Chapter 38 - UNA HAMU

Joselyn alipomaliza kusema maneno nayo akamwangalia Ed usoni, na wala hakuficha jitihada zake za kujaribu kumvuta Mrs Simunge upande wake. Aliachia tabasamu na kuendelea kula, akimuacha Ed katika kidimbwi cha mawazo, na sio yeye pekee lakini Derrick, Coletha na Li waliona kama maombi yao yamekosa majibu. Hawamkubali Joselyn lakini tayari kashatanua mabawa yake kuruka na kaka yao.

Mama yao aliangalia yote yaliyoendelea na akachagua kunyamaza pasipo kuuliza chochote ili kufanya chakula kiwe cha amani. Walipokuwa karibia na kumaliza pale mezani, mama akamwangalia Aretha ambaye kichwa chake kiliinamishwa chini karibia kila wakati

"Derrick hujui kutambulisha wageni we mdogo eeeeh!?" Mrs Simunge akataka kumfahamu huyu binti ambaye hakujua ni mgeni wa Derrick au Edrian

"Oooh mama, una haraka sana, au una hamu ya mabinti wengi" Derrick akamtania mama yake ambaye alicheka

"Kama ni binti yangu fanya haraka nimfahamu..

"Mama" Coletha akamtolea jicho mama yake kumuonesha wanamjadili mtu aliyeko mezani...

"Shhhhh....hawa ndugu zako wanataka nisipate wajukuu"

Derrick akamwangalia Edrian ambaye alikuwa kama kapigwa radi akimwangalia mama yake. Alimjua vyema na maneno kama yale hayakumshangaza, shida ilikuwa kile Derrick atakachokisema akihofia kufadhaishwa ikiwa uhusiano wa wawili hawa utakuwa wa wapenzi.

Aretha ambaye sasa alihamisha macho yake na kumwangalia Derrick kwa namna ya kumuomba amalize sakata hilo na anataka kuondoka...

"Mama, kutana na rafiki yetu" jinsi Derrick alivyolikazia neno 'yetu'. . Kulimfanya Aretha kugeuza macho na kumwangalia huku Edrian akimwangalia yeye..

Akaendelea, "Anaitwa Aretha"

Coletha ambaye muda huu alikuwa akimwangalia kaka zake, Edrian na Linus, akahisi kuna kitu kinaendelea na yeye hakijui. Alipomwangalia Aretha akamuonea huruma, maana alijua hajazoea mambo ya familia yake...

"Aretha, karibu sana binti yangu, unasoma na huyu Derrick?" Mrs Simunge akamuuliza Aretha ambaye alikuwa akifinyanga vidole vyake..

"Hapana mama, hasomi na mimi" Derrick akawahi kujibu na akataka kuendelea mama yake akamkatisha..

"Derrick muache binti wa watu ajieleze mbona unasumbua jamani"

"Hapana mama, sisomi naye bali nimefahamiana naye tu..." sauti ya Aretha ilikuwa ya chini na iliyoonesha kutulia. ..

"Oooh sawa. Unasoma au unafanya kazi?" Mama akaendelea na maswali

"Mama, panga muda muonane uulize jamani utamchosha mgeni wangu" Derrick akamwambia mama yake. Ed ambaye muda wote huu alikuwa kama hayupo, akainua macho kumuangalia mama yake....

"Aretha binti yangu ni sawa eeeh? Karibu Jumamosi. Utakuwa umenisaidia maana wanangu wenyewe wameniacha niwe huku peke yangu" akaweka tabasamu laini na kumgeukia Aretha ambaye wakati huu macho yake yalikuwa kwa Derrick kumlilia amsaidie

"Mama, nitamleta Jumamosi..muda gani Retha?" Aretha aliona ngome yote ya utetezi ikiporomoka, akageuka upande wa Ed na akakutana na Edrian ambaye hakujaribu hata kumuangalia maana hakika alianza kufurahia mambo alivyokuwa, japokuwa alibaki kizani kuhusu aina ya uhusiano na mdogo wake.

"Sawa mama. Nitakuja mchana" Aretha akatoa sauti yenye kuonesha kukubali matokeo.

Joselyn ambaye muda wote aliangalia mambo yalivyoenda... akaamua kuongea..

"Basi tutaungana sote mama. Jumamosi sina ratiba ya kazi. Nitakuja! " Derrick na Li walijikuta kwa pamoja wakimuangalia Ed wakitegemea aseme kitu. Ukimya ule wa Ed ulimshtua Coletha na kuamua kuingilia kati..

"Na mimi nitakuja mama, tuwe na chit chat yetu ya wanawake eeeeh" alimuuliza mama yake huku akimpa ishara akubali kitu ambacho alifanya.

Aretha akainuka taratibu akamuomba ruhusa mama yule aweze kuondoka, huku ghafla Ed pasipo kuelewa alishangaa amesimama na kufanya ndugu zake kumwangalia, Derrick akainuka.

"Bro naomba kama unaondoka sasa hivi uongozane na Retha mie natamani kuendelea na mama hapa?" Wazo hili la Derrick lilikuwa kama sukari kwenye chai kwa Li maana alifurahia kiasi angepata makofi.

Wakati Li akifurahia, Ed alimwangalia Derrick na hakuweza kuamini kama mdogo wake huyu anaweza kuwa mtundu kiasi cha kubuni njia za kuwaweka pamoja..