Safari ya kuelekea nyumbani kwa Aretha iliendelea taratibu, huku mawazo ya Ed yakiwa huku na kule. Hakuelewa kwa nini alikuwa akijisikia kama mwenye uzito fulani hivi!
"Oooh God please help me, huyu mama ananitisha sana."
"Ed tulia...hakuna baya lolote litatokea, anamjali binti yake tu" alijisemea moyoni kila mara alipohisi hofu. Kwa nini amkataze kurudisha koti lake na alifuate mwenyewe ni jambo lilimtia shaka sana Ed.
Macho yake yakiwa barabarani, hakusahau kuangalia kama lile gari aliloliona linaweza kuwa linamfuatilia au la. Alipoangalia mara kadhaa kwenye kioo cha pembeni hakuweza kuiona. Akaamua kumuachia Captain suala hilo.
Akafika mwisho wa safari yake, mbele ya geti la nyumba ya akina Aretha. Akashusha pumzi kabla ya kushuka kwenye gari, hakutaka kupiga honi akiamini si heshima. Akapiga hatua kuelekea kwenye mlango mdogo, akasita kidogo kisha akagonga mara mbili akasubiri. Sekunde kadhaa zilipita akaamua kugonga tena na kusubiri, akafikiri kumpigia Aretha kumwambia yuko getini tayari, aah akalisukuma hilo wazo pembeni baada ya kukumbuka maneno ya mama yake atakuwa chuo..arghhhhh.. akatuliza tena akili. Akainua mkono kutaka kugonga akasikia hatua kwa ndani zikielekea getini
"Nakuja mwanangu" sauti ilisikika kwa ndani.
Mapigo ya moyo ya Ed yaliongezeka, akarudi hatua tatu nyuma na wakati huo geti lilifunguliwa, mbele yake akasimama mama wa makamo ambaye tabasamu lake lilimfanya afikiri anamuona Aretha mbele yake.. akarudisha tabasamu kwa mama huyu..
"Karibu mwanangu na pole kuchelewa kukupokea..nilikuwa bustanini kuangalia mboga" mama huyu alifululiza kuongea
"Ah..hapana shida mama...Asante. " Ed alijibu huku akiwa amesimama pale pale
"Mbona mmesimama mwanangu karibu ndani" mama akasema huku akisogea pembeni kumpisha Ed ambaye hakujua afanye nini, picha aliyokuwa nayo kichwani ilikuwa ya kupewa koti na kuondoka. Akatoka kwenye mshangao na kusema
"Aaah...Asante.. .mama, naomba nizime gari" akageuka kuelekea alipoegesha gari lakini mama huyu akamwita
"Mwanangu.... hebu subiri nifungue geti ili likae ndani, ni salama zaidi"
Haaaaaaa ndio mara ya kwanza amefika na afunguliwe geti, mama akamchanganya Ed zaidi akiangusha kila wazo aliloliwaza..
"Sawa....mama" Ed akajibu na kuingia kwenye gari..
Mama huyu akaingia ndani na kisha akafungua geti kubwa, katika umri wake akahangika kidogo kulisukuma hata lilipofika mwisho akampa ishara Ed aingie huku akimuonesha sehemu ya kuegesha.
Ed akafanya kama alivyoelekezwa na alipohakikisha ameegesha vyema akashuka na kumfuata mama ambaye alisimama kwenye baraza dogo la mlango wa kuingilia.
"Pole kwa usumbufu mwanangu karibu ujisikie nyumbani" mama huyu aliongea na kuachia tabasamu lake ambalo hakujua kwa kiasi gani Ed analihusudu sababu lilifanana na la mwanae.
"Asante mama...nashukuru" Ed akajibu huku akivua viatu na kuingia ndani. Alipoingia sebuleni akavutiwa moja kwa moja na picha iliyokuwa ukutani iliyoonesha kuwa ni ya familia.
Akaketi kwenye kochi lililokuwa likitazama na ubao uliobeba picha mbali mbali.
"Mwanangu kuna juisi na maziwa nini utapenda?" Mama akamuuliza tayari akiwa amesimama kuelekea jikoni
"Aah..Maziwa mama" Ed akamjibu. Acha aone mwisho wa suprise hii maana alikuja akijua atapewa koti na kuondoka lakini matokeo yake yuko ndani kwao Aretha. Duh!
"Baridi au moto?" Mama akauliza na kumfanya Ed kuachia tabasamu zaidi maana aliona ukarimu wa mama huyu umeshinda wasiwasi wake..
"Baridi mama" hakutaka kumsumbua mama huyu akachemshe
"Nakuja sasa hivi mwanangu"
Akaingia jikoni huku Ed akibaki sebuleni akiangaza macho kwenye picha alizoziona mara alipoingia. Sebule hii haikuwa ya ghali sana lakini ilivutia kwa mpangilio wake wa makochi, meza ndogo iliyowekwa kati. Pembeni kulikuwa na kabati lililobeba vitabu na pembeni meza nyingine iliyobeba mtungi wa maua. Ukuta mfupi mdogo ulitenganisha ukumbi huu na ule wa chakula. Karibu na mlango ulioingia vyumbani kulikuwa na meza nyingine ilikuwa na kikapu kidogo kilichonakshiwa na rangi tofauti zilizovutia.
Mama akarudi na glasi ndefu na chupa ya maziwa iliyoonesha kuwa ilitoka kwenye jokofu.