Chereads / TUFANI YA MAFANIKIO / Chapter 5 - SURA YA NNE

Chapter 5 - SURA YA NNE

Mwezi wa kumi ukafika, wahadhiri na wanafunzi wa vyuo Vikuu ndiyo kumepambazuka. Masomo yakapamba moto, mara kwenye mihadhara, mara kwenye semina. Athalia na wenzake utawatambua kwani walijulikana kwa jina la yeboyebo, wanafunzi wa mwaka wa kwanza walijulikana kwa kushangaa mihadhara inavyoendeshwa, wanajiuliza hivi ndivyo mihadhara ilivyo mithili ya mahubiri! Walijipa moyo hivyohivyo lakini sasa shida kubwa ilikuwa ni maeneo ya kuendeshea mihadhara hiyo. Maeneo ni mengi mithili ya Mikoa na wilaya zote za Mafanikio, mara Gomeni, mara Chalini, mara Shimoni, PTC, Science buildings na Shalom kwa kutaja machache tu. Ama kweli kuku mgeni hakosi kamba mguuni, utawatambua tu mwaka wa kwanza kwa kuuliza maswali. Lakini kwa kuuliza kwao walifanikiwa, kwani wahenga husema "aulizaye si mjinga bali ataka kujua." Hayo ndiyo maisha aliyoishi Athalia na wenzake alipokuwa mwaka wa kwanza.

Athalia mwanzoni aliona kama masomo ni magumu katika kozi yake ya B.A Education (Bachelor of Arts with Education). Alijikuta katika somo la Fasihi ya Kiingereza (Literature) na Kiswahili lugha inayozungumzwa nchini Mafanikio kama haelewi vile. Alisoma sana alipoona wenzake wanaandika sana alihisi labda yeye hana akili kama wengine, kumbe ukubwa wa pua si wingi wa kamasi.  Miezi ikayoyoma majaribio yakafanywa, Athalia akajikuta anafaulu vizuri. Hapo ndipo alipojua kuwa anawaelewa wahadhiri wake. Mara semesta ikaisha wakafanya mitihani ya kumaliza semesta. Lakini kabla ya kuanza mitihani kulikuwa na dokta mmoja aitwaye Makedonia, ni mkorofi anawafundisha akina Athalia kozi ya SM (Stadi za Mawasiliano), alijikuta hajabandika tamrini ya Athalia. Athalia aliingia ofisini kwa dokta Makedonia, dokta akahamaki wewe vipi? Mbona umekasirika kiasi hicho? Athalia akajibu "la hasha, mimi sijakasirika hata kidogo ila naomba kujua tamrini yangu kwa sababu pale ubaoni haipo. Dokta akamjibu usijali nitabandika jioni.

Jioni ikafika Athalia akawasili katika mbao za tamrini akakuta tayari tamrini yake imebandikwa.  Hapo Athalia akajua kuwa anaweza kufanya mtihani. Siku iliyofuata walianza mitihani yao vizuri na wakamaliza salama.

Mitihani ilipomalizika Athalia akaondoka na kushika njia kuelekea Matamvua. Majira ya saa mbili usiku alifika kitongojini kwao Katela. Athalia anakuthamini sana kwao ingawa kwao ni masikini sana.  Mama yake alifurahi sana kumwona binti yake amewasili salama kutoka safari ndefu, maana kutoka wilayani Chanua hadi jijini Highway ni muda wa zaidi ya saa kumi na mbili. Barabara inasifika kwa kona za kutisha lakini Mungu huwalinda na wanyama, ajali na majambazi huko njiani.

Athalia kwa hela yake ya kula chuo aliyopewa na serikali alijibana na kusakafia nyumba yao, hili lilikuwa faraja kwa mama yake.  Kama kawaida yake alipofika nyumbani aliendelea na kazi zake za shamba, aliamini kufanya kazi kwake kama mtumwa kuna siku ataishi kama mfalme. Athalia alijituma akishirikiana na ndugu zake bega kwa bega madamu yupo na ni mzima kiafya. Athalia alikumbuka kuwa aliacha hela zake shuleni Apple akaamua kwenda kwa mkuu wa shule hiyo ili kuzichukua hela zake.

Athalia alipofika kwa mkuu wa shule ya Apple alimkuta kajaa tele mithili ya maji ya bahari yasiyo na ukomo. Mkuu wa shule alipomwona Athalia alitetemeka, Oooh binti yangu Athalia! Hujambo? Athalia akaitikia sijambo, Bw. Chukua Chako Mapema akamkaribisha Athalia kwa ukarimu, Athalia akaitikia asante.

Athalia akamtazama mkuu wa shule ya Apple akaona huyu anaumwa, kwani Bw. Chukua Chako Mapema alikuwa anasumbuliwa na tatizo la Shinikizo la damu (Blood Pressure). Chukua Chako Mapema alianza kumhoji Athalia kuhusau habari za shule. Athalia akajibu kuwa ni nzuri kabisa, "na wewe unaendeleaje?"  Athalia akauliza. Chukua Chako Mapema akajibu ninaendelea vizuri.

Baada ya mazungumzo marefu, Chukua Chako Mapema akamwambia Athalia "naomba msamaha kwa kukufokea siku ile ofisini." Athalia akamjibu "mimi nilishakusamehe na ndiyo maana nimekuja kukusalimia. Chukua Chako Mapema akafurahi sana na kumwambia Athalia aende kwa mhasibu akachukue hela zake. Athalia alishukuru, akaondoka na kuelekea kwa mhasibu wa shule ya Apple kwenda kuchukua hela zake zote. Fedha hizo aliongezea kwenye ujenzi wa nyumba yao.

Kabla ya Athalia kuondoka Chukua Chako Mapema akaaga dunia. Yawezekana Chukua Chako Mapema alijijua kama atakufa akaanza kusafisha njia yake mapema, nani ajuaye hayo, lakini sisi twapapasa tu. Mwalimu Shalom alimpigia simu Athalia kumjuza, kisicho riziki hakiliki kwani Athalia alikuwa kishakata tiketi tayari kwa safari siku inayofuata.

Athalia akarudi chuo tayari kwa semesta ya pili ya mwaka wa kwanza. Katika kozi moja ya Kiswahili alikutana na dokta mmoja machachari jina lake Mikidadi, huyu ana sifa ya kuwa na utaratibu wake binafsi katika uendeshaji wa tamrini. Majaribio yake yote ni ya kushitukiza ingawa wengine na kwa mujibu wa utaratibu wa chuo mwanafunzi anatakiwa kupewa taarifa mapema kabla ya jaribio kufanyika. Hiyo ni hulka ya dokta huyu hata hivyo Athalia hakuona shida kwani aliona ni vizuri mwanafunzi anakuwa na utayari wake katika masomo yake. Jambo ambalo Athalia hakukubaliana na hakusita kulisema kwa dokta Mikidadi ni hili, alipoona wanafunzi wengine wanahudhuria semina mbili na wao wanahudhuria semina moja. Hata hivyo dokta Mikidadi alijibu kuwa kinachotakiwa ni kujiandaa na mtihani kwa sababu maswali ya mtihani hayatokani na maswali ya semina. Hata hivyo dokta Mikidadi akampenda Athalia kwa ujasiri na kujiamini kwake.

Katika somo la fasihi ya Kiingereza alikutana na dokta Mabumo, huyu anaongea kama Mmarekani mweusi. Wakati wa uwasilishaji anauliza maswali mengi mithali ya mpelelezi hadi mwasilishaji anapoteza mwelekeo. Athalia aliamua kumwendea dokta huyo ili kuona kama kuna uwezekano kwa wenzie kusalimika katika kozi hiyo. Lakini dokta huyo hakuacha kuuliza maswali kama Wanamafanikio wasemavyo; "mtu haachi asili yake."  Kwenye uwasilishaji wa Athalia aliuliza kuhusu tungo aliyoitoa kama kweli ni tashihisi. Athalia alijibu; "tashihisi kwa mujibu wa falsafa ya Kiafrika, lakini sijui falsafa ipi unayoirejea dokta ila tunaweza kujadili na kukubaliana. Athalia aliendelea kuwasilisha na akamaliza, akapewa alama zake.

Baada ya semina kuisha dokta Mabumo alimuuliza Athalia "ni kwa nini unajiamini hivyo?" Athalia alijibu kuwa alikuwa na uhakika na kile alichokisema. Dokta Mabumo alifurahi sana kisha akawa rafiki wa Athalia.

Masomo yakapamba moto, wakafanya majaribio, mazoezi mbalimbali kisha mitihani ya kumaliza semesta ijulikanayo kama UE (University Examinations). Wakamaliza mitihani na kurejea makwao.

Athalia akarejea nyumbani na kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi. Aliendelea na shughuli zake za kilimo na nyingine nyingi. Athalia akiwa likizo alipata matokeo yake akiwa amefaulu vizuri sana. Aliyapata kwa kumuuliza profesa Henry ambaye alimtumia kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi.

Likizo ikaisha, Athalia akarejea chuoni na kuanza masomo ya mwaka wa pili. Athalia aliendelea kufanya vizuri katika masomo yake mbali na kuwepo kwa migongano ya hapa na pale katika masuala ya tamrini. Lakini yote haya yalikuwa sehemu ya maisha ya kitaaluma, migongano hiyo ililenga kuleta mafanikio zaidi katika safari ya kuzifanya ndoto za Athalia siku moja ziwe kweli.

Siku moja wakiwa katika mhadhara wa dokta Mikidadi aliyekuwa akifundisha vizuri sana kozi ya Tamthiliya, Athalia alijiuliza sana kuhusu tamthiliya ya Mchungaji Mlevi iliyoandika na Ngahyoma kuwa iko katika kundi gani. Dokta Mikidadi alifundisha aina kuu mbili tu ambazo ni tanzia na ramsa, lakini tamthiliya ya Mchungaji Mlevi ina sifa za tanzia na ramsa, sasa itawekwa katika kundi lipi? Athalia akiwa anaendelea kujiuliza, katika kusoma kwake alikutana na kitabu kilichoandikwa na Mbene kinachozungumzia aina za tamthiya kuwa ziko tano, nazo ni tanzia, ramsa, tanzia – ramsa, ramsa – tanzia na melodrama. Kwa sehemu akapata jibu lakini Athalia ni mwanasayansi alitaka kuthibitisha kutoka kwa dokta.

Ndani ya mhadhara Dokta akaruhusu maswali laiti angelijua asingethubutu kuruhusu maswali kwani Athalia ni mdadisi kama mwanafalsafa. Athalia akanyosha mkono, dokta akamruhusu, Athalia bila kuchelea akauliza "Dokta naomba kujua tamthiliya ya Mchungaji Mlevi iliyoandikwa na Ngahyoma ni aina gani ya tamthiliya?" Dokta akajibu "ni Tanzia." Athalia akazidi kudadisi "mbona ina nguli wawili?" Dokta akakataa. Athalia akaendelea kuhoji dokta, "mimi nimemsoma Mbene anasema kuna aina tano za tamthiliya kati ya hizo, hii tamthiliya naona inaingia kwenye aina ya tanzia –ramsa kwa sababu nguli anayepigania jamii anaanza vibaya anamaliza vizuri wakati nguli anayeidhuru jamii anaanza vizuri na kumaliza vibaya." Dokta akakumbuka na kukubaliana na Athalia kisha akasema "ni kweli Athalia aina hizo tatu sikuzifundisha, umepatia. Kisha akaliambia darasa tunataka msome namna hii hapo tunajua tuna wanafunzi ambao watakuwa wanazuoni wa baadaye.

Semesta ya kwanza ikaisha wakafanya mitihani, Athalia akaenda zake likizo kwa dada yake Hana, huko Pakanga. Aliporejea chuoni aliendelea na masomo yake huku akifanya bidii katika kumtumikia Mungu. Kanisani kwenye maombi na ibada hakosi pia. Hayo ndiyo maisha ya Athalia. Mwaka wa pili ukaisha akafanya vizuri zaidi katika masomo yake zaidi ya mwaka wa kwanza. Miaka iliyofuata wa tatu na wa nne akafanya vizuri zaidi hata alipomaliza chuo alikuwa amefuzu vizuri sana katika masomo yake ya shahada ya kwanza kiwastani.

Dokta Lwanje alipoona anafanya vizuri katika masomo yake alimshauri Athalia aunganishe masomo ya uzamili (shahada ya pili). Ni kweli Athalia ndoto yake ni kuwa profesa lakini kuna changamoto nyingi zinamkabili, kwani ana mdogo wake mpendwa aitwaye Dorcus yuko kidato cha pili. Je ataweza kusoma shahada ya pili wakati anatakiwa kumsomesha Dorcus?. Athalia alijikuta anaitema bahati, hivi hivi "lakini ndoto yangu itatimia tu hata iweje kwa njia yoyote ile madam Mungu akinipa uhai." Athalia Alisema. Athalia alipokuwa chuoni hapo hela alizokuwa akizipata alizitumia kwa mambo mengi.

Athalia ni mjasiriamali, katika kupambana na maisha alijikuta akifanya biashara ya nguo. Fedha alizokuwa akipewa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu Athalia alizitumia kula, kulipia pango kama ilivyoelekezwa na bodi ya mikopo. Lakini katika kula kwake alijibana na kiasi kikubwa cha fedha hizo alikuwa akinunulia vitenge, kanga, vitambaa vya magauni, magauni ya watoto, vitambaa vya suti za kiume, na kadhalika na kuvituma kwao Matamvua. Dada yake aitwaye Rehema alikuwa akipokea mzigo huo kwenye basi la Ayubu na kuuza.

Mzigo ulipokuwa umeuzwa dada yake Athalia alizituma fedha hizo kwenye akaunti ya Athalia. Maisha yakaendelea hivyo, kila alipozipokea fedha hizo, faida alitoa ada ya mdogo wake Dorcus, na mtaji ukaendelea kukua, huku akiendelea kutuma mzigo kwao.

Athalia hakuridhika na hilo, alipokuwa mwaka wa nne aliamua kutafuta kazi ya kufundisha kama mwalimu wa muda maalumu Aliandika barua ya kuomba provisional results, akapewa, akayapeleka Pepee High School na barua yake ya kuomba kazi ya kufundisha. Nyota ya mtu kamwe, kamwe haifunikwi, Athalia akapokelewa vizuri shuleni hapo na kuambiwa arudi Jumatatu kwa ajili ya usaili.

Jumatatu ikafika, Athalia akaingia ofisini kwa mkuu wa shule ya Pepee, Bw. Otieno akapata mgeni "oh Athalia! Welcome. How are you? Alisema Otieno. Athalia akajibu I'm fine sir! How are you too? Otieno akajibu "we are doing well and we were expecting to see you today, it's lucky that you are here."  Bw. Otieno kutoka nchini Kashanga akamwambia Athalia akisema kuwa "we have a problem on Kiswahili subject, we need a competent teacher! Can you manage it? Athalia akaitikia yes sir!

Otieno alimwita mwalimu Halima na kumtuma aende na Athalia ili wakamfanyie usaili. Athalia akiwa darasani kidato cha nne akafanya vizuri sana katika usaili huo, walimu waliomsaili wakafurahi sana. Ripoti ilipofika kwa mkuu wa shule Athalia aliambiwa arudi Jumatatu kuanza rasmi kazi. Jumatatu hiyo ikafika, Athalia akatia mguu shuleni, mambo yakawa sivyo ndivyo, Athalia alifikiri siku ya Jumatatu ni ya kukabidhiwa darasa la kufundisha, lakini cha ajabu alipofika tu alikutana na sauti ya Otieno "Athalia." Otieno aliita. Athalia akaitikia "yes sir!" Otieno akamwambia Athalia "we noticed that you have ability to teach advanced level, so we assigned you in advanced level. Do you agree?" Athalia akajibu "yes, I can manage it." Athalia akapewa kidato cha tano na cha sita, akafanyiwa usaili tena, akafanya vizuri zaidi. Basi akaendelea na kazi ya kufundisha.

Wanafunzi wa shule ya Pepee High school wakampenda sana Athalia, wengine walisema "madam usiondoke, ukiondoka na sisi tutahama." Athalia akawaambia "nyinyi watoto someni. Mi nipo wala sitaawacha kamwe." Wanafunzi walifurahi sana walihisi wamepata ukombozi kutoka kwa Mungu.

Siku zikaendelea kuisha Athalia akamaliza masomo yake ya shahada ya kwanza, hapo Otieno aliona kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuwa na Athalia milele. Otieno akamwita Athalia na kumweleza yaliyo katika mutima wake. Otieno akasema " Athalia we found that you're talented in teaching and our students like you so much, therefore, as a board we decided to employ you permanently. Athalia akahamaki "what?" Otieno akajibu "don't worry, we shall give you a good package of salary, do you want to reject our offer?" Athalia akajibu "no sir, mh! Anyway, I agree it but how much will you give me as a degree holder?" Otieno akajibu "three hundred fifty thousands! Are you satisfied with it? Athalia akaitikia "yes sir I'm ok."

Wahenga husema ukiona kobe kainama jua atunga sheria. Athalia alikubali huku akijua kuwa tayari ameomba kazi serikalini. Akaendelea na kazi lakini kosa kubwa walilolifanya utawala wa Pepee High School ni kutomlipa Athalia fedha zake za kufundisha wanafunzi wakati wa likizo. Hili lilimvunja moyo Athalia hata hakutamani tena kuendelea na kazi katika shule hiyo. Miezi ikapita wanafunzi wakafanya mitihani ya mhula wa kwanza, Athalia akasahihisha mitihani yao, akajaza ripoti kisha akawaaga na kurudi nyumbani kwao Matamvua. Otieno na wenzake walijua kuwa Athalia atarudi tena kufundisha lakini kumbe si wazo la Athalia kwani alikumbuka walivyomnyanyasa katika zamu na kutomlipa fedha zake wakati yeye anatafuta fedha. Athalia alisema moyoni mwake "hawa wana utani na mimi, wanafikiri mimi nachezea maisha, nipo kutafuta fedha tu."

Mwezi wa Agosti ukafika walimu waliohitimu vyuo vikuu wakapangiwa vituo vya kazi, Athalia akapangiwa shule ya sekondari ya Magamba iliyoko wilani Chanua mkoani Matamvua. Athalia alipoisoma barua hiyo alihisi hajatendewa haki na serikali yake ya Mafanikio kwani Mkuu wa shule hiyo Bw. Pangu Pakavu alisifika kwa ubandidu. Athalia aliwaza aende au la! Majibu yalikuwa magumu kuyapata, kwani kweli shule iko mjini, mahali pazuri lakini huyo mkuu ni kikwazo tosha kwake, kwa sababu mkuu wa shule hiyo amewahi kupigana na walimu wake. Athalia aliamua kutuma maombi ya kazi katika chuo kikuu cha MKU (Mwanamaendeleo Kamili University) kilichopo mkoani Matamvua. Masikini muda wa bajeti ya chuo ulikuwa umepita japokuwa Athalia alikuwa na sifa za kufanya kazi hapo.

Mwezi ukapita, Athalia akiwa na mahusiano na kaka mmoja aitwaye Johnson Paschal, Athalia aliamua kumshirikisha juu ya ajira yake. Johnson Paschal alisoma chuo Kikuu cha Highway kisha akapata nafasi ya kufanya kazi nchini Ukarimu. Akiwa huko alimshauri Athalia aende serikalini na asihangaike na ajira ya chuo cha binafsi. Johnson alisema kama Athalia anataka kuwa mhadhiri, atasoma shahada ya pili na ya tatu hadi afikie uprofesa. Athalia akatiwa moyo naye akaazimia kufanya hivyo kwani hata hicho chuo walikuwa wakimpiga tarehe tu.

Athalia akafika shuleni Magamba mwezi Novemba na kumkuta huyo mkuu wa shule Bw. Pangu Pakavu, akamweleza yeye ni nani na anatoka wapi. Pangu Pakavu kama ilivyo ada yake akauliza mbona umechelewa sana ulikuwa wapi? Athalia akamjibu kuwa alikuwa Highway kuhangaikia mzigo uliotumwa kutoka nchini Ukarimu na yeye ndiye aliyekuwa anahusika na mzigo huo, hivyo akashindwa kuripoti mapema. Pangu Pakavu kwa vile alikuwa na shida ya mwalimu wa somo la Kiingereza hakuchelea, akamjazia Athalia fomu za ajira na kumwandikia barua ya kuripoti, kisha akampeleka halimashauri ya wilaya ya Chanua ili kukamilisha hatua zote za ajira. Athalia akaanza kazi rasmi.