zunde anaondoka nakumwacha tulya akiendelea kujiuliza kilichotokea pindi amezaliwa kuwa hakikuwa kitu Cha kawaida.lakini anaamua kuachana nalo na kuendelea na Mambo mengine kwani zimebaki siku tatu tu kabla ya harusi yake na nzagamba, na inampasa kuendelea kupanga akili yake kwa majukumu yake mapya.
siku tatu zikasogea zikawa mbili,na Sasa yakibaki masaa ya usiku,yakiisha tu inakuwa ni siku ya harusi yake.akiwa amekaa kitandani chumbani kwake jioni ya Leo,mwanga hafifu wa kibatari ukikiangazia chumba chake,masikio yake yakisia kwa mbali mlio wa shamrashamra za ngoma zilizokuwa zikipigwa nje na watu waliokuja kukesha kusherehekea, macho yake makubwa yakulegea akiwa ameyaelekeza kwenye kibatari hicho kama anakikifanyia uchunguzi wa macho lakini uhalisia ni kwamba mawazo yake hayakuwa hapo na sio kama alikuwa anakiona kibatari hicho.
Mawazo mengi yakipita kichwani kwake,wasiwasi na woga ukimwingia.anashtuliwa na mlango uliofunguliwa na kufanya mlio wa ngoma kusikia zaidi.anageuza sura yake na kumuona mke wa mjombaake runde akiingia akiwa na chakula mkononi.anavuta pumzi ndefu na kujiweka sawa kitandani.
" kulikoni mbona unapumua kama Mzee mwenye majukumu ya ukoo mzima" runde anaongea akiweka chakula chini.
" chakula hicho ukae ule ulale mapema leo kesho siku itakuwa ndefu sana"
" hapana mama sisikii njaa" anaongea akivuta tena pumzi ndefu nakumfanya runde akae kitandani.
" kwa nini?wasiwasi?"
anaitikia kwa kichwa na macho yake yaliokuwa yakiangalia chakula kilicholetwa kurudi kuangalia kibatari na kusema
" mwanzoni niliona ni harusi tu na nikiolewa maisha yataendelea kama kawaida, lakini Sasa nimeanza kuona ni zaidi ya majukumu"
" kivipi?kwa sababu utakuwa na watu wawili wa kuhudumia?"
anatikisa kichwa kukataa
" Sasa tatizo liko wapi?"
" sijui mama,lakini hapa.." anautoa mkono wake uliokuwa mapajani na kuuweka kifuani kwake sehemu ulipo moyo wake.
"..ninahisi Nina majukumu makubwa mno kuanzia kesho"
runde anatoa tabasamu pana likionyesha mwanya wake ulio kwenye mstani wa meno yake ya juuu.
" hivyo ndivyo Kila mtu hujisikia"
tulya anageuka na kumwangalia runde naye anaendelea.
" mabinti wote wanaoolewa siku za harusi zikikaribia hujisikia hivyo tunaita wasiwasi wa harusi" anamwangalia tulya aone kama ana lakusema baada ya kuona haongei anaendelea.
" mabinti hupata wasiwasi na wengine hufikia hatua ya kubadili mawazo kipindi hiki wakishindwa kujidhatiti vizuri"
" na wewe pia ulijisikia hivi?"
" ndio,tena wewe umefanya kazi nzuri sana tulikuwa na wasiwasi ungeanza mapema lakini umevumilia mpaka Leo wengine huanza siku kumi kabla hadi hufikia hatua ya kuugua"
" inakuwa mbaya kiasi hicho?"
" ndio,kwa hiyo usiwe na wasiwasi Kila kitu kitakuwa sawa chukua chakula ule kwani kesho Hali itakuwa mbaya zaidi hatutaki kuona bibi harusi akianguka"
" sawa,lakini ninaweza kula baadae kidogo"
" nitakuja kukagua" anasimama runde na kutoka akimwacha tulya apambane na Hali yake.
Upande wa nzagamba Hali haikuwa tofauti na ya tulya,akiwa amelala kitandani mgongo wake ukiambatana na ngozi zilizotandikwa kitandani humo macho yake yakiangalia bangili iliyoko mkononi pake asijue atafanya nini nayo kuanzia kesho,anajua wazi kuwa anatakiwa kuachana na hisia zake za zamani kama anaenda kuoa mtu mwingine lakini bado hawezi sababu anampenda Sana lindiwe.
Anashtuliwa na sauti za watu wakiongea sebuleni kwake kwa sauti za chini.sio kama kulikuwa hamna watu nyumbani kwao la hasha , nyumba Yao iliyozoeleka kuwa na watu wawili tu yeye na mama yake Leo ilikuwa na watu wengi ndugu na majirani waliokuja kwa ajili ya mkesha wakipika pombe kwa ajili ya kesho ngoma na nyimbo mbali mbali zikipigwa,lakini sauti zinazoongea sebuleni kwake anazijua vizuri sana.
Anaamka na kutoka sebuleni na aliowakuta ni walewale aliowahisia.
" aaa umetuharibia tulitaka tukushtue" anaongea mkita.
" niliwaambia Mimi msiongee atatusikia mnaona Sasa" ntula anaongea
" hata mngeingia kama sisimizi nzagamba angewasikia tu au mmesahau jina lake lingine" anaongea lingo aliyekuwa amesimama mlangoni bega lake likiegemea ukuta na macho yake yakiwa nje.
" kweli,hujapoteza kipaji tembo" anatania mkita.
Kwa mwindaji masikio ni muhimu sana na nzagamba anajulikana kwa kuwa na masikio mazuri zaidi na hisia mpaka kupelekea wenzake kumwita tembo.mda wote huo Wanaongea nzagamba anawangalia tu asijue hawa vichaa wanefuata nini kwake usiku huu ambao hataki usumbufu,anajiuliza moyoni.
" kwani mmefuata nini usiku huu" anawauliza macho yake yakipita kwa Kila Mmoja lakini kabla hawajajibu sauti nyingine inaongea njee.
" mnampango wa kulala humo au"
" kilinge naye yupo?" nzagamba anazidi kushangaa.
" ninavyomwangalia yupo sawa twendeni" anaongea mkita na lingo aliyekuwa kaegemea mlango anakuwa wa kwanza kutoka akifatiwa na mkita wanamalizia nzagamba na ntula aliyekuwa anamsukuma nzagamba mgongoni .
" tunaenda wapi?" anauliza nzagamba baada ya kutoka nje lakini hakuna aliyemjibu.
" mama tunaondoka nae huyu" anaongea kilinge akimwangalia bibi sumbo na kina mama wengine waliokuwa wakipika pombe.
" msije mkamlewesha tu kesho tukawa na bwana harusi mlevi"
"unajua mwanao hata anywe mtungi mzima halewi" anatania mkita wakiondoka.
wanaenda mpaka sehemu wanayokusanyika vijana jioni kunywa pombe na kuongea,lakini eneo hili Leo lilikuwa patupu tofauti na siku zingine. moto uliokuwa unaelekea kuzima ukiwaka eneo la kuwashia moto linalojulikana kama keanda,wote watano wanasogea karibu na eneo hilo na kukaa lingo akiongezea Kuni kwenye moto na kuuchochea uwake zaidi. mdomoni mwake akiendelea kutema mate yaliyokuwa yanatokana na utafunaji wake wa tumbaku.
" mbona pako kimya namna hii wengine wako wapi?" anauliza nzagamba macho yake yakizunguka kuangalia eneo lile.
" tumewafukuza tuna mambo yetu ya kikubwa Leo" anajibu ntula na akimfanya nzagamba amwangalie kwa maswali.
" hii nimeitoa mtaa wa pili nimeenda kuitafuta Leo asubuhii namapema kwa mama muza maarufu huko,imekolea hatari" anaongea mkita aliyekuwa amenyanyuka na kurudi na kibuyu Cha pombe akiinadi pombe yake.
"lete hapa" lingo anasimama na kumnyang'anya kibuyu na kumimina pombe kwenye kipeo anatoa tumbaku yake mdomoni na kuipachika katikati ya sikio lake na kichwa kwa juu kidogo, ikiwa ni akiba ya baadae kwani akiba haiozi ananyanyua kipeo na kunywa pombe yote aliomimina akiwashangaza wenzake.
" utaanzaje kunywa wewe,hii nilinunua maalumu kwa ajili ya nzagamba" analalamika mkita ambaye siku zote huonyesha kumpenda nzagamba zaidi.
" nilikuwa na kiu" likaja jibu kutoka kwa lingo akimimina pombe nyingine na kumpatia nzagamba ambaye anaipokea na kuipeleka mdomoni huku mkita akimwangalia kwa tabasamu pale aliposimama.
" hivi mkeo huwa haoni wivu mkita" anauliza ntula akimwangalia mkita aliegutuka na kutoa macho yake kwa nzagamba na kuyarudisha kwa ntula.
" wivu wa nini?"
" kwa sababu unampenda sana nzangamba kuliko mkeo" ntula anaongea macho yake yakienda kwa nzagamba aliyepaliwa na pombe kwa mshtuko na wengine kucheka.
" yeye ana nafasi yake na nzagamba ana nafasi yeke" anajibu mkita akikaa kwenye gogo huku akilamba midomo yake ya chini.
" kuwa makini wivu wa mwanamke unaweza ukafanya mvua ikanyesha kiangazi" anatania kilinge na wengine kucheka.
" tena pasipo na mawingu" anaongezea lingo.
"acheni" anakemea nzagamba akimpatia mkita kipeo aliyekuja kujipenyeza pembeni yake na wengine kucheka.
" tuachane na hayo twende kwenye kilichotuleta hapa" anaongea mkita akipiga makofi kama mwenye kiti wa kikao akitaka watu waelekeze masikio kwake kwenye mkutano mkubwa.
" kimetuleta nini?" anauliza nzagamba aliyekuwa gizani mpaka Sasa hivi asijue kwa nini marafiki zake wamemchukua na kumleta huku usiku huu na kesho ni harusi yake.
" kukupatia vidokezo vya kesho usiku siunajua sisi wazoefu" anaongea lingo na kumfanya nzagamba akohoe akimwangalia kilinge aliyekuwa akitikisa kichwa kukubaliana na alichokisema lingo.
" hatutaki uaibike kesho kaka yetu ndio maana tukaita kikao hiki" mkita nae anachangia akimshika bega nzagamba.
" kesho hiyo mkifika chumbani.." anaanza ntula lakini kabla hajaendelea anakatishwa na nzagamba.
" acha" lakini bado anaendelea tu
" anatakiwa kwanza atoe shanga zake za shingoni.."
" nimesema ACHA" nzagamba anaongea kwa ukali akiwafanya wote wafunge midomo Yao.
" Mimi sio mtoto mdogo,na hayo Mambo yote tumeshafundishwa jando.."
" tukajua umesahau" anaingilia mkita mdomo Wake usio na kishikizo na kumfanya nzagamba amwangalie kwa jicho Kali anageuka anamwangalia kilinge.
" siamini na wewe kama umejiingiza kwenye mchezo huu,tulya si binamu yako utaongeaje vitu hivyo?"
" sijaja hapa kama Binamu au kaka nimekuja kama rafiki yako,ukubwa wa majukumu huu jamani" likaja jibu kutoka kwa kilinge akimalizia kutikisa ulimi na kuwafanya wengine wacheke na yeye akimalizia kucheka.
" usijali nzagamba sisi tunataka tu kukupa ujuzi kidogo unawezafika hapo ukapotea" anaongea lingo na wengine wakiendelea kucheka.
" acheni nimesema, hilo nitalishughulikia mwenyewe" anakazia nzagamba.
" makosa yanatokeaga ujue" anazungumza ntula aliyekuwa bado Yuko mbali kuacha kumtania nzagamba na wengine kucheka.
Nzagamba anawaangalia tu wakiendelea kucheka.Licha ya nzagamba kutokuoa au kutokuwa na wanawake hapo awali sio kama hajui namna ya kuwa na mwanamke kwani amesikiliza hadithi nyingi za wazee na marafiki zake huko awali ambako bado alikuwa anajichanganya na wenzake ukijumlisha na mafunzo ya jando ambako vijana hufundishwa Kila kitu kuhusu maisha ya unyumba hivyo anauwelewa mzuri wa kutosha kummudu mwanamke kitandani ila aliahidi ujuzi huo angeutumia kwa mwanamke aliyempenda na kwa mkewe,baada ya lindiwe kumwacha alipoteza mvuto na Mambo hayo ila kwa Sasa kuwa anaoa inabidi arudishe.
" ulivyoenda kumsalimia umempelekea zawadi gani?"anashtuliwa na sauti ya lingo
" hajaenda" anajibu kilinge kwa uhakika na wengine kumwangalia nzangamba kwa mshangao.
" umekwisha" anajibu mkita na kumfanya nzagamba amwangalie kwa kutokumuelewa.
" we mwache adhabu atakayopata ataikumbuka maisha yake yote na ninavyomjua tulya." anamalizia kilinge akitikisa ulimi wake.
lingo anapiga mluzi na kusema " kweli umejipalia makaa kichwani"
" ongeeni kwa kueleweka niwaelewe acheni kuzunguka" anang'aka nzagamba akikereka na tabia za marafiki zake.
" unasikia nzagamba" anaongea mkita akiinamisha kichwa chake karibu na sikio la nzangamba kama anataka kumnong'oneza " usipoenda kumsalimia mwanamke akiwa ndani ukimuoa huwa wanatoa adhabu"
" adhabu gani?"
wote wananyanyua mapega Yao kuonyesha hawajui.
" mbona sijawahi kusikia hiyo" anauliza kwani kweli hajawahi kusikia kuwa usipoenda kumsalimia mwali unapewa adhabu ukimuoa.
" nani anatoa adhabu?"
" mkeo,awe nani?" likaja jibu kutoka kwa kilinge na anaendelea " wanafundishwa huko wakiwa wali ni kuhakikisha waume zao wanakuwa hapo wanapowahitaji,Sasa wewe hujaenda hata siku Moja kama naona maisha yako muuliza lingo alifanyweje?"
Macho ya nzagamba yanaenda kwa lingo aliyesema " niliambiwa nilale uvungu wa kitanda siku mbili" na wengine kucheka akiwemo yeye mwenyewe lingo.
" usiku wa harusi yenu?" anauliza nzagamba
" hapana" ntula ndio anajibu na kuendelea " anaweza akasubiri hata mwaka ndio akakukomesha utakuwa Hadi umeshasahau"
" wanawake wanajua kuweka fundo." anajibu nzagamba akikumbuka siku chache zilizopita alikutana na sinde aliyemuuliza kwa nini hajaenda kumuona tulya na yeye kumjibu kuwa sio lazima " unabahati tu unamuoa tulya ingekuwa Mimi ningekukomesha" lilikuwa jibu la sinde siku ile na Sasa anaelewa alikuwa anamaanisha nini.
" tena sana" kilinge anakubaliana nae.
" Mimi alisubiri msimu wa baridi tena wakati namuhitaji zaidi nikaambiwa nisipotii mpaka msimu utakapoisha nisimsogelee,nikaona Bora kulala siku mbili uvunguni kuliko nipate ngiri ya mwaka"
anamalizia lingo na wengine wakicheka zaidi na wakati huo nzagamba akijiona yupo hatarini hakujua kuwa Kuna upande wa pili wa shilingi kwani tamaduni zinakataza sema vijana huwa wanajiiba tu kwenda na yeye sio kama aliamua kufuata Sheria ila hakuona umuhimu wake kwani alikuwa hana cha kuongea nae akienda.
" Nina uhakika alikuwa anakusubiria Kila siku ninavyomjua binamu yangu yule kazi unayo" anajazia chumvi kwenye kidonda kilinge huku akiwasha Kiko yake nakuanza kuvuta.
" nilimuona mara Moja tu siku ya tambiko anaonekana sio wa mchezo" anakandia ntula
" nyie hamkumuona siku amegombana na manumbu" mwili unamsisimka mkita nakuendelea" alikuwa hatari mpaka manumbu akazima" anaongezea mkita.
' ndio najua ni kichaa' anawaza nzagamba mwili ukimsisimka hakujua kama Mambo yangekuwa hivi,sura ya tulya inapita usoni kwake nakuona ilivyokasirika mwili unamsisimka tena ataishije na mwanamke kama yule na Sasa ameshariharibu kabisa.
" usiwaze utapewa adhabu yataisha mbona ya lingo yaliisha tu ila kwa binamu yangu tegemea makubwa zaidi ya kulala uvunguni nasubiri siku ukija kusimulia" anaongea kilinge akipiga Moshi wa tumbaku aliyovuta kwenye Kiko hewani aking'ata na kupuliza.
"kesho tutacheza ngoma ya harusi yako vizuri" anaongea kilinge macho yake yakiwa angani na wengine kufuatiza macho yake na kwenda angani.
" ndio mwezi utakuwa mkubwa kesho" anaitikia ntula.
" hivi mmewahi kusikia usemi unaosema kuwa watu wakioana au wakikutana siku ya mwezi mkubwa hupendana mpaka kufa" mkita anakuja na dawa yake.
" kama ingekuwa hivyo wengi wangesubiri siku hiyo" anajibu kilinge.
" ni kweli kabisa" mkita anatetea hoja yake.
" na Mimi nimewahi kusikia,ila sio upange, hiyo huja tu kama bahati kama nzagamba ambaye hakujua kama kesho itakuwa mwezi mkubwa,na wakioana huishi mda mrefu" anachangia lingo.
" unaona,Mimi niliisikia kwa babu yangu" anachangia tena mkita.
" basi nzagamba anabahati"
Nzagamba anashtuka kusikia jina lake likitajwa kwani akili yake haikuwa pale, kwa muda ilihama na kuhamia nyumbani kwake ikifikiria ni adhabu gani atakayopewa na yule mwanamke kichaa anatikisa kichwa chake kuzuia mawazo.
" unasema?" anauliza baada ya kurudi kundini.
" mda wote huo hujatusikia?" anauliza mkita.
" atakuwa anawaza adhabu,usijali shemeji yangu,Nina uhakika hiyo haitakuja Leo wala kesho,ninavyomjua tulya anaweza kusubiri hata ukazeeka" wote wanacheka.
" naenda kujisitiri" anaongea akinyanyuka,baada ya nzagamba kuondoka wenzake wanacheka.
" atakuwa anaenda kwenu ee" anauliza ntula akimwangalia kilinge.
" Nina uhakika wa kupinga kichwa changu kwenye shoka" mkita anapinga kichwa chake.
" ila mmemtisha" anaongea kilinge.
" lingo ndio alizidisha ya kulala chini ya uvungu na ngiri" anaongea ntula akimwangalia lingo aliyekuwa Anacheka na kuchukua akiba yake alikoiweka awali sikioni na kuirudisha mdomoni.
Miguu ya nzagamba inampeleka Hadi kwa Mzee Shana,anafika na kuona watu wengi waliokuja kukesha wakiwa nje wakipiga ngoma na kucheza wakiimba nyimbo mbali mbali za harusi.
Macho yake yanaenda kwenye nyumba ndogo kati ya nne zilizokuwa maeneo yale na kuona mwanga wa kibatari ukipenya na kutoka njee kupitia matundu mbalimbali yaliyopo katika nyumba ile,miguu yake inataka kupiga hatua kuelekea huko lakini inakataa kwani Kila akitaka kusogea watu wanapita na yeye hatakiwi kuonekana hapa.
' nimekuja kufanya nini hapa' anajiuliza ile anataka kugeuka aondoke anagongana na mtu.