Mwaka 2020, kulikuwa na majina makuu manne Tanzania; Leah Shahidi, Suzanne Depo, Janat Marko na Annabella Majimbo. Wanawake hawa wanne walikuwa wenye mafanikio makubwa sana katika sekta zao, kitu ambacho kiliwapa umaarufu mkubwa sana nchini, na nchi za jirani.
Leah Shahidi - Mwandishi wa vitabu vya watoto. Nyumbani, Leah alikuwa ni mke wa Paul, mwanasheria na profesa wa chuo kikuu cha Dar es salaam. Katika miaka yao yote kumi ya ndoa hawakubarikiwa mtoto. Ingawa Leah alivaa uso wa ushujaa, jambo hilo lilikuwa likimuuma sana.
Suzanne Depo - Mwanamitindo. Mwaka 2015, jina lake lilikuwa miongoni wa wanamitindo maarufu zaidi Africa. Hakuwa ameolewa, na wala hakuwa na mpenzi. Alipenda kusema ameolewa na kazi yake na ni ndoa ambayo haitakuja kuvunjika kama ndoa nyingine.Â
Janat Marko - Mmiliki wa JM Pharmaceuticals. Mwaka 2018 hadi 2020 mfululizo alipokea tuzo za mwanamke bora kutoka kwa raisi wa Tanzania kwa jinsi alivyoweza kusaidia wanawake na mabinti wengi nchini. Kwenye swala la mahusiano, Janat hakuliweka wazi.Â
Annabella Majimbo - Mmiliki wa Space Hotels and Resorts, hoteli zenye hadhi ya kimataifa nchini Tanzania. Hoteli zake zilipatikana Dar es salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, na Zanzibar. Annabella aliolewa akiwa na umri wa miaka 18 na mwanaume aliemzidi miaka 25. Katika mahojiano mbalimbali aliyoyafanya, alisema kuwa mume wake hakuwahi kumtesa na alimuonesha mapenzi ya kweli ambayo mwanaume yoyote hatoweza kufikia. Mwaka 2000 mume wake alifariki kwa ajali ya ndege.
Hawa ndio wanawake wanne waliovunja tamaduni na kufanikiwa kwenye dunia iliyowapa kipaombele wanaume. Wadada wengi walipata motisha ya kufanikiwa kama wao. Changamoto na mafanikio yao yalihamasisha wengi. Hawakuwa na doa; lakini hayo ni watu waliyokuwa wakihisi wanajua. Ukweli ulikuwa umejificha mbali na umma.
Â
 ***