Mwezi Novemba ndio huo, Athalia ndani ya nyumba, kazi imepamba moto kwani ndo mwezi wa pili tu tangu shule ifunguliwe kwa wanafunzi wa kidato cha sita. Athalia akakutana na walimu wenzake wakaendelea kuendesha gurudumu la maendeleo ya taifa lao la Mafanikio. Athalia alipewa somo la Kiingereza moja na Kiingereza mbili kufundisha katika kidato cha tano na sita. Athalia baada ya kutambulishwa na Pangu Pakavu darasani akaendelea na ufundishaji.
Wanafunzi wa shule ya Magamba waliona wamepata mkombozi katika somo la Kiingereza. Wakati kazi imepamba moto wanafunzi nao hasa wale wa kidato cha sita maswali hayakuwaisha mara maswali ya Kiingereza mara ya Kiswahili wakimwandama mwalimu Athalia. Athalia hakusita kuwasaidia mbali ya kuzungukwa nao mithili ya siafu waliopata kitoweo. Athalia aliwasaidia wanafunzi hao kadri awezavyo bila kujali kama amekula au la, cha msingi kwake ni wanafunzi wamesaidiwa.
Maisha yakazidi kuwa ya mashaka na wasiwasi kwani tangu Athalia awasili hapo kazini serikali ya Mafanikio haina hata mpango wa kuwapa mishahara. Siku moja Athalia aliwaza hana hela kwenye akaunti yake ya NBM (National Bank of Mafanikio) hivyo akaamua kwenda mjini Matamvua kuchukua hela katika akaunti yake ya benki iitwayo CDB (Community Delopment Bank). Hahahaa! Athalia yuko kazini ni lazima amwarifu mkuu wake wa kazi. Athalia anaamua kumwendea mkuu wake kwa ujasiri. Walimu wanamwogopa Pangu Pakavu kama chatu aliye katika mawindo akitafuta nani ammeze. Lakini Athalia ni jasiri, komandoo wa vita akajitosa kumweleza mkuu wake bwana Pangu Pakavu. "Mkuu" Athalia aliita, Pangu Pakavu akaitikia "Unasemaje Athalia" Athalia bila kuchelea akajibu "samahani mkuu naomba ruhusa ya kwenda Matamvua kuchukua hela." Pangu Pakavu akahamaki na kusema "umefika juzi tu halafu unaanza kuzurura." Athalia akajibu kwa hasira "Mkuu siwezi kufundisha huku nina njaa." Pangu Pakavu alishangaa na kujiuliza huyu binti yukoje? Mbona anajiamini sana? Kwa nini? Maswali haya yalizunguka kichwani mwa Pangu Pakavu. Pangu Pakavu akiwa katika dimbwi la mawazo na hasira juu ya Athalia, Athalia yeye akawa anaondoka taratibu kwenda kupanda basi la kwenda Matamvua. Kalani wake akampoza ndivyo walivyo watoto wa siku hizi, waache usisumbue sana akili. Pangu Pakavu ataacha, kamwe hawezi amezoea udikteta, anataka kila mtu awe chini yake.
Athalia akapanda gari na kuelekea mjini Matamvua, akafika huko mjini na kufanya michakato ya kuhamisha fedha zake kutoka benki ya CDB (Community Development Bank) na kuzipeleka katika benki ya NBM (National Bank of Mafanikio). Alipokamilisha kuhamisha fedha hizo, Athalia akarejea wilayani Chanua, shuleni kwake Magamba. Katika kuishi kwake alijikuta akiwa na majukumu mengi lakini alikabiliana nayo.
Shule ya sekondari Magamba haina nyumba za walimu, kwa kuwa Athalia ni mgeni katika eneo la shule kutokea nyumbani kwao ingawa ni wilaya hiyohiyo alijikuta yu mashakani tena. Alipokuwa akiripoti shuleni hapo alijikuta hana mahali pa kuishi, "je nitaweza kutoka nyumbani kila siku? La hasha mbona nauli ni kubwa sana." Athalia alijiuliza na kujijibu mwenyewe. Lakini ashukuriwe Mungu kwamba katika shule ya Magamba alikuwepo mwalimu Rhoda Ayubu ambaye walisoma wote katika chuo kikuu cha Highway. Rhoda akamfadhili Athalia mahali pa kukaa huku akiendelea kutafuta nyumba. Wilaya ya Chanua ina watu wengi lakini si wafanya biashara. Ama kweli penye miti mingi hapana wajenzi kwani wafanyakazi ni wengi lakini nyumba za kuishi ni za shida sana.
Athalia akiwa anaishi na Rhoda alijishusha sana, Rhoda ni mweusi, mwembamba wa umbo, anaongea kama chiriku lakini hana dogo. Siku moja alimwita Athalia na kumwambia chakula ajitegemee. Rhoda alifanya hivyo baada ya kuona mchele na mafuta ya kupikia alivyovileta Athalia vimeisha. Rhoda alikuwa mkakasi kwa jinsi alivyo na anayoyafanya havifanani hata kidogo. Athalia kwa bahati nzuri alikuwa ametoka kuongea na mwenye nyumba ili ahamie kwake. Athalia kimsingi alikuwa amechoka kuishi kwa mtu bali alitamani ajitenge naye, kwani Rhoda ni mwingi wa habari. Sura mbalimbali za wanaume utaziona zikiingia hapo nyumbani kwake. Hili lilikuwa likimkera Athalia kila kukicha. Mungu hufanya jambo katika wakati muafaka ndivyo wanavyoamini Wanamafanikio. Siku hiyo alifanikiwa kupata jibu la kuridhisha kutoka kwa mwenye nyumba kwamba anaweza kuhamia kwani tayari aliyekuwa akikaa humo ameshaondoka. Athalia akahamia jioni ile ile, kwani Wanamafanikio husema akufukuzae hakuambii toka bali utaona matendo. Rhoda ana tabia ya ajabu ambayo haiwezi kuigwa anaonesha kukupenda machoni lakini ni mbwamwitu ambaye amevaa vazi la kondoo. Haoni shida kukuanika hadharani na kukuvua nguo ukajiona u uchi wa mnyama. Hiyo ndiyo sifa kuu ya Rhoda.
Athalia alihamia nyumbani kwake na kuanza maisha ya ubachela, Rhoda kwa aibu alikuwa anashindwa kwenda kwa Athalia, lakini Athalia hakumchukia hata kidogo aliuthamini msaada wake, na kila alicholetewa na ndugu zake alimgawia Rhoda. Athalia ni mcheshi na mpenda watu, kutokana na tabia yake hiyo akapendwa sana na walimu wenzake. Mwalimu Christina Haule ajulikanaye kwa jina la mama Tamali akawa rafiki mkuu wa Athalia. Kitendo hiki kilimkwaza sana Rhoda, akaanza kumchukia Athalia na kila mara alipojaribu kuwatenganisha harakati zake ziligonga mwamba. Alipoona ameshindwa kuwatenganisha, akaamua kuwachukia wote wawili.
Athalia anamthamini sana mtu ambaye anamjali. Katika shule ya Magamba kulikuwa na mwalimu Neema Ambilikile mwenyeji wa jijini Highway. Neema ni mpole na si mwongeaji sana mpaka amekufahamu vizuri ndipo utagundua anaongea, ana hekima na ni mshauri mzuri pale unapotatizwa. Huyu urafiki wake na Athalia ulianzia siku walipokwenda kuchukua fedha ya kujikimu. Siku zikaendelea wakawa marafiki wakuu wa kushibana na Athalia. Wawili hawa walishirikiana kwa kila jambo na Athalia Mungu hakumuacha kamwe. Neema anafundisha somo la Kiswahili moja na ni mwalimu mzuri, wanafunzi wanampenda sana.
Ndoa ni kifungo kidogo kwani mwalimu Christina Haule alilazimika kutengana na rafiki yake kipenzi Athalia kwa kumfuata mumewe aliyekuwa akiishi jijini Pateni. Athalia alimwombea Baraka kwa Mungu katika maisha yake ya ndoa. Kuondoka kwa Christina Haule lilikuwa pengo kubwa kwa Athalia lakini Mungu akamrudishia faraja Athalia kwani Neema akawa mtu wa karibu sana kwa Athalia. Neema na Athalia walikuwa wakipika pamoja, wakinywa pamoja, wakila pamoja, hayo ndiyo maisha waliyoyaishi Neema na Athalia lakini kila mmoja alikuwa na kwake.
Miaka ikaendelea kusonga mbele, wakaingia mwaka mwingine, kidato cha sita wakamaliza shule na wakafanya vizuri sana katika mtihani wao wa Taifa. Pangu Pakavu akavimba kichwa "watoto hawa walikuwa na akili sana" Pangu Pakavu akanena. Wanafunzi hao walishika nafasi ya kumi na sita kitaifa. Mwaka uliofuata kidato cha sita awamu ya pili wakafanya vizuri zaidi ya waliotangulia na kushika nafasi ya tatu kitaifa na kuongoza karibu masomo yote kimkoa, hapa sasa Pangu Pakavu nusura avae suluari kichwani. Lakini ukweli aliumia sana moyoni kwani kijana wake Ilimradi aliyehitimu katika kidato cha sita mchepuo wa sayansi katika shule iitwayo Pambana Kiume alikuwa amefeli mtihani huo kwa kupata daraja la nne. Pangu Pakavu aliona aibu sana kwa walimu Neema na Athalia kwani masomo wanayoyafundisha yaliongoza kwa ufaulu kimkoa na hata kitaifa.
Wahenga walisema usimdharau usiyemjua, lakini kwa Pangu Pakavu haikuwa hivyo, yeye humdharau mtu yeyote anayemfahamu na asiyemfahamu akijivunia uchifu. Siku moja kwenye tafrija ya walimu wa shule ya sekondari ya Magamba bwana Pangu Pakavu aliwaalika wakaguzi wa kanda ya nyanda juu kusini mwa nchi iliyobarikiwa sana kwa amani duniani wahudhurie tafrija hiyo. Wakiwa katikati ya tafrija aliwasimamisha walimu hawa: Athalia, Neema, Abdallah, Masumbuko, Rajab, Rhoda na Mbayawangu, kisha akatamka mbele ya kadamnasi "watoto hawa walioko kidato cha sita wakifeli, wachawi ni hawa walimu niliowasimamisha." Jambo hili liliwaumiza sana akina Athalia lakini hawana la kufanya. Siku ya siku ikafika kidato cha sita wakafanya mtihani wa taifa, matokeo yakatoka, kidato cha sita wakafaulu mtihani na kushika nafasi ya tatu kitaifa na ya kwanza kimkoa, huku kijana wake akiwa amefeli kwa kupata daraja la nne. Athalia akasema waziwazi na kwa sauti "mchawi ameonekana kajilogea mwanae"
Siku mbili baadae wakiwa katika kikao cha walimu, Pangu Pakavu akaanzisha mada ya matokeo ya kidato cha sita. "Ooooooooh! Ninawashukuru sana walimu kwa kazi yenu njema, nilikuwa najiuliza Kiingereza wanazungumzia wapi hadi wanawashinda shule za sainti. Hongera sana mama Athalia, Neema hongera sana, eti Magamba wanawashinda shule za watu wa Pwani ambao ndiyo wazungmzaji wa lugha ya Kiswahili. Kweli mmefanya kazi kubwa mno nawashukuruni sana." Walimu wakasemezana mh! Uchawi umeisha! Mwalimu Abdallah anapenda pombe, lakini akasema "anaona aibu tu Pangu Pakavu afanyeje." Mwacheni huyo let us take our time for better future." Wakatawanyika.
Wakati fulani Athalia na rafiki yake Neema walitamani sana wahame shule ya sekondari Magamba kutokana na ukandamizaji wa Pangu Pakavu, lakini hawana sababu ya kuwafanya wahame. Si Athalia wala Neema kaolewa kwamba labda iwe ndiyo sababu ya kuwaondoa Magamba sekondari. Walikubali kufa kibudu kwani ni lazima wapambane tu na hali waliyonayo.
Pangu Pakavu ni mzee wa vikao kila saa nne wakati wa mapumziko utaambiwa kuna kikao, lakini Athalia wakati mwingine anakuwa na mgomo baridi, kama ana kipindi darasani anaenda kufundisha kipindi chake badala ya kuhudhuria hii ilitokana na vipindi vyake vingi kuwa baada ya mapumziko ya saa nne. Aliona vipindi vyake vinaingiliwa na vikao vya bwana Pangu Pakavu ambaye mara zote hashauriki. Athalia akaamua kuchukua msimamo wake binafsi. Siku moja aliamua kuhudhuria kikao cha Pangu Pakavu na kikao hicho kilikuwa kinahusu utovu wa nidhamu kwa wanafunzi. Athalia yeye alikuwa katibu wa kamati ya nidhamu, baada ya mjadala mrefu sana Athalia aliamua kumuuliza Pangu Pakavu kuhusu sheria za shule juu ya usukaji nywele kwa wanafunzi wa kike. Pangu Pakavu akawa mkali kama mbogo aliyekoswa na risasi mbugani. Athalia alipogundua hilo aliamua kujiuzulu kazi ya ukatibu wa kamati ya nidhamu.
Watoto wa shule ya sekondari Magamba ni watukutu mno. Wenye kubeba mimba na kuzaa, yote haya Athalia alikumbana nayo. Mara yuko na askari kukamata wahalifu, mara mahakamani kutoa ushahidi juu ya vijana waliofanya uharibifu kwa wanafunzi wa kike. Lakini alipokwazwa na Pangu Pakavu Athalia akaachana na masuala ya nidhamu kiofisi, mara tu alipomaliza kesi ya Tuntule Lwitiko aliyebeba mimba na kuzaa mtoto.
Siku moja kiongozi wa wanafunzi/ katibu wa shule alikamatwa akiwa amelewa akaletwa shuleni hapo, naye akakiri mbele ya Pangu Pakavu kama alikunywa pombe na kulewa. Hapo Pangu Pakavu aliona umuhimu wa Athalia, akamwita Athalia na kumuuliza maswali haya: "mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ni nani?" Athalia akajibu kuwa "ni mwalimu Nelson" ambaye alipandishwa cheo na kuwa mkuu wa shule ya Pishaneni. Pangu Pakavu akauliza tena "msaidizi wake ni nani?" Athalia akajibu "ni Aaron ambaye yuko masomoni anasomea shahada ya kwanza Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtemi. Na wajumbe wengine ni Mwakyambiki na Mengo." Pangu Pakavu akagundua kuwa Nelson na Mwakyambiki wamepandishwa vyeo na kuwa wakuu wa shule, Aaron yuko masomoni na Mengo yuko kusimamia mitihani ya kidato cha nne ya Taifa. Pangu Pakavu ilibidi awe mpole akamwomba Athalia alishughulikie suala hilo na walimu wenzake waliopo kituoni hapo. Kwa bahati nzuri sana mwanafunzi Thomas akaamua kuingia mitini, hivyo kikao hakikufanyika tena.
Kuishi na mtu au watu ni kazi, Athalia ni mvumilivu sana lakini Magamba sekondari aliishiwa ujasiri. Siku moja aliamua kumtafuta Johnson Paschal kwa njia ya simu na kumweleza hali halisi ya maisha ya hapo Magamba sekondari. Johnson Paschal alimtia moyo kwamba mwaka unaofuata watafunga pingu za maisha na hiyo adha ya Pangu Pakavu itaisha tu. Athalia alifurahi akijua msiba wake uko ukingoni lakini kumbe Johson Paschal ujana unamtesa.
Johnson ni msomi na mwelewa ila ana hasira mithili ya nyati aliyenusurika risasi mawindoni. Siku moja akiwa huko nchini Ukarimu alipigiwa simu na shangazi yake kipenzi kuwa baba yake mzazi anaumwa sana, alijikuta akiondoka Ukarimu kabla ya nyakati zilizokusudiwa. Kuchanganyikiwa kwa Johnson kulisababisha Athalia apatwe na hofu, kwani akiandika baruapepe hazijibiwi, simu haipatikani. Athalia alihaha kwani kipenzi cha roho hapatikani, lakini baadaye alifanikiwa kumpata. Johnson alijitetea, Athalia akamwelewa kwani alikuwa akimpenda kwa dhati ya moyo wake.
Johnson kabla hajarejea Ukarimu kumalizia masomo yake ya umahiri walionana na Athalia eneo la baridi kali sana kwani yeye alikuwa mwenyeji wa mkoa wa Usicheze kabila lake Mnguu. Wakalala katika hotel moja hapo lakini kesho yake alitakiwa kwenda Songeni na hapo ndipo walipotofautiana na Athalia. Athalia hataki Johnson aondoke, Johnson anataka kuondoka, mvutano huo ulipelekea Johnson aondoke kwa hasira.
Athalia alibaki analia kama mtoto aliyenyimwa ziwa na mamaye. Johnson akazima simu yake asipatikane usiku mzima. Siku iliyofuata Athalia akaanza safari ya kurudi Magamba sekondari. Miezi minne ikapita Johnson hapatikani kwenye simu wala hajibu baruapepe. Baada ya muda wa miezi miwili kupita bila masiliano baina yao, siku moja Athalia akaamua kutembelea baruapepe ili kuona kama kuna jipya. Alipoingia katika baruapepe yake alikutana na ujumbe kutoka kwa Johnson. Athalia alishukuru Mungu kuwa, Johnson amefufuka baada ya kuzima ndoto iliyoanza kupea ghafla ikafunikwa na lindi zito la giza. Wakaendelea kuwasiliana lakini sijui kama watafika. Johnson akaomba msamaha, Athalia akamsamehe, huku mama yake Athalia akisema "mimi sina amani kabisa naye huyo, lakini kama ya Mungu yatatimia." Maisha ya kimahusiano baina ya Athalia na Johnson yakaendelea kwa tahadhari kubwa mno. Athalia hana uhakika kama Johnson anachosema kinatoka moyoni. Haya ndiyo maisha ya Athalia katika ulimwengu wa mapenzi.
Athalia akaendelea na kazi yake ya ufundishaji huku kazi zake za shamba haziachi, wahenga walisema "mtu haachi asili yake." Athalia hakuacha kazi yake ya kulima viazi mviringo, lakini wazo la kurudi shule haishi kuliwaza. Hayo ndiyo maisha ya Athalia katika ulimwengu wake wa ndoto za kuufikia uprofesa, sijui atakuwa profesa siku moja, nani ajuaye hilo, mwenye kujua ni Mungu wake peke yake.