zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya harusi ya tulya.wageni wanazidi kuwasili na maandalizi yanazidi kupamba moto.
" imekukaa sawa?"
anauliza bibi sumbo aliyeleta nguo na urembo mbalimbali kwa ajili ya tulya kuvaa siku ya harusi na kama ilivyotamatuduni familia ya bwana harusi huusika na mavazi na urembo wote wa bibi harusi siku ya harusi.Tulya anavijaribisha nakuona vimemkaa vizuri.
" ndio,kama ulinipima" anajibu tulya akijiangalia.
"mmmh" wanaitikia runde na zunde waliokuwepo ndani ya chumba.
" umependendeza sana mwanangu"
anaongezea zunde akimwangalia Binti yake
" kwa sababu ni mrembo sana" anaongezea bibi sumbo na runde kuitikia kwa kichwa na kusema.
" yupo kama wewe ulipokuwa Binti umejizaa kabisaa"
" kweli kabisa" anasapoti bibi sumbo na kuaga
" Mimi nawaacha bado Nina Mambo mengi kidogo ya kufanya nyumbani" anaongea akisimama.
" Haina shida tutaonana"
anatoka runde nae anatoka kumsindikiza na kuwaacha mama na mwana ndani tulya akivivua vitu vile na kuviweka pembeni.
" chukua na hii"
zunde anampatia mfuko wa ngozi,tulya anaupokea huku akimwangalia kwa maswali na mama yake anaendelea.
" hivyo vimetoka kwa shangazi zako"
Tulya anatoa vitu vilivyopo kwenye mfuko na anakuta shanga anazotakiwa kuvaa kiunoni (chachandu) na kama ilivyo Mila shangazi wa bibi harusi ndio anayetakiwa kutengeneza shanga hizo.
" ni nzuri sana" anaongea akiwa na tabasamu pana.
" ndio ni nzuri wewe ndio mpwa wao wa pekee unaeolewa kwa nini wasitafute shanga nzuri"
tulya anaitikia kwa kichwa na kuuliza
" shangazi mkubwa anakuja?"
" hawezi Kuja,unajua miguu yake inavyomsumbua hawezi kutembea umbali mrefu analalamika tu kwa nini umeolewa mbali asiweze kucheza ngoma yako ya harusi anywe pombe mpaka wamzoe"
Tulya Anacheka " na kweli ninavyomjua shangazi mngemzoa kweli,shangazi wadogo si wanakuja"
" ndio,watakuja na baba yako na kaka zako" zunde anaziangalia tena shanga na kusema
" wamefanya kazi nzuri sana"
"ndio" anajibu macho yake yakiwa kwenye shanga,kimya kifupi kinapita tulya anasikia kama mtu analia,anamwangalia mama yake aliyebadilika sura na kuwa ya huzuni machozi yakimtoka.
anaweka shanga pembeni na kwenda kukaa pembeni yake.
" unalia nini tena mama?"
" napata huzuni sana Kila nikiwaza utakuwa mbali na Mimi milele"
" usiseme hivyo mama nitakuwa nakuja kuwaona" anaongea macho yake yakitokwa machozi pia.
" nisamehe mama nimekuwa nakusumbua tangu utoto mpaka Sasa nakusumbua tu"
anaongea akimshika mikono yake,na zunde anafuta machozi yake na kumwangalia Binti yake.
" hapana mwanangu,hii ni karma yangu nilipotaka kuolewa na baba yako mama yangu alilia namna hii na kusema sielewi anavyojisikia nikamwambia naelewa,Sasa Leo hii nimeona mama yangu alikuwa anamaanisha nini"
" usilie mama nitakuwa sawa,vile vile mjomba na kina binamu wapo karibu hapa sitapata shida hata kidogo"
anamwambia huku akimfuta machozi mama yake.
" nakuombea na wewe uzae mtoto wa kike awe mbishi kama wewe Ili uone ninavyojisikia"
" Nina uhakika bibi alikwambia hivyo"
" umejuaje?"
" Mimi hapa ndio shahidi anayeishi"
" kweli"
wote wanacheka huku wakikumbatiana.
" jaribu na hizo tuone kama Zina kukaa vizuri kama ndogo au kubwa tuzirekebishe"
" nisaidie kuvaa" anamwambia mama yake kwa kudeka.
" unatakiwa kukua mtoto wa kike wewe unaolewa kesho kutwa tu hapo"
" ndio maana nataka kunyonya mara ya mwisho"
wote wanasimama na zunde anachukua shanga na kuanza kumvalisha tulya kiunoni baada ya kumaliza zote anasogea mbali kidogo kumwangalia.
" zimekukaa vizuri"
" ndio na nimezipenda sana"
" zinafanana na za mama mkwe wako kama zimetengenezwa na mtu Mmoja"
" ndio,utakuwa upendo wao unalingana" anaongea tulya akijiangalia kiunoni akigeuka huku na huko.
" shangazi yako mkubwa alinunua na wale wadogo wakazitengeneza wamefanya kazi nzuri sana"
" hawana mpwa mwingine wa kuozesha wakamtengenezea shanga ila Mimi tu" anaongea tulya kwa kujivuna na mama yake Anacheka.
" mama mkwe wako ni mtu mzuri sana sina wasiwasi juu ya hilo" anaenda kukaa kitandani akimwangalia Binti yake akivua shanga alizotoka kujaribisha na kumpatia.
" ndio,Nina bahati sana"
" vipi kuhusu mumeo mtarajiwa?"
tulya anajichekesha na kuendelea kutoa shanga kiunoni asimwangalie mama yake usoni
" ni mtu mzuri,habari zake si umeshazisikia Kila mtu anamzungumzia kasoro ni kuwinda tu"
zunde anamwangalia Binti yake akijua Kuna kitu anamficha na yeye ameliona hilo kwani kamlea mwenyewe.
" vipi? hakupendi?"
" mama unaongea nini?,hii ndoa imekuja kwa ghafla kwa Kila Mmoja kutokunipenda ni sawa tu na sio kama nampenda"
" usinidanganye tulya,nakuona kabisa unampenda huyu kijana"
" hapana mama umelelewa vibaya" anamkwepa mama yake lakini zunde alikuwa bado Yuko mbali kuachana nae.
" kama humpendi kwa nini Kila siku unakaa nje usiku unamsubiri nani?"
tulya anamwangalia mama yake kwa mshtuko akijiuliza amejuaje wakati huwa anahakikisha Kila mtu amelala ndio anatoka nje.akisubiri labda nzagamba atatokea Kuja kumuona lakini hajawahi kufika hata siku Moja,roho inamuuma sana,kwani hata awafiche vipi wengine moyo wake hawezi kuuficha uliokuza hisia juu ya nzagamba baada tu ya kumuona siku ya sherehe macho yake yakavutiwa naye yakamfanya asigeuze peo za macho yake kwingine ila kwake kama anavutwa na sumaku hapana moyo wake ulimoenda kabla hata ya kumuona alipousikia mziki wake wa huzuni kwa mara ya kwanza siku ile mtoni mapigo ya moyo wake yakienda mbio kwa kutambua kuwa mtu waliokuwa wanamsubiria Yuko karibu,lakini akili yake ikaamua kupuuzia.
" nachoka kukaa ndani ndio maana huwa nakaa nje wakati wa usiku nipate upepo kidogo" anamwongopea mama yake.
" njoo ukae hapa"
Tulya anaenda na kukaa pembeni ya mama yake " Haina haja ya kumdanganya mama yako mwanangu Mimi najua Kila kitu kwa sababu nimekuzaa maumivu anayopitia mwana siku zote mzazi hujua,unakaa nje kumsubiri yeye ukijua atakuja kukuona"
tulya ananyanyua mdomo Wake kusema kitu anakosa na kufunga tena.
" kwa nini ulimchagua mwanaume akuoe wakati hakupendi na hakutaki,afadhali ungeolewa na huyo mwingine nani.." zunde anaanza kufikiria jina la manumbu
" manumbu na ungeishi vizuri kabisa"
" hivi mama unajua kwa nini nilikuwa sitaki kuolewa na kufanya vituko vyote hivyo?"
" kwa nini?" zunde anamwangalia Binti yake kwa uso wa maswali.
" kwa sababu nilikuwa sitaki kuolewa mitala,sikutaka kuishi kama wewe na mama wakubwa mnavyogombana na wao kukufanya wewe kijakazi wao na masimango sikutaka kuishi kama hivyo mama"
" tulya mwanangu utapata wapi mwanaume ambae hataki mitala wote wako hivyo"
" nzagamba, kwake yeye nitakuwa peke yake milele"
" lakini hakupendi"
" hayo ni Mambo yanayoweza kubadilika mama,yawezaikawa ananichukia Sasa lakini nikimwonyesha moyo wangu wa dhati ipo siku ninauhakika atalirudisha pendo langu"
" kwa nilivyosikia anamwanamke anayempenda unadhani ataweza kumsahau kirahisi Nina hofu hilo ndilo litakalo kutesa zaidi"
" usiwe na wasiwasi mama,yule alikuwa mchumba wake aliyemuumiza Mimi naenda kuwa mke wake nitakaeenda kutibu majeraha yake Nina uhakika atapona kwani nitahakikisha nimekuwa tabibu mzuri"
zunde anamwangalia Binti yake nakujiona kama anajiangalia kwenye kioo kwani Hali hii ni inajurudia tofauti ni kuwa yeye aliolewa na mwanaume aliyempenda anamhofia Binti yake ataishije, lakini anaamua kuacha Mambo yaende kama yalivyo anauhakika huko mbeleni yatajirekebisha.
anamkumbatia Binti yake na kuvuta pumzi ndefu.
" ohh,tulya nikufanyeje wewe"
" unamchukia nzagamba mama?"
anamuuliza na kumfanya mama yake avunje kumbatio lao na kumwangalia Binti yake usoni.
" kwa nini unasema hivyo,anaenda kuwa mkwe wangu hata kama sijamuona bado lakini kutoka na alivyoniambia zunde na wewe unavyomzungumzia pia ni rafiki wa kilinge,Nina uhakika ni mtu mzuri wasiwasi wangu ni huo tu hakupendi najua hutaki kuonyesha ila unaumia sana,unakaa njee Kila siku usiku licha ya kuogopa mafisi unamsubiri hilo linaniuma"
Machozi yanamtoka tulya akiinamisha kichwa chini akiangalia mikono yake iliyoshikana na mama yake.
" kusema ukweli mama inaniuma sana,Kila nikikumbuka macho yake yanayoniangalia kwa chuki nakosa matumaini,anaona Mimi namletea shida zaidi katika maisha yake, nakaa na matumaini pasipo kujua ataniangalia hivyo mpaka lini,hasa pale nitakapokuwa namuona Kila siku,ninaogopa mama" anazidi kulia.
" oooh,Binti yangu maskini"
zunde anamkumbatia " usijali Nina uhakika Kila kitu kitakuwa sawa,kwani wewe ni nani?"
anatoa mikono yake mabegani nakuanza kumfuta machozi.
" wewe ni Binti yangu tulya,kama jina lako lilivyoa (tulivu) we vuta subira tu Nina uhakika ataangukia pua kwako kwani hamna mtu anayekuchukia wewe hivi nimewahi kukwambia?"
" nini?" anamuuliza akifuta makamasi yaliokuwa yakichungulia matundu madogo mawili yaliopo usoni pake kwa kiganja chake Cha mkono.
" ulipozaliwa,tulitaka tukupeleka kwa Mzee wa Kijiji hapo kupata baraka kwani katika ukoo wa baba yako kulikuwa amna Mzee wa umri mrefu"
kwa Mila na desturi watoto wote wanaozaliwa hupelekwa kwa wazee wakubwa walioko Kijijini Ili kuwabariki au kama Kuna Mzee mkubwa wa familia au ukoo huja na kumbariki mtoto wakimwambia akue afikie umri kama wao.
zunde anaikumbuka siku hiyo ambayo alishasahau anaikumbuka leo.wakati wanajiandaa kutoka wanasikia mtu akibisha hodi,zunde anatoka na anashangaa kumkuta mwanamke kikongwe sana tena akiwa na mkongojo mkononi ambaye hajawahi kumuona.
" shikamoo bibi" zunde anamsalimia kwa heshima na yule bibi akatoa tabasamu pana lililoonyesha meno yake meusi na machache mdomoni.
" Marahaba mjukuu,ninaweza kupata maji Nina kiu" anaongea kikongwe,zunde anamwangalia kwa makini bibi huyu aliyekuwa amefunga kaniki Moja tu ndefu,nywele zake zikiwa ndefu na kujisokota pua yake ikiwa imepauka kama katoka kuvuta tumbaku na mkononi mkongojo wake ukimsaidia kujihimili, mwili ukimtetemeka. zunde akagundua kuwa ana njaa na akiendelea kusimama mda mrefu anaweza kuanguka.
anamshika mkono haraka " bibi njoo ukae hapa wakati unasubiri nikuletee maji"
zunde anampeleka. chini ya kivuli Cha mti uliyokuwa uaani na kumkalisha kwenye kiti Cha miti kilichoambwa ngozi na kumkalisha.
"nisubiri hapa, sawa bibi" anarudi ndani haraka anapita jikoni na kuchukua kipeo chake anaweka maziwa ya mgando aliyokuwa kwenye kibuyu,akikumbuka baba yake anapenda sana maziwa akisema yanakata kiu na njaa kwa wakati Mmoja.
" nani huyo" Mzee kijoola aliyekuwa amekaa na mtoto anamuuliza.
" simjui ila ni bibi na anaonekana ananjaa sana,ameomba maji nimeona nimpatie maziwa.mzee kijoola anaitikia kwa kichwa zunde anaendelea na safari yake kwenda nje.
Anaenda Mahali alipokuwa amekaa na kumpa maziwa.
" kunywa haya bibi yatakusaidia kukata kiu na njaa"
" hahahaha,una roho nzuri sana mjukuu ndio maana umebarikiwa,asante sana" bibi anakunywa maziwa yote kwa wakati Mmoja pasipo kupumzika na kumshangaza zunde.
wakati anamalizia mtoto akawa analia ndani na kumfanya bibi akatishe kunywa maziwa na kumwangalia zunde.
" unakachanga?"
" ndio" zunde anajibu akitabasamu.
" haya nenda usimfanyie akusubiri Mimi nitakuwa sawa mwenyewe hapa nikimalizia maziwa yangu.
" sawa bibi"
Zunde anarudi ndani haraka na kumchukuwa mtoto.
" huwezi hata kumbembeleza" anamwambia Mzee kijoola.
" ni mlizi sana huyu"
zunde anamcheka mumewe aliyekuwa na furaha ya kupata mtoto wa kike.
" nenda basi ukaangalie kama bibi kamaliza maziwa uchukue kipeo tuondoke.
" sawa"
Mzee kijoola anatoka nje na kushangaa kumuona bibi ambaye hajawahi kumuona Kijijini hapa akiwa ameshika mkongojo wake kwa mikono yake miwili na kuegemeza kichwa chake kwenye mikono iliyoshika fimbo na kufumba macho kama amelala,kama anasikia mtu anakuja ananyanyua kichwa chake a kumuona kijoola akija bibi anatoa tabasamu kama kijoola ni mjukuu wake ambaye hajamuona miaka mingi. Mzee kijoola anamsogelea na kumsalimia.bibi anampatia kipeo ambacho tayari alikuwa amekiweka chini na Mzee kijoola kuanza kuondoka.
" unaumri gani?"
" ehh?" Mzee kijoola anashtuka kwani alikuwa hajui anazungumzia nini.
" mtoto anasiku ngapi?" bibi anarudia swali.
" siku tatu"
" mtakuwa hamjampeleka kwa wazee basi au wamekuja"
" hapana ndio tulikuwa tunajiandaa tumpeleke"
" ninaweza kumuona?"
" ehh! ndio" Mzee kijoola anajibu akimwangalia kwa makini huyu bibi na kupata uhakika kuwa hajawahi kuamuona hapa Kijijini ' labda ametoka Kijiji Cha jirani' anajiwazia na kumpotezea.
" twende huku ndani bibi"
" hapana kijana wangu nimechoka sana unaweza kumleta tu hapa sitachukua mda mrefu"
Mzee kijoola anakuwa Hana jinsi ila kumwita mkewe.
" zunde mlete mtoto huku bibi amuone"
baada ya muda wa dakika kama tano zunde anatoka akiwa na mtoto na kumpatia bibi huyo aliyekuwa amekaa.
" ayii,ayii,ayii, mrembo kweli wewe" anaongea bibi baada ya kumshika.mzee kijoola wanatazamana wakijiuliza amejuaje kama mtoto ni wa kike,bibi kama lionaona nyuso za maswali wakati macho yake yalikuwa kwa mtoto anasema " kafanana na mama yake" anamrusha juu na kufanya mawazo ya zunde na kijoola kuhama upesi kuelekea kwa mtoto wao. roho za wazazi wawili kulipuka kwa kuhofia kuwa bibi angemuangusha mtoto kwani hakuwa na nguvu za kutosha na kumfanya bibi acheke kwa mwonekano wa wazazi hao.
anamweka miguuni na kumwangalia usoni kama anamsoma.
" mmepata Binti mzuri sana,sura yake inaonyesha kuwa atapendwa na watu wengi sana,ardhi itamtiii na ataheshimika na watu wengi atakaa pembeni ya nyota kubwa ya magharibi inayotembea na mwezi na jua,mikono yake imebeba vingi vya thamani,ulimi wake ni dawa na ni mtu asiyerudi nyuma ni mpambanaji" bibi anamalizia kwa kucheka akiwaacha njia panda zunde na mumewe ambao hawakujua anazungumzia nini.
Bibi anamnyanyua juu tena mtoto na zunde na kijoola wakajua alikuwa anambariki.
" ukuwe uwe na maisha marefu kama mababu zetu,mizimu ikulinde na Kila mwenye Hila mbaya na wewe, udhaifu wa mwili iwe mwiko kwako Kila utakachogusa ni thamani kwako,utakuwa ni mtulivu kama bahari."
bibi anamaliza na kumpatia zunde mtoto aliyekuwa amenyamaza mda wote tangu ameshikwa na yule bibi.
" asanteni sana wajukuu Sasa Haina haja ya kwenda kwa wazee" anaongea akisimama mkono wake ukishikilia mkongojo,macho ya zunde yanaenda kwenye vidole vyake vilivyopauka na kucha zilizokuwa ndefu na chafu kama katoka kuchezea udongo anajiuliza kama ndugu zake walikuwa wanamtesa.
" Mimi naondoka"
" sawa bibi asante sana" anaongea zunde na bibi kucheka akiondoka. wote wanageuka na kuelekea ndani baada ya kupiga hatua chache zunde anageuka kumwangalia bibi huyo na kukuta hayupo.
" kijoola"
" mmhh" anaitikia na kumwangalia mkewe nakuona akiangalia alikokuwa yule bibi na yeye kufuata macho ya mkewe.
" kaenda wapi?" anauliza Mzee kijoola baada ya kuona bibi kapotea kwani ilikuwa ni wakati wa kiangazi angeonekana hata kwa umbali mrefu na kwa mwendo wake asingefika mbali au akimbie.
mbio zenyewe ziwe za swala akikimbizwa na Simba lakini bibi hata kama angekimbizwa na Simba asingeweza kupiga hatua hata Moja anajiwazia kijoola lakini mawazo yake yanamwonyesha uhalisia mwingine bibi kakimbia na kupotea.
Leo hii zunde ndio anakumbuka tukio hili la maajabu lililotokea siku tatu baada ya tulya kuzaliwa.
" alipotea?" anauliza tulya kwa mshangao.
" ndio,hatukujua alikuwa ni nani na katoka wapi,tulimweleza Mzee Mmoja mganga wa Kijiji akasema tuliikaribisha mizimu tukaitendea wema nayo iakatubariki,ndio maana tukakuita tulya kama mwenyewe alivyosema maana yake ni tulivu kama bahari"
" hayo maajabu!"
" ndio,yalikuwa maajabu lakini Sasa nimeamini kwani Kila kitu alichokisema kipo kwenye tabia zako na hayo mengine ya ardhi kukutii na pembeni ya nyota na mwezi sijui hata alimaanisha nini,ila Nina uhakika nzagamba atakupenda tu wewe hukuandikiwa chuki maishani mwako"