Mama akaelekea hadi kitandani kuketi na hakuacha kuona koti alilokuja nalo binti yake likiwa chini ya mito miwili iliyokuwa kitandani!
Aretha akajiwahi kukaa karibu na ile mito akijaribu kumziba mama yake asilione lile koti,
"Retha, nimeshaliona, niambie ni la nani?" Mama akamwambia huku akimtazama kwa jicho la upole...
Kwa namna Aretha alivyoshtuka mama yake akatabasamu na kunyoosha mkono wake uliolivuta koti.
"Mm..a..mama..jamani" Aretha akapata kigugumizi cha ghafla...
"Mwanangu wala usione aibu, natamani tu kumfahamu mwenye koti hili, ni la Derrick?"
"Hapana mama...sio Derrick." akamkatalia kwa haraka
"Niambie binti yangu" mama akamwambia kwa kumsihi mwanae maana alitamani kujua
Akashusha pumzi kwa nguvu kisha akaanza kumwambia, "mama hivi unafahamu Derrick ni mdogo wa Edrian Simunge?"
"Hapana sikujua kabisa, maana Derrick hakutaja jina la Simunge wakati alipojitambulisha" Mama akajibu kwa mshangao..
Aretha akamsimulia jinsi walivyofika na hadi Edrian akamrudisha..
"Retha.... unampenda Edrian?" Mama akamshtukiza binti yake...
Aretha akatikisa kichwa akikataa huku akimlalamikia "mama aaaah unataka nini?"
"Mwanangu mimi ni mama yako... nakujua... ni aidha Derrick au Edrian?"
"Aaaarghh... Mama nataka kulala.." Aretha akaamua kukimbia mahojiano na mama yake sababu alimjua hataweza kumpa nafasi kwa kuwa ni mara ya kwanza ameonesha udhaifu kwa mwanaume.. Siku zote mama yake amekuwa akimlazimisha kuwa na urafiki na watu wa jinsi zote mbili kitu ambacho Aretha hakuwa anapenda.
Mama yake alimsisitiza wakati wote kwa sababu ya changamoto ambazo Aretha alikuwa nazo alipokuwa mtoto... Aretha hakupenda sana kuchangamana na watu sababu aliwahi kuwa mhanga wa udharirishaji kutoka kwa wanafunzi shule aliyosoma. Akiwa binti mdogo alisumbuliwa sana na kigugumizi, udhaifu huu ulichukuliwa vibaya na wengine, walimdhihaki hata kumcheka kila mara alipotaka kuongea. Aretha aliamua kuwa peke yake wakati mwingi. Alighairi kuwa na marafiki japokuwa kuna watu walijitahidi kuwa karibu naye.
"Kabla hujalala niambie hili koti unalirudisha lini au amekupatia liwe lako?"
"Ma..Mama" akafungua uso wake
Mama yake akamtazama binti yake na kutabasamu..." Niambie nikuache ulale"
"Kesho mama" akajibu kwa sauti ya chini..
"Hautalipeleka, ataliijia mwenyewe. Nimemaliza" mama akainuka na kuondoka na lile koti...
"Mama aaaaah unapeleka wapi koti la.la watu" akashusha pumzi akimuangalia mama yake akiondoka chumbani na lile koti..
Akajitupia kitandani na kushusha pumzi. Mama kwa upande wake akaenda chumbani na kuliweka koti kwenye kishikio nyuma ya mlango..
"Oooh Mungu wangu...msaidie mwanangu awe kwenye mikono sahihi" akanong'ona taratibu..
Akapanda kitandani na kulala japokuwa alitamani kumjua huyu Edrian! Akaamua kumtafuta Derrick kesho tu atakapoamka...
Na ndivyo alivyofanya...
"Hellow mwanangu Derrick!"
Baada ya salamu, mama Aretha akamuuliza Derrick kuhusu Edrian...
"Na kwa nini hukuniambia kama unatoka kwa Simunge?"
Derrick akashusha pumzi akijiuliza nini kilitokea baada ya Ed kumrudisha Aretha,
"Nisamehe mama, sikupenda kutumia hili jina maana linafahamika sana..."
"Derrick hutaniongopea mwanangu eeeeh, Niambie ukweli, kwa namna ulimfahamu binti yangu. Naomba ukweli tu mwanangu" mama alimsihi kwenye simu kiasi Derrick akajisikia kujihukumu kwa kile alichofanya..
Akaanza kumsimulia hatua ya kumuona Aretha kwenye kipindi cha Tv hadi alivyomfuatilia na kwa nini alitaka aende naye kwenye sherehe...." Mama niamini haya yote tunafanya kwa sababu tunampenda kaka na pia kwa upande wangu Aretha ni mwanamke mwema kwa ajili ya Ed." Hakumwambia kuhusu Joselyn kabisa.
Mama alibaki mdomo wazi akishangazwa na jitihada za Derrick. Kitu cha ajabu zaidi Aretha kushiriki kipindi cha TV ulikuwa ni mshangao mkubwa kwake.. akahisi kuna kitu zaidi kwa Aretha ambacho anahitaji kukifahamu.
Mwanangu, unamuamini kaka yako kwa ajili ya Aretha au unaongopa?" Akauliza mama
"Mama, si tu kwa sababu ni kaka yangu bali ni mtu ninayemfahamu kuwa akisema kitu yuko tayari kuupindua ulimwengu wote akipate kile anachotaka!" Derrick akamtetea kaka yake. Ni damu moja.