Chereads / THE JOKE / Chapter 3 - CHAPTER 2

Chapter 3 - CHAPTER 2

Paul, mume wa Leah, alishuka kwenye gari lake na kuwahi ndani ya nyumba akitweta. Karibia nchi nzima ilikuwa imekwishasikia tangazo lile la redioni, na habari bado zilikuwa zikisambaa kwa kasi. Kipaombele chake kilikuwa jinsi mke wake alivyolipokea swala lile. Moja kwa moja alielekea kwenye chumba chao cha kulala. Na kama alivohisi, alimkuta Leah amejilaza kitandani, mkono wake ukiwa kwenye paji la uso na macho yake yakitazama dari.

"Mke wangu.", Paul aliita kwa upole.

Leah hakugeuka, "Nataka kuongea na wewe.", alisema kwa unyonge.

"Usijali mke wangu. Hili swala talifungulia mashitaka mahakamani. Station yao nzima itapigwa _",

"Siongelei huo upuuzi wa kwenye redio. Naongelea ndoa yetu.", Leah alinyanyuka na kukaa kitako huku akimtazama mumewe. 

Paul alipatwa na wasiwasi. Hakuwa na jinsi, bali kusikiliza.

"Nini kimetokea?", aliuliza.

"Leo nilienda hospitali kufanya check-up. Nina Endometriosis.", alielezea Leah.

Paul alishtuka. Hakuhitaji maelezo mengi. Alielewa ufafanuzi mzima wa ugonjwa ule, "Nimewahi kusikia huo ugonjwa. Matibabu yake _",

"Umri wangu umeenda. Matibabu yatashindikana.", Leah alimkatisha mume wake, "Ningekuwa nina miaka ishirini na kitu wangeweza kufanya upasuaji. Ila it's too late now.",

Paul aliketi pembeni ya mke wake. Alimshika mkono, "Naelewa maumivu unayoyapitia, mke wangu. Nipo pamoja na wewe. Kuna njia nyingine ya kupata mtoto _",

"SITAKI NJIA NYINGINE!", Leah alifoka. Machozi yalianza kutiririka tena, "Kila mtu anasema hivyo hivyo. Njia zote nazijua.",

"Mtoto atakuwa ni wa kwetu _",

"Hiyo sio tafsiri yangu ya mama.", Leah alitikisa kichwa, "Kwanini tupandikize mbegu zetu kwenye kizazi cha mtu mwingine? Huoni kama ni hatari? Mtoto wangu alitakiwa akulie kwenye tumbo langu mwenyewe, nipitie kila ugumu, kila hisia, kila kitu!",

"Lakini huwezi sasa, mama.", Paul alijitahidi kumtuliza.

Leah alivuta mkono wake kwa nguvu na kunyanyuka kitandani. Vidole vyake vilizama kwenye nywele zake. Alitembea mbele na nyuma, akilia. 

"Unajua nini kinaniuma?", Leah aliuliza, "Miaka yote hii nilidhani kuwa wewe ndie mwenye tatizo. Nilikuwa nikikuhukumu moyoni. Ni kama Mungu ameamua kuniadhibu.",

"Leah, mimi sijakuhukumu. Ndiyo, inaniuma, lakini najua wewe upo kwenye wakati mgumu zaidi yangu.",

"Why me?", Leah alilia zaidi, "Mbona nimeishi vizuri na watu? Sijawahi kuumiza mtu maishani mwangu. Kitu pekee nilichokuwa nahitaji ni mtoto. Sasa kuna point gani ya kuwa na pesa zote hizi na hakuna mtu wa kuzirithi?",

"Leah, usimkufuru Mungu. Yeye ana nia yake.", alisema Paul.

"Nia gani? Ya kuniumiza?",

"Mtoto anaweza akapatikana kwa njia yoyote ile. Sio lazima umbebe tumboni mwako miezi tisa. Kuna watoto wachanga wapo hospitalini bila mtu wa kuwajali. Labda kuna mtoto Mungu amemuandaa kwa ajili yetu, yupo hospitalini akisubiri siku tukutane.",

Leah alisitisha kutembea na kumtazama Paul, "Nahisi huelewi nachokisema.",

"Najaribu kutafuta ufumbuzi, maana according to you unaona familia yetu haijakamilika.", alisema Paul.

"Vitu vingine havina ufumbuzi.", Leah alianza kuondoka.

"Sasa unaenda wapi?",

"Naenda kulala chumba cha wageni. Bora niwe peke yangu kuliko kuwa na mtu asiyenielewa.",

Leah aliondoka chumbani. Paul hakujua ni kitu gani amesema ambacho ni kibaya. Alikuna kichwa. Hiyo haikuwa mara ya kwanza yeye kujaribu kutafuta ufumbuzi wa jambo fulani na mke wake kutokuonesha ushirikiano. 

Wote walikuwa na kazi nzuri pamoja na mali nyingi. Ila Leah alikuwa na kipato kikubwa sana kuliko yeye. Kuna muda Paul alikuwa akihisi labda hiyo ndiyo sababu inayomfanya Leah asimsikilize kama mke anavyopaswa kumsikiliza mumewe. Uvumilivu ulianza kumshinda.

Asubuhi iliyofuata ilikuwa tofauti na asubuhi nyingine. Leah hakuwa na nguvu ya kuishi siku mpya. Aliona kuwa kila kitu kilienda tofauti na matakwa yake. Lakini nafsi ilimsuta baada ya kukumbuka maongezi aliyofanya na mumewe usiku uliokwisha. Hakupenda kujishusha ila ilimbidi maana hakustahili kumalizia hasira zake kwa mtu ambaye hakuwa na hatia yoyote.

Alipoingia chumbani, alimkuta Paul akimalizia kuvaa nguo zake za kazini. Hali ya hewa ilibadilika baada ya macho yao kukutana. Leah aliingiwa na aibu.

"Sijapenda nilivyokuongelesha jana.", Leah alianza, "Forgive me.",

Paul alitabasamu, "Yameshapita. Leo ni siku mpya.",

"Umenisamehe?",

"Takusamehe kama ukinisaidia kufunga tai yangu.",

Kwa furaha, Leah alimsogelea mume wake na kumsaidia kufunga tai shingoni. Alipomaliza alimkumbatia mume wake bila kuongea kitu. Kwa Leah, Paul alikuwa ni kila kitu kwake. Hakupenda kumkwaza. Basi tu, binadamu hatujakamilika. Kwenye dunia yake, walikuwa ni wawili tu. Mume wake alimpa nguvu.

Akili imeumbiwa kusahau, hivyo Leah alipowasili kazini hakuelewa kwanini watu walikuwa wakimtazama kwa machale namna ile. Hakukumbuka tangazo la siku iliyopita la redioni. Hakulitilia maanani, kwani hakuona umuhimu wowote wa kulizingatia.

Aliingia ofisini kwake na kukuta Babra ameshamwekea kikombe chake cha chai mezani. Babra alisimama mbele ya meza. Leah aliketi na kuonja chai yake. Alitabasamu na kutikisa kichwa.

"Thank you.", alimwambia Babra, "Nipe ratiba ya leo.",

Babra aliwasha simu yake na kuanza kusoma ratiba ya Leah, "Utakuwa na kikao na mkurugenzi wa City Publishers leo saa tano asubuhi kuzungumzia uchapaji wa kitabu chako kipya. Saa nane kutakuwa na ufunguzi wa maktaba ya Agape Secondary School. Baada ya hapo saa kumi na moja jioni umealikwa kwenye chai ya jioni.",

"Nimealikwa na nani?", kwa mshangao, Leah aliuliza.

"Suzanne Depo, Janat Marko na Annabella Majimbo. Space hotel.", Babra alifafanua.

"Mwaliko unahusu nini?",

"Tangazo lililorushwa na Faraja station. Wanasema ni vizuri mkutane pamoja kutatua hili swala kabla halijawa kubwa.",

Leah alicheka kidogo, "Taangalia. Nikiwa nimechoka siendi.",

"Sawa boss. Niite ukiwa na shida yoyote.",

"Thank you, Babra.",

Babra aliondoka ofisini na Leah aliendelea na kazi.

***