"umefuata nini hapa"
" kwani ni vibaya kumtembelea rafiki yangu"
"mmh,sio kawaida yako Kuna nini?"
" kwa nini umeshuka ningekufuata huko juu"
nzagamba anamwangalia rafiki yake kilinge alieanza kupanda mti kuelekea juu alikokuwa amekaa na yeye anaanza kupanda,baada ya kufika juu kilinge anatafuta tawi anakaa akililalia chali nzagamba nae anakaa pale alipokuwa amekaa awali.
" Kuna nini" nzagamba bado anaendelea kumpeleleza rafiki yake akijua hakuja hivihivi tu.
" nimekwambia nimekuja kukusalimia,kwani sio mda tutakuwa ndugu,au hujafurahi kumuona shemeji yako"
nzagamba anamwangalia pasipo kusema neno.
" nipe hiyo" anaonyesha kalimba na nzagamba anampatia,kilinge anaiangalia nakupitisha dolegumba yake kujaribu.
" siku nyingi sijapiga vidole vimeanza kuwa vigumu" anaanza kupiga kwa mikono yake yote miwili nzagamba analala chali kwenye tawi la mti anafumba macho kama amelala akisikiliza mziki.
" bado uko vizuri ungeendelea Sasa ungekuwa mbali" anaongea nzangamba baada ya kusikia kilinge ameacha kupiga macho yake yakiwa bado yamefumbwa.
" ningefanyeje kama mwalimu wangu amenikimbia"
" hukujua pakumpata"
kinapitakimya kifupi Kila mtu akiwaza lake moyoni.Kilinge aliyekuwa akijifunza kupiga kalimba kutoka kwa nzagamba wakiwa Kambi ya vijana miaka miwili iliyopita aliacha baada ya mafunzo ya mwisho yaliyomfanya nzagamba kujitenga nao na yeye mwenyewe kuwa na majukumu mengi kuonana kwao kukawa ni kwa nadra sana tofauti na zamani.
" mkeo hajambo" nzagamba anavunja ukimya
" hajambo,bado yupi kwao" anaongea akiendelea kuiangalia kalimba macho yake yanaenda kwa nzagamba na kuuliza
"vipi kuhusu wewe"
Nzagamba anamwangalia kwa kumtathimini na kujua anamaanisha nini lakini kwa sababu hataki kuzungumzia maada aliyokuja nayo rafiki yake anaamua kumpotezea.
" Mimi sijambo kama unavyoniona"
" unajua namaanisha nini nzagamba acha kunipindishia maada"
" nadhani utakuwa unajua najisikiaje kama unajua ninavyowaza"
" ndio maana umefanya binamu yangu Alie"
" naona kanisemea" anaamka na kukaa vizuri na kuendelea "usijali nimemuepushia matatizo mengi yatakayomfanya Alie zaidi maishani mwake akiishi na Mimi"
" hajaniambia tulya,sinde ndiye aliyeniambia kwani tulya alilia sana siku ile"
nzagamba anashangaa kusikia tulya alilia ' analia nini wakati Mimi ndio natakiwa kulia kwa kutumiwa na yeye' anawaza akimuona tulya wa ajabu zaidi.
" najua binamu yangu ni waruwaru sana" anatulia kidogo " lakini ni mwema sana sijapata kuona na ni mtu asiyejali watu wanasema nini,ndio maana aliposema anataka kuolewa na wewe nikajua atakufaa sana"
nzagamba anamwangalia rafiki yake kwa hasira.
" kwa kunitumia Mimi kukataa posa ya manumbu" Anacheka kidogo na kuendelea " sihitaji mwanamke atakayenimwagia maji ya baridi Kila siku asubuhi kunikumbusha madhaifu yangu maisha yangu yote, kwa kunionyesha ni jinsi gani alivyonionea huruma kwa kunifanya nionekane angalau mwanaume,pia sitaki kuwa katika mchezo wake huo wa kijinga nenda ukamwambie tena" anang'aka nzagamba.
" najua mahusiano yenu yameanza kama mchezo,kwani ni kweli tulya alikutaja siku ile kumfanya baba asimuozeshe kwa manumbu" anaongea kwa utaratibu kilinge kiasi fulani akimuelewa rafiki yake anavyojisikia kwani hata kama yeye angekuwa kwenye Hali yake angekasirika vilevile.
" lakini baada ya baba kuleta posa kwenu,ameamua kukubaliana na Hali halisi na kuukubali uhusiano wenu kutoka moyoni"
" atakuja atakaa na Mimi siku kadhaa Akala ndege akachoka akakimbia shida nini,Bora kumaliza mzizi wa fitina kabisa huku mwanzo"
" kwa nini usimpe nafasi,najua amekosea lakini kama nilivyosema sio mtu mbaya na kuhusu kukimbia sidhani kama atakimbia kwani hata hivi ninavyoongea atakuwa Yuko kwenye harakati zake za kujifunza kutengeneza vyungu" kilinge Anacheka kidogo akivuta taswira ya tulya akipambana na udongo nguo mpaka uso ukiwa umejaa udongo.
" kufinyanga vyungu?" anauliza nzagamba asielewe vyungu vya nini.
" Ili akiolewa asiilaze familia yake njaa" kilinge anazidi kucheka.
"nini?"anauliza tena kana kwamba hakumsikia kilinge.
" ndio maana nakwambia mpatie nafasi Nina uhakika hata kutelekeza na atakukubali jinsi ulivyo,namaanisha tayari ameshakukubali.siku ile umemwambia avunje uchumba mikono ilikuwa inamuuma mpaka vidole kutokana na kukanda udongo nadhani hiyo ilimuuma zaidi kuona anafanya kazi ya Bure mtu anayemfanyia hayo yote hajali"
nzagamba anabaki mdomo wazi.
" mmewahi kufikiria kuwa huwenda binamu yenu anamatatizo ya akili" anauliza na kumfanya kilinge acheke.Anashangaa kwani mambo anayoyafanya tulya mschana wa kawaida hawezi kufanya.
" ni mpambanaji tu sio kama ni kichaa,akiamua kitu mpaka aone mwisho wake huwa harudi nyuma,nikupe tu pole kazi unayo,sio mwanamke wa kawaida ndio maana nakwambia atakufaa nadhani anaweza kupigana na Dunia kwa watu anaowapenda"
nzagamba anamwangalia akimpima kilinge kama anamdanganya.
"isitoshe nyie wote mnamajeraha ya zamani ya kuumizwa na watu muwapendao"
" kivipi?"
" hiyo sio sehemu yangu kuelezea kama unataka kamuulize tulya mwenyewe " kilinge anaanza kushuka chini " naona umepata wengi Leo" anaangalia ndege aliokamata.
" tunaweza kuchoma wachache" anauliza akiwa chini nzagamba nae anashuka.
" utaweza kula ndege,wewe umezoea nyama pori"
"ndege Wana radha yake na nyama yake ni tamu tu hasa ya kuchoma"
" nisubiri hapo"
Nzagamba anaondoka na baada ya muda anarudi akiwa na Kuni anachukua mawe madogo mawili ambayo hutumia kuwashia moto mara nyingi akiwa hapa akitaka kuchoma ndege anakusanya Kuni na kuwasha moto baada ya muda ndege wanakuwa tayari wanakaa na kuanza kula.
Jioni hiyo nzagamba anarudi nyumbani na kumkuta mama yake akiendelea na kazi yake kutengeneza shanga za mwali,anamsalimia na kupita ndani,anajua kabisa mama yake hawezi kurudi nyuma kwa nafasi hii nzuri aliyoipata ya kumuozesha.
Anajitupa kwenye kitanda chake Cha kamba kilichotandikwa ngozi juu yake analala chali akiangalia dari kichwa chake kikiegemea mikono yake aliyoipishanisha juu na kuifanya mto anawaza mengi aliyoongea na kilinge mchana na kwa maelezo ya kilinge tulya sio mtu wa kuacha Mambo na Kuna mfano ambao hauko mbali nae mama yake mwenyewe.
kwa hiyo itabidi tu akubaliane na Hali halisi kwani Hawa wanawake wawili watafanya maisha yake kuwa magumu hivyo awe makini nao kwani tabia zao zinafanana.
Lakini je anampendaa? kujiuliza swali hilo anaamka na kukaa,kichwa chake akikiinamisha miguu yake ameikunja na mikono yeke ikiwa juu ya goti kwa Kila Mmoja.
taswira ya tulya inakuja akilini mwake ingawa alimuona kwa haraka siku ile na kutokana na hasira hakumuangalia vizuri lakini alimuona ni mrembo wa kutosha.
urembo sio kitu Cha muhimu tatizo ni upendo una uhakika umemsahau lindiwe nafsi yake inamuuliza na kujikuta mkono wake ukienda kichwani na kukuna nywele zake zilizojisokota lindiwe ni mwanamke aliyeuteka moyo wake mpaka Sasa ingawa anajikaza na kujisahaulisha lakini ndani ya moyo wake bado anampenda na hakutaka kuonyesha kwa watu kuwa amedhurika moyoni,je ataweza kuishi na tulya?
Anashuka kitandani miguu yake inampeleka kwenye Kona ya chumba hicho na kufunua chombo kilicho kama box lakini chenyewe kimetengenezwa kwa magome ya miti na Cha duara anaweka mfuniko wake chini anaingiza mkono na anatoka na bangili anarudisha mfuniko na kwenda kukaa kitandani akiiangalia bangili hiyo
" wewe nitakufanya nini" anaongea kwa sauti ya chini macho yake yakiwa kwenye bangili iliyopo kiganjani mwake na mkono wake mwingine ukienda kufuta chozi lililodondoka katika jicho lake Moja la kushoto.
Ikiwa imebaki siku Moja kabla tulya akae ndani, anaendelea kujituma kutengeneza vyungu vyake na Leo runde na sinde wanamsaidia kuvifunika vikiwa tayari kwa kuchoma ingawa havikuwa vingi vilimtosha kwa majaribio na sio kama alikuwa anauza au kubadilisha vitu kama walivyozoea wao kuita yeye amepanga kuvigawa na vingine kubeba nyumbani kwake kwa matumizi kwani vingine havikuwa na umbo zuri kwa hiyo Amna mtu ambaye angekubali kutoa vitu vyake kubadili na vyungu vibovu.
Baada ya kumaliza kupanga vyungu sinde na mama yake wanakaa chini ya kivuli Cha mti wakipumzika baada ya kazi ngumu.
" unaenda wapi" sinde anauliza baada ya kumuona tulya akitoka na kibuyu
" mtoni"
" na jua hili lote" anauliza runde
" unajua kuanzia kesho hamtaniruhu hata kushika hata kipeo zaidi ya kupumua nifanyeje Leo ndio siku yangu ya mwisho ya uhuru"
" Mimi nimechoka, wewe nenda tu mwenyewe" anaongea sinde akijilaza kabisa chini na kuwafanya tulya na runde kucheka
" kuwa makini,hatutaki kusikia bibi harusi mtarajiwa katumbukia mtoni" anaonya runde
" sawa"
anaitikia na kuondoka.
Akiwa njiani anakutana na lindiwe na marafiki zake wawili wametoka mtoni.' kwa nini nikutane nao Leo Hawa' anawaza baada ya kuwaona.lindiwe na wenzake wanamuona Wanaongea kitu na kucheka tulya anajua wazi kuwa wamemsema yeye lakini hakuwa kwenye Hali ya kuanzisha ugomvi sio mda atakuwa bibi harusi hataki kuwa na ngeu usoni au kovu lililotokana na Mambo ya kijinga hivyo anaamua kuachana nao.
" habari zenu" anawasalimia akiwapita lakini inavyoonekana lindiwe na wenzake hawakuwa radhi kuachana nae.
" nani huyo,kama sio mama ndege" anaongea Mmoja na wote wanacheka ' mama ndege?ndio wameamua kuniita hivyo' anawaza tulya na kuvuta pumzi ndefu kuzuia hasira lakini kina lindiwe bado hawakutaka kumwacha.
" hiyo ndio hadhi yako,huyo nzagamba asiye na kitu kwa mtu kama wewe unayetolea macho waume za watu anakufaa" lindiwe anaongea na kumfanya tulya kukosa uvumilivu na kuwageukia akimwangalia lindiwe.anawaza atamsemaje mtu vibaya namana ile hataka kama wameachana kwa nini asiheshimu uhusiano wao wa zamani waliowahi kuwa nao.
" kuwatolea jicho waume za watu?" anatulia kidogo na kumsogelea lindiwe " kwa ninavyokumbuka mumeo ndio kaangukia pua kwangu na nasikia analewa kama mbwa huko sababu nimemkataa na nadhani atakuwa hata hakuoni huko ndani sababu yangu,kwa hiyo unavyoongea uwe unahakikisha kunyoosha sentensi vizuri mtu akitusikia huko atajua Mimi namkimbilia mumeo" tulya anampa kinachouma lindiwe na uso wake ukisawajika kwa aibu na hasira .
" unasemaje?"
" kama ulivyosikia,na kuhusu nzagamba ni mara mia ya huyo mumeo hata kama hana kitu kuliko huyo anayekufanya ngoma"
" tumpige huyu hatujui sisi" anaingilia rafiki yake
" thubutuu! una uhakika mtaniweza?" anauliza tulya kwa kujiamini moyoni akipiga mahesabu wakimchangia Hawa watampiga hivyo afanyeje kujihami,na kuwakimbia hawezi sababu watamzoea.
" sisi tupo watatu wewe uko peke yako kwa nini tusikuweze" anaongea mwingi na tulya kucheka kwa nguvu.
" mna uhakika huo,mmeangalia kwanza kati yetu nani atapata hasara" anaongea akiangalia vibuyu vyao kichwani na wote wanagundua anawaza nini na anaendelea
" na kingine wewe lindiwe huwezi hata kuongea mwenyewe mpaka watu wakusaidie Sasa nimejua kwa nini mumeo anakutafutia msaidizi" anamchochea lindiwe Ili ugomvi upungue mtoano ubaki fainali na anafanikiwa.
" msiingilie huu ugomvi wangu" anajibu lindiwe na tulya kutabasamu kumpatia.
" sikia" anaongea lindiwe anatulia kidogo na kuendelea " ninavyoona wewe ndio mwenye shida zaidi,kwani huyo nzagamba ananipenda Mimi mpaka kesho na huwezi kubadili hilo utaenda na kukaa kama gunzi likisubili kukokwa moto tu" lindiwe nae anampa kinachouma lakini tulya anawahi na kurudi katika Hali yake ya kawaida.
" mmmh,najua hilo na usijali nitalishughulikia kwa sababu ya kale Yanasahaulika na gunzi Lina kazi nyingine pia kama mkono haufiki mgongoni tumia gunzi kujikuna liko vizuri kweli" anatulia kidogo kumwangalia lindiwe kama mvua ya mawe imemfika
" jionee huruma wewe kwani mumeo ananipenda Mimi na huyo nzagamba nitahakikisha kakusahau kabisa kwani kesho haitabiliki"
lindiwe anazidi kupandwa na hasira wakati akijaribu kurudi kundini tulya anaamua kuachana nao akiona ugomvi hauna radha " samahani inanibidi kuondoka kwani Leo ndio siku yangu ya mwisho kukaa nje kesho naanza kuwa mwali mnakaribishwa Kuja kutwanga mahindi na mtama hasa nyie" akiwaangalia marafiki zake lindiwe " pumba zitakuwepo za kutosha mje mpake mlainishe ngozi maana zimekomaa sana,wanaume zenu waangalie wanawake wengine muanze kulaumu" anaanza kuondoka.
" ndio tumwache hivi anatutukana" anaongea rafiki yake lindiwe.
" muacheni,ila nitahakikisha namlipa kwa alivyonidhalilisha Leo labda Mimi sio lindiwe" anaongea akimwangalia tulya aliyewapatia mgongo akiondoka.
Mtoni tulya anafika anachota maji anaweka kibuyu pembeni ya mto na kwenda kukaa chini ya mti.lengo la Kuja mtoni Leo ni kuongea na nzagamba kurekebisha uhusiano wao na kumpa jibu kuwa hatavunja uchumba kwani akikaa ndani itakuwa ni vigumu kuonana nae, na hataki akiolewa waanzie pabaya anataka kurekebisha mambo.baada ya kufika mtoni na kutokusikia sauti ya kalimba anajua atakuwa hajafika hivyo anaamua kusubiri kidogo.akiwa chini ya mti anakumbuka maneno ya lindiwe roho yake inamuuma na kujiuliza huenda kweli nzagamba bado anampenda lindiwe ndio maana anakataa kumuoa yeye.
Anajiuliza ataishije na mwanaume asiyempenda kwani macho ya nzagamba yanaonyesha chuki dhahiri.' nimlaumu nani nimejitakia mwenyewe kumtumia kumkataa manumbu' anawaza.Lindi la mawazo likimzunguka anashtuka mtu akimshika bega anageuka na kunyanyua uso juu anashtuka na kusimama haraka haraka.
" wewe unafanya nini"