Chapter 49 - MSHTUKO

Akarudisha macho yake kwenye zile picha kuna picha ilimvutia.. ya binti mdogo wa miaka 12 aliyesimama peke yake. Sura yake ilikuwa kama alishawahi kuiona lakini bado hakuwa na hakika.

Akashusha pumzi na kumwangalia mama yake Aretha ambaye hakukwepesha macho hata mara moja..

"Mwanangu nimekupa jukumu zito?"

"Hapana mama, nashukuru kuniamini" Ed alimjibu mama yake Aretha kisha akaendelea.... "mama naomba niondoke"

"Hamna shida mwanangu, asante sana kuniheshimu na kuja. Kitu kingine naomba Retha asijue haya tuliyoongea. Yabaki kati yetu" mama huyu alimsihi Ed huku akiinuka kuchukua glasi

"Sawa. Nitafanya hivyo" Ed akamhakikishia

Akapeleka glasi jikoni, Ed shauku yake ikazidi hiyari yake, akasogea mpaka kwenye ubao wa picha akaangalia na kuona watu tofauti kwenye picha. Akamwangalia yule binti kwenye picha sura ikaja ya Aretha akatabasamu japokuwa kulikuwa na utofauti kidogo

"Umemtambua huyo?" alishtuliwa na sauti ya mama Aretha

"Kidogo anamfanania Aretha....ni yeye?

"He he he usijali mwanangu utamfa...." hajamaliza alisikia geti likifunguliwa kwa funguo..

"Amerudi huyo.... ngoja nikuletee koti lako" mama huyu akapiga hatua za haraka kuelekea kwenye mlango ulioelekea vyumbani. Ed akabaki amesimama huku akisikia hatua za haraka zilizokuwa zikielekea katika mlango alioingilia...

Moyo wake ukapata fukuto la furaha kuwa atamuona Aretha..

Akageukia ule ubao wa picha na kuendelea kuangalia ili asionekane alikuwa akimsubiri... kitasa cha mlango kikafunguliwa taratibu na sekunde kama ishirini zilipita pasipo mtu kuingia. Ed akageuka akashangaa hamna aliyeingia ila mlango ulikuwa wazi kwa sehemu ndogo... Ed akapiga hatua kuangalia nani alifungua, alipofika na kutoa kichwa akashangazwa..Aretha aliegama kwenye ukuta huku akiwa amefumba macho

"Hauna mpango wa kuingia ndani?" Akauliza, Aretha alishtuka hadi akajigonga katika mtungi wa maua uliokuwa pembeni yake

"Oooh..sssh.. a aamh...hapana.... nilikuwa navua viatu" katika maumivu ya kujigonga akajikaza kujibu...

"Pole. .. hujaumia?" Ed akauliza akiwa amepiga hatua kumsogelea Aretha ambaye aligonga mguu wake kwenye mtungi uliopandwa maua...

"Niiniiko....sssawa.." alipata kigugumizi kujibu maana Ed tayari alikuwa amepiga goti kumwangalia mguuni alipojigonga.

Ed akainuka na kumwangalia,

"Samahani naona nimekushtua..sikukusudia"

"Hapana. ..nnniko salama..kkaribu" Aretha akamjibu huku macho yake yakiangalia kwingine isipokuwa usoni kwa Ed..

"Asante...japokuwa ndio naondoka, habari ya jioni?" Ed akiwa amesimama hakuondoa macho yake usoni kwa Aretha, mwanga wa taa iliyomulika pale barazani ulimwezesha vyema.

"Ssalama....mama hajakupatia koti?"akauliza Aretha

"Anani...." kabla Ed hajamaliza sauti ilitokea nyuma yake

"We Retha huku nje unafanya nini badala ya kuingia ndani?" Mama yake akamuuliza

"Mmh..aaah nni..." kabla hajatengeneza sentensi mama yake akamuwahi

"Haya msindikize mgeni maana umeona ubaki nje akufuate"

"Aargh mama... hapana... nime. ..." akalalamika Aretha

"Haya. ...assssh...msindikize" akamwambia huku akimkabidhi koti Ed

"Mwanangu koti lako liko salama, nashukuru kuja kuniona...wakati mwingine tutaongea zaidi" Ed ambaye alikuwa na tabasamu usoni baada ya kutazama mama na binti yake wakibishana.. akapokea koti

"Sawa mama....Asante sana. Karibu nawe nyumbani" wakati anayasema maneno haya Ed akaelekea alipovua viatu...

"We Retha hebu msaidie koti avae viatu" mama akamsukuma kidogo Aretha ambaye alifumba macho kuonesha uchokozi wa mama yake umemzidia

Akasogea alipokuwa Ed, ambaye wakati huu aliachia tabasamu kuonesha anaelewa usumbufu ambao mama anampa binti yake. Akampa koti na kuvaa viatu...alipomaliza akainuka na kuchukua koti mikononi mwa Aretha...

Ed alimshukuru mama na kuelekea alipoegesha gari na wakati huu ilibidi Aretha akafungue geti ili atoke. Alipohakikisha gari imetoka nje, bado hakukaa kwenye gari akashuka kumshukuru Aretha..."lazima nimuone kabla sijaenda" aliwaza Ed. Aretha alipomaliza kufunga geti akadhani Ed ataondoa gari moja kwa moja.. Akafungua geti dogo kuchungulia... alikutana ana kwa ana na macho ya Ed ...