa kwa nini unataka kuanza kujitesa udongo ni mzito sana na mnakoenda kuchukulia ni mbali sana"
" Nafanya hivi kwa sababu napenda kufinyanga,na kuhusu udongo usijali nitakuwa nabeba kiwango ninachoweza kukibeba tu kwa hiyo usiwe na wasiwasi" anamhakikishia " naenda mtoni" anamuaga " sawa" anamuitikia na Tulya anatoka uso ukiwa umejaa furaha na Sinde anamuona.
"Nzagamba atakuwa mrina asali mzuri" anaongea Sinde baada ya kuondoka pale nyumbani.
" kivipi?" anamuuliza " maana umeingia ndani na umetoka na sura ile ya mtoto kupewa asali" anaongea na kucheka, inamchukia Tulya mda kidogo kujua Sinde anamaanisha nini.
" huna adabu wewe" Tulya anaongea akimpiga
" Ahh!unanipiga nimekosa nini mimi,wakati nyie ndio hamchelewi kuonyesha mahaba yenu hadharani" analalama Sinde.
" Amna lolote"
" kivipi,wakati watu tunaona kabisa juzi tu mlikuwa kama paka na panya Sasa mnaangaliana kama hamuwezi kuachana chumba kimebadilisha mengi"
" Amna kitu kama hicho,nimeshukuru tu kwa sababu amekuwa ni tofauti na nilichokitarajia "
"nilikwambia Nzagamba ni mtu mzuri,kasoro moja tu"
" najua,na hilo tutavumiliana hakuna mkamilifu hapa dunuani"
" ndio,na unabahati sana ndugu yangu"
" hata wewe pia,Tinde ni kijana mzuri na mpole,hivi si anakaribia kumaliza lindo?" anauliza Tulya akimzungumzia mchumba wake Sinde.
" mmh,nadhani mwezi ujao nitakuwa ndani"
" huuu!nakuja kucheza ngoma yako Mimi" anashangilia Tulya.
" ndio,we andaa njuga tu"
Wanafika mtoni na kwa mbali wanamuona Lindiwe na marafiki zake.
" hawa nadhani wamebaki kuhamia nyumba moja tu" ananong'ona Tulya wasimsikie.
" ndivyo walivyo siku zote wanagandana kama kupe" Sinde naye ananong'ona.Wanafika nakuwasalimia " habari zenu" " Nzuri" kina Lindiwe nao wanaitikia kwa pamoja huku wakikaguana juu mpaka chini.
Macho ya Tulya kidogo yatoke kwenye soketi zake baada ya kuiona sura ya lindiwe iliyovimba anafumbua mdomo wake na kuufumba asijue cha kusema ' kweli Manumbu ni mharibifu' anawaza Tulya.
" mnaangalia nini?" anaongea rafiki yake Lindiwe baada ya kuona Tulya na Sinde wakimwangalia Lindiwe " kwani wewe unaangalia nini?" Tulya nae anamjibu na kumfanya Sinde amvute kumnyamazisha. " ameanza kuringa sana tangu aolewe na Nzagamba" anaongea mwingine.Nimeringa nini na nimeolewa juzi tu,vilevile tangu niolewe sijawahi hata kuwaona anawaza Tulya.
"aringie nini mtu mwenyewe kaolewa mateso tu" Lindiwe ndie aliyeongea na kumfanya Tulya kumwangalia kama mtu aliyewehuka " najua ndoa yangu ni shida tupu,lakini yako imezidi" Tulya anamjibu huku akikunja sura yake kuashiria jinsi Lindiwe alivyovimba " unasemaje wewe?" Lindiwe analipuka nakutaka kwenda kumrukia Tulya wenzake wanamzuia.
"Tulya acha we bado mwali unajua,ukitolewa ngeu utamwambia nini mumeo" Sinde anampoza Tulya aliyekuwa tayari kumrukia Lindiwe endapo akimsogelea " kwani Mimi ndio nimeanza si amenianza mwenyewe" anaongea Tulya akimgeukia Lindiwe." Mimi na wewe tunamatatizo sawa Lindiwe" anaongea nakutulia kidogo kama anafikiria kitu "hapana mimi ni bora yako kwa sababu mume wangu hawezi kuninyoshea mkono nadhani unamjua vizuri,kwa hiyo siku nyingine tukionana kila mtu awe na lake itakuwa vizuri zaidi kwetu sote"
"unadhani niko hivi kwa sababu ya nani kama sio wewe,mume wangu amebadilika zaidi baada ya kukuona wewe sijui umemroga na nini" Anaongea Lindiwe na kumfanya Tulya acheke.
" utakuwa umesahau kama nilimkataa huyo mumeo mbele ya wazee,nimroge Ili iweje na hata kama ningekuwa na uchawi nisingehangaika kumroga mumeo kwani huko kungekuwa ni kupoteza mizizi yangu tu"
" kwa hiyo unasema mume wangu sio chochote?"
" sijasema Mimi,wewe ndio umesema" Tulya anamjibu kana kwamba hajui anachokisema Lindiwe au alichozungumza yeye
" nakuapia Tulya nitakufanya ujisikie ninachojisikia mimi we subiri tu"
" kama unataka kukosa usingizi juu yangu hicho kibarua ni chako,Mimi nitalala usingizi mzuri kabisaa"
Lindiwe anamwangalia kwa hasira lakini hakuwa na namna ila kuachana nae kwani anaona kabisa mwenzake karizika na maisha yake,shida ni zake na maamuzi yake aliyoyafanya,lakini kila akimuona Tulya anapata hasira kwa mambo mengi,kwanza kabla hajaja yeye ndio alikuwa mrembo wa Kijiji na baada ya Tulya kuja akawa gumzo la mtaa akimyanganya mwenzake taji la umaarufu,pili wivu,asijue unatokana na mumewe kumpenda Tulya au Nzagamba kumuoa Tulya wanaume wote waliokuwa wanamgombania yeye sasa mawazo yao yote yapo kwa Tulya.
Na Manumbu anamalizia hasira za kukataliwa na Tulya kwake na mwisho hiyo hali ya Tulya ya kujifanya hajali chochote inamkera zaidi kwani inamfanya ajifikirie kuwa angekuwa na ujasiri kama wa Tulya hali yake ya maisha ingekuwa tofauti lakini hiyo yote kwa sasa ni majuto ni mjukuu na kwake yeye anakaribia kupata na kitukuu.