Chereads / THE JOKE / Chapter 2 - CHAPTER 1

Chapter 2 - CHAPTER 1

Macho ya Leah hayakutulia akiwa ndani ya ofisi ya daktari wake wa uzazi. Moyo wake ulijaa uwoga. 

Je, daktari atakuja na jibu gani? Nikiwa na tatizo je? Eh Mungu nisaidie.

Mawazo hayo yalitapakaa akilini mwake, na hakuna hata wazo moja lililompa auheni. Baada ya muda mfupi, daktari alirudi ofisini kwake akiwa ameshika faili. Sura ya daktari haikuwa hata na tone la habari njema. Daktari aliketi kwenye kiti chake na kuvuta pumzi.

"Nipo okay, doctor?", aliuliza Leah,

"Leah, ultrasound imeonesha kuwa una Endometriosis.", alisema daktari, "Huu ni ukuta unaojijenga kwenye kizazi chako ambao unafanana na ukuta wako wa asili. Kazi yake ni kuzuia yai lako na mbegu za kiume kukutana na kutunga mimba.", 

"Endometriosis? Kwahiyo unasema kuwa sababu ya mimi na mume kushindwa kupata mtoto miaka yote hii ni mimi?",

"Ndiyo. Na inaonekana kuwa tatizo limeshakuwa kubwa hivyo tiba itashindikana.",

Leah aliangua kicheko cha ghafla, ila hakikumshitua daktari kwani hakikuwa kicheko cha furaha. Kilikuwa ni kicheko kilichobeba mkusanyiko wa hisia zote mbaya. Machozi yaliteremka mashavuni pa Leah bila kujijua.

Daktari alimsogezea boksi la tishu, "Kuna njia nyingi za kupata mtoto, Leah. Ila hapa nchini hatuzifanyi. Njia hizo ni _",

"Doctor, stop.", Leah alifuta machozi, "Hizo njia nyingine nazijua. Ila mimi nilitaka nimbebe mwanangu kwenye tumbo langu miezi tisa, nimzae mwenyewe kwa uchungu.",

"Hata ukibebewa mimba na mtu mwingine, bado yule mtoto atakuwa ni wako kwasababu ni yai lako na mbegu ya mume wako ndizo zilizotumika.",

"Sitajiona mama niliyekamilika, doctor.",

Leah alibeba mkoba wake na kunyanyuka. Mtu hakuhitaji miwani ya ajabu kuona maumivu aliyokuwa akiyasikia moyoni. Ilikuwa wazi kama anga. 

"Asante doctor.", alisema Leah na kuondoka.

Hakuna daktari anayependa kumpa mgonjwa wake habari mbaya. Kitendo kile pia kilimuumiza daktari yule.

Kikao hakikuwa kimeenda jinsi Suzanne alivotaka. Alikusanya wanamitindo wake bora kwenye ofisi yake. Ukimya ulitawala huku akizunguka meza moja baada ya nyingine kukagua michoro iliyowakilishwa na wafanyakazi wale. Kwa mbali ofisi ile ilifanana na chumba cha mtihani, na kila mwanafunzi alihofia kupata sifuri. 

Suzy alijulikana kama bosi asiye na huruma kipindi cha ukaguzi. Hakusita kutamka neno lolote alilofikiria, hata kama litakwenda kuvunja moyo wa wafanyakazi wake. Hivyo wanamitindo walijitahidi sana kuwakilisha michoro isiyo na kasoro.

Lakini bado Suzy hakuvutiwa na mchoro hata mmoja. Kila mchoro ulimfanya atikise kichwa chake na kuguna.

"Mbona kama mnaleta mchezo?", Suzy aliuliza huku akitembea, "Naona mmeanza kupoteza kipaji, si ndio?",

"Hapana boss!", wanamitindo walijibu kwa pamoja.

"Sasa mbona wote mnaniletea utumbo? Mnachora mishono ambayo haisisimui. Tena wengine mmeenda kuiga michoro from the internet. Mna mpango gani? Mnataka kuniharibia kampuni yangu au?",

"Hapana boss!",

"Nilipowaajiri niliona your talents and potential. Naona sasa mnataka kuniaibisha.",

Suzy alirudi kwenye siti yake na kuketi. Macho yake yalijaa hukumu akiwatazama. Wote walishindwa kumuangalia usoni. Walijua wamemuangusha.

"Nawapa siku tatu. Kila mmoja wenu aniletee perfect designs. Ukiiga sehemu, au ukiniletea design za kishamba nakufukuza kazi kwasababu itakuwa ni dharau. Nyie wote hapa mna vipaji vya hali ya juu. Msilete uzembe. Changamsheni akili. Tupo pamoja?", aliongea Suzy,

"Tupo pamoja, boss!", 

"Rudini kazini",

Wanamitindo waliondoka ofisini mule tena kwa haraka. Suzy alichukua simu yake na kupiga namba ambayo ameisevu kama Escape. Simu iliita kwa sekunde chache, na baadaye kupokelewa na mwanamume mwenye sauti nzito.

"Suzy hapa.", alisema Suzy kwa sauti ya kuamrisha.

"Ndiyo mkuu.", aliitika mwanamume yule.

"Amechora mshono wowote hizi siku mbili tatu?",

"Tunajitahidi kumshikisha kalamu na karatasi lakini amegoma kufanya chochote.",

"Mmejaribu kumnyima chakula?",

"Ndiyo ila bado haikumhamasisha.",

"Mmemuongezea kazi kama nilivyowaambia?",

"Kazi anafanya tena kwa bidii, lakini hachori.", mwanaume alijibu.

Suzy aliweka mkono wake shingoni na kuvuta pumzi nzito. Ilionesha kuwa ni kitu kilichomsumbua sana akili, na kumtia hasira, "Naweza nikaja weekend hii kumuona. Muandaeni vizuri.",

"Sawa mkuu.",

Suzy alikata simu na kuisukuma pembeni. Alisonya, "Naona unanitafuta, Flaviana.", alijisemea kimoyomoyo.

Leah alikuwa ndani ya gari, siti ya nyuma. Macho yake alikuwa ameyafumba lakini haikuwa usingizi. Mawazo mengi yalimjaa kichwani. Alitamani apige yowe ili apunguze yale maumivu, lakini maumivu ya moyo hayana tiba.

Dereva wake aliitwa Babra. Ukiachana na udereva, pia alikuwa ni sekretari wake. Babra alimfahamu Leah kama kiganja cha mkono wake. Kitu kikubwa ambacho alijua kuhusu Leah ni kwamba akiwa na mawazo huwa anapenda ukimya wa hali ya juu. Hivyo, ndani ya gari hakukuwa na redio wala muziki.

"Boss, unarudi ofisini au twende moja kwa moja nyumbani?", aliuliza Babra.

"Nipeleke nyumbani.", alisema Leah, macho bado yakiwa yamefungwa.

"Sawa boss.",

Babra aliendelea kuendesha gari kwa ukimya.

"Washa redio.", alisema Leah.

Ingawa ilimshangaza Babra, alifanya alichoambiwa. Dakika walikuwa wakisikiliza miziki. Zilipita kama dakika 15. Wakiwa barabarani, kwenye foleni, mziki ulikatishwa ghafla.

"Habari za mchana, watanzania.", ilisikika sauti ya kike kutoka redioni, "Kwa jina sitajitambulisha, na wala sitasema ninakaa wapi au nina miaka mingapi. Muikariri sauti yangu, kwani mtakuwa mkiisikia kila wiki kwa wiki nne zijazo.",

Taratibu, Leah alifumbua macho yake.

"Kwa miaka mingi nchi yetu, na hata majirani zetu wamewasujudu wanawake wanne. Najua mnafahamu ni wanawake gani nawaongelea. Tunawafahamu fika. Kila mtu anataka kuwa kama wao; Suzanne, Annabella, Janat na Leah Shahidi. Mnawaona ni watakatifu. Ila je, mnajua ni nini wamefanya mpaka wamepata mafanikio na umaarufu huu mkubwa?",

Babra alimgeukia Leah kwa haraka, "Boss, ni nani huyu?", aliuliza kwa wasiwasi.

Leah alitikisa kichwa. Hata yeye hakujua.

"Ndani ya wiki nne zijazo, tafichua siri ya kila mmoja wao. Sitaficha chochote. Lengo langu ni kuonesha dunia kuwa hawa mnaowaita malaika ni mapepo _",

Babra alizima redio kwa haraka. Leah alibaki kimya. Hakuonesha dalili yoyote ya mshangao. 

"Boss, twende makao makuu ya station yao! Hawawezi kuruhusu mtu kufanya _",

"Babra, achana nao.", Leah alisema kwa uchovu,

"Lakini boss _",

"Nipeleke nyumbani. Kichwa kinaniuma.",

Foleni ilianza kwenda na Babra alirudisha akili barabarani. Ukimya ulirudi tena ndani ya gari, na kichwa cha Leah kiliongezeka tatizo lingine.

...

Kabla siku haijaisha, mkurugenzi wa stesheni ya redio ya Faraja, Bwana Rajabu Balozi, alijiwa na ugeni. Wanawake watatu wenye nguvu za kipesa walitinga rasmi ofisini kwake. Ijapokuwa Bwana Rajabu alikuwa na pesa na umaarufu wa kiasi chake, hakuwahi kukutana na wanawake shupavu hawa wote. Hivyo hiyo ilikuwa ni siku yake ya bahati sana. Kwa bahati mbaya, ugeni wao haukuwa wa nia nzuri.

Suzanne, Janat na Annabella; hakukuwa hata na mmoja aliyekuwa na subira ndani yake. Ilikuwa ni dharura na hawakutaka kupoteza dakika hata moja. Kitu pekee kilichokuwa kinawasubirisha kilikuwa ni ujio wa Leah. Ujumbe uliorushwa kwenye redio uliwahusu wote wanne. Hawakutaka kuamini kuwa Leah hakutokea.

Kipindi wanasubiri, Bwana Rajabu alitumia umakini kuwatathimini. Wanawake wale walivaa mavazi ya bei na yenye kuvutia. Marashi yao yalikinzana na kufanya hali ya hewa ya ofisi kuwa mithiri ya bustani safi ya maua. Alivutiwa zaidi na Annabella. Ingawa umri wa wadada wale ulikuwa ukikaribia miaka arobaini, pesa na matunzo ziliwafanya waonekane wadogo zaidi.

"Ningependa maongezi yaanze. Sidhani kama Leah anakuja.", alisema Janat huku akiangalia saa yake ya mkononi.

"Mimi nachotaka kujua ni kimoja tu; huyu mtangazaji ni nani na naweza kumpataje?", aliuliza Suzanne,

"Na kwanini station imeruhusu kitu kama hichi kurushwa hewani?", aliongezea Annabella.

Bwana Rajabu aliwekwa mtu kati.

"Ndugu zangu, naelewa wasiwasi wenu. Lakini kwa bahati mbaya, sitaweza kuwapa taarifa za mtangazaji wangu.", Rajabu alijitetea.

"Why? Wewe unaona alichosema ni sawa?", aliuliza Suzy,

"Hii haihusiani na vilivyo sawa. Sisi tulio kwenye tasnia ya burudani lengo letu ni kukamata akili za wasikilizaji na watazamaji wetu. Habari kama hizi ndizo zenye soko sana nchini.",

"Funny.", Janat alitabasamu kwa kejeli, "Yani unaona ni sawa watu wasio na hatia wasulubishwe ili wewe upate pesa?", aliuliza,

"Ndio dunia inavyoenda.", Bwana Rajabu alijibu, "Nchi yetu imetupa uhuru wa kuongea. Pia hii ni ofisi na mimi ndiye mkurugenzi. Ndani ya hili jengo, mimi ndie mfanya maamuzi. Nyie hamna mamlaka.",

"What!", walishangaa kwa pamoja.

"Suzy, utajisikiaje nikija ofisini kwako nikiomba kumuhoji mwanamitindo alieshona gauni ya mke wangu eti kisa alipendeza sana na kila mwanaume alikuwa akimuangalia?", aliuliza Rajabu.

"Swali lako halina mantiki. Nina wasiwasi hata kichwani mwako pia kutakuwa na itirafu.", alisema Annabella.

"Mtangazaji wako ametuita mapepo na kusema kwamba tumepata umaarufu wetu kwa njia zisizo za halali. Hajui ni jinsi gani tumesota mpaka tumefika hapa tulipo.", alisema Janat kwa hasira.

"Dada zangu, kama njia zenu za mafanikio zilikuwa safi, kwanini mna wasiwasi?", Rajabu aliuliza kwa upole, "Hapa ofisini kwangu nina waandishi wa habari bora sana. Nje ya ofisi hii kila mtu anataka kujua historia kamili ya mafanikio yenu. Ndicho kitu tunachokifanya. Mtangazaji wangu hajakosea chochote. Punguzeni hofu.",

Maneno yake hayakuwapa afadhali, bali yaliwaongezea hasira.

"Wewe na wafanyakazi wako mmeanzisha vita.", alisikika akisema Suzy, "Na kwa mahesabu yangu ya harakaharaka, vita hii hamtaweza kushinda. Labda sio sisi mnaotuchezea.",

Suzy alinyanyuka na kuondoka kwa hasira.

"Kuwa makini sana, mkurugenzi. Ni vitu vidogovidogo sana vinavyoharibia watu maisha.", alisema Janat na kuondoka pia.

Annabella alinyanyuka taratibu na kubeba mkoba wake, "Endelea kumficha huyo mtangazaji wako. Ila mpe ujumbe huu; tutamjua tu. Awe makini sana na atachokiongea.",

Rajabu hakujibu kitu. Alimsindikiza Annabella kwa macho mpaka alipotoa mguu wake nje. Alipobaki peke yake, Rajabu alitoa leso na kupangusa jasho. 

***