Chereads / TUFANI YA MAFANIKIO / Chapter 8 - SURA YA SABA

Chapter 8 - SURA YA SABA

Mwaka wa tano sasa Athalia yuko kazini, lakini ndoto zake bado zinaendelea kuzunguka kwenye akili yake. Johnson naye anamhimiza Athalia aende kusoma, bila hata kinyongo Athalia anamsikiliza tu. Kweli maisha ndugu ni safari ndefu sana lakini kuimaliza kazi kweli. Athalia hajui hatima yake kama atafanikiwa kuufikia uprofesa licha ya kuwa ndoto yake ina uimara mithili ya ngome ya Yeriko. Anachowaza ni elimu tu ila mazingira rafiki hayapo kabisa ya kufanikisha ndoto, lakini anajipa moyo mkuu kama Daudi alivyomkabili Goliati, akiwa na tumaini kuwa ipo siku atafanikiwa kuwa profesa.

Vitendawili vya Athalia ni vingi, ndoa nayo ni mwiba kwani mpaka sasa hajui hatima yake ataolewa na nani. Je ni Patrick au Johnson au wote wawili si riziki? Kadri siku zinavyokwenda ndivyo Johnson anavyobaini makosa yake. Baada ya miezi sita Johnson alijitosa tena kumwandikia Athalia kumsalimu. Athalia alibeep, matokeo yake Johnson alipiga simu na kumwomba msamaha Athalia. Ni nani ajuaye kama Johnson atasamehewa na Athalia? Mungu pekee ndiye ajuaye yaliyomo katika moyo wa Athalia.

Siku zinayoyoma, Athalia hana mume wala mchumba, Patrick yeye kajifia kwenye shimo la maangamizi lisilo na matumaini ya kufufuka tena labda Jehova atamfufua kutoka katika kundi la wa nafsi, roho na uaminifu. Patrick alikuwa amepata msukosuko wa kesi kazini kwake kutokana na tamaa zake za kifedha, alifanya uhalifu wa kutumia dawa za hospitali nje ya Matumizi yaliyoidhinishwa na serikali pendwa ya Mafanikio. Jambo hili lilimgharimu hadi kufukuzwa kazi katika hospitali ya Maji Marefu. Katika sintofahamu hiyo Patrick aliondoka wilayani Chanua bila kuaga na akabadilisha namba za simu.

Masikini kijana mtanashati, hekima kwa wingi, na uongo mwingi kuzidi Lusifa kazama kwenye shimo la waliokata pumzi. Patrick aliishi mwili lakini sifa za ufahamu na matendo alikuwa amekufa kabisa. Hali hii ilipelekea kuvunja Mahusiano na Athalia kwa sababu tu Patrick alikuwa si mwaminifu tu bali pia alikuwa mwingi wa Habari. Taarifa zake nyingi zilimfikia Athalia juu ya mienendo yake. Athalia aliona ni sawa na mtu aliyefiwa na Mpendwa wa roho yake. Athalia aliomboleza kufiwa na mtu wa karibu sana katika ulimwengu wa mapenzi, lakini ajuaye ni Mungu Patrick hakuwa riziki kwa Athalia. Inawezekana Patrick angemsababishia Athalia maradhi ya shinikizo la damu maana tabia ya usiri na wingi wa habari hilo ndilo kero kubwa kwa Athalia. Kutokana na kifo cha Patrick kimatendo na kifikra akatoweka mbele ya macho ya Athalia na dunia ya fikira na matendo ya ustaha licha ya kwamba Athalia alimpenda mwili na roho. Patrick alitoweka mithili ya ua lichanualo saa sita na kunyauka siku hiyo hiyo. Ajisemea moyoni Athalia "yote hupangwa na Mungu", kumbe Patrick alikuwa ni mlevi pia, si pombe na ikulu za wavaa sketi. "Asante Mungu mwema" Athalia alishukuru.

Athalia akiwa kituoni kwake anaamua kuanza mikakati ya kwenda shule, maana aliona wanaume wote anaokutana nao ni vimeo tu, kila akiangalia wa leo bora wa jana. Sasa kilichomjia akilini mwake ni bora aende shule akasome. Swali gumu linaloibuka akilini mwa Athalia ni je atapata ruhusa ya kwenda kusoma? Athalia alijiuliza maswali mengi akiwa katika wimbi zito sana la mawazo, lakini alijipa moyo kwani yeye amekwishakutimiza miaka zaidi ya miwili kazini na kwa mujibu wa sheria za nchi na serikali ya Mafanikio mfanyakazi wa umma anaruhusiwa kwenda masomoni ikiwa ametimiza miaka miwili kazini.  Athalia hakuishia hapo kuwaza, akajijibu kwa mujibu wa sheria nitaruhusiwa lakini je Pangu Pakavu atakubali Athalia aondoke Magamba sekondari? Baada ya maswali mengi Athalia aliamua kutunga sera yake.

Athalia binti jasiri hakujali Pangu Pakavu atajibu nini, anachotaka yeye ni kutimiza ndoto yake. Athalia aliamua kutuma maombi ya kusoma shahada ya umahiri katika taaluma ya isimu ya Kiswahili, kisha akawasiliana na wahadhiri wake ambao anawaheshimu kama baba zake Dkt.  Mabumo, Lwanje na Maringo wanaompenda Athalia kama binti yao na hivyo kwa hali zote wanamsaidia Athalia kimawazo na kivitendo. Athalia akiwa Magamba sekondari aliamua kupakua fomu za maombi ya shahada za umahiri katika mtandao. Athalia akajaza fomu hizo na kuzituma kwa njia ya basi na kupokelewa Highway na kaka mmoja aitwaye Benard ambaye alizipeleka kwa Dkt. Maringo. Dkt. Maringo alizikamilisha fomu hizo sehemu yake na kuzipeleka katika Taasisi ya taaluma za Kiswahili.

Siku moja Athalia akiwa nje ya kituo chake cha kazi kwenye kazi maalumu ya uwezeshaji wa vijana wa kulitumikia taifa la Mafanikio. Athalia alipokea simu, namba ngeni kabisa. Alipoongea na aliyempigia aliambiwa kuwa ni mratibu wa masomo ya uzamili katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili iliyoko katika Chuo Kikuu cha Highway nchini Mafanikio. Mratibu alimwambia Athalia kuwa barua za wadhamini wake hazionekani na tayari walikuwa wanaingia kwenye seneti ya uchaguzi wa wenye sifa za kudahiliwa katika shahada ya umahiri. Akamwambia Athalia awambie wadhamini wake wapeleke barua mara moja. Ashukuriwe Mungu wa mbinguni wadhamini wa Athalia baada ya kuarifiwa kuwa barua za udhamini kwa Athalia zinahitajika hawakufanya ajizi, mara moja wakazituma ofisi inayohusika.

Ehehehe! Mambo yamekuwa mambo, Athalia kaomba chuo na kupata nafasi katika Chuo Kikuu na kikongwe nchini Mafanikio cha Highway. Chuo hiki kiko katika mji mkubwa wa kibiashara na kiutawala, watu wake wana pilika pilika nyingi mno za kila namna, mchana kutwa na usiku kucha. Lakini Athalia yeye hana shida na jiji hili lililoko ufukweni mwa bahari ya Amani ambayo ni kubwa ulimwenguni. Athalia anafurahia kupata nafasi ya kusoma kwani hiyo ndiyo dira ya kutimiza ndoto zake taratibu na ombi lake kwa Mungu linazidi kujibiwa. Highway ni chuo kikubwa ambacho watu wa kutoka mataifa mbalimbali duniani husoma hapo na huipenda sana nchi ya Mafanikio ambayo wakazi wake wengi ni masikini licha ya kuwa na rasimali nyingi kama madini ya kila aina yanayopatikana nchini humo, wanyama wa kila namna na misitu ya aina zote. Hii ndiyo nchi aishiyo Athalia.

Athalia anathamini sana kazi lakini pia anahitaji elimu. Athalia akaandika barua na kumpelekea Pangu Pakavu lakini huyu Pangu Pakavu anaonekana kutoridhia vema, hata hivyo anazipokea barua za Athalia na dada yake mpendwa wa karibu Martha. Athalia na Martha wanapendana na wote wanataka kusoma shahada ya umahiri. Pangu Pakavu baada ya kupokea barua za Athalia na Martha anaamua kuwatangazia walimu wake wote ili kufahamu ni wangapi wana nia ya kwenda kusoma.  Mwalimu Johari na Joabu nao wanajitosa kuonesha nia yao kwa kuandika barua zao na kumpatia Pangu Pakavu.

Athalia akiwa katikati ya harakati za kutafuta ruhusa anaendelea na shughuli zake za shamba za kilimo cha viazi mviringo. Katika mkoa wa Matamvua viazi mviringo hustawi sana hususani wilayani Chanua. Athalia analima viazi mviringo kila mwaka akitiwa nguvu na kaka yake Hoshea. Kaka yake ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za mashamba, hivyo Athalia hana shida juu ya kuhudumia zao la viazi mviringo.

Athalia hakika amesongwa na mawazo akilini, msongo wa mawazo ya shule, kazi, maisha ya mahusiano yote yamemuweka kwenye mtanziko mkubwa ambao Mungu na nafsi yake ndo pekee mashahidi wa mtanziko wake. Athalia anajiuliza katikati ya bahari nyeusi, "kwa nini nilimkubali Patrick. Eeeee Mungu! Athalia akahamaki, ni kitu gani hiki kinanitokea. Hata hivyo ninakushukuru kwani imetupasa kushukuru kwa yote." Lakini Athalia anajilaumu laiti kama angelijua kama Patrick atafia katika kaburi la Sahau asingemkubali kabisa kuwa na mahusiano nae ya kimahaba. Patrick masikini kajifia yuko ndani ya kaburi la Sahau, swali lililopo ni je Patrick atasaulika katika akili ya Athalia? Lakini Athalia mwanamke shujaa anajipa moyo kwamba yote hupangwa na Mungu.

Athalia alipokuwa chuoni Highway alikuwa na mpenzi wake wa karibu sana aitwaye Jackson ambaye walipendana sana lakini ni mtu asiye na msimamo. Athalia na Jackson walidumu kwa muda wa miaka mitatu kabla ya kukutana na Johnson. Jackson hakuwa na mpango wa kuoa. Muda ukaendelea kwenda akamwambia Athalia anahisi si mpango wa Mungu yeye kuwa na mwandani Athalia maishani, kwani moyoni mwake hukosa amani, na kila aitafutapo amani hudumu kwa muda mfupi tu.  Athalia alipoona vitendawili vinazidi kuongezeka aliamua kuendelea na utaratibu mwingine.

Athalia baada ya muda kupita aliamua kuingia katika mahusiano mengine na kijana mtanashati Johnson anayependa kusoma na ni mpenda maendeleo na mwenye kujibidisha sana katika kutafuta fedha. Hapo Jackson hakuamini kama Athalia amefikia uamuzi huo lakini hayo ndiyo yaliyojiri, kwani ukisema wa nini wenzio wanamezea mate, tutampata lini. Athalia akamua kuachana na Jackson katika suala la mapenzi na kila mtu akashika hamsini zake. Jackson hakuamini kama Athalia alifikia maamuzi magumu kiasi hicho.

Jackson jamani alikumbuka stepu muziki ukiwa umekwisha. Anampigia simu Athalia kumuulizia kama ana mtu, Athalia hakufanya ajizi akamjibu kwa roho nyeupe, tayari nina mtu na ikimpendeza Mungu mwakani tutafunga ndoa. Jackson alihamaki "unasema kweli siamini. Athalia hivi kweli nimekukosa kabisa?" Jackson alisema. Athalia akamweleza Jackson hali halisi vipi kwani? Si wewe ulisema huna amani nami? Bwana eeeh! Niache mwenzio mie nshajicommit kwa mwingine." Athalia alihitimisha hivyo.

Jackson hakuwa na la kufanya kwani sasa mwana si wake tena, lakini wanawasiliana kama ndugu. Jackson ni mtaalamu wa kuandaa vipindi vya kwenye runinga na redioni. Jackson ni kijana mtanashati, mrefu wa wastani, ana hekima sana katika kuongea na huruma nyingi sana kwa wahitaji lakini kilichomshinda ni kufanya maamuzi juu ya kumwoa Athalia. Mbali na kwamba baba yake Jackson alimpenda sana Athalia lakini mwoaji hakuwa tayari.

Miaka ikapita Athalia akiwa huko mpakani akapigiwa simu na Jackson. Masikini ni miaka mingi sana Jackson anamtafuta Athalia kwenye simu lakini Athalia hapatikani, kumbe sababu kuu ni Johnson amesababisha Athalia abadilishe namba ya simu. Haswa hawakukosea wahenga waliposema kipenda roho hula nyama mbichi.  Athalia aliona ni bora atumie gharama kubwa kuwasiliana na ndugu zake kuliko kumpoteza Johnson. Laiti kama angelijua kuwa Johnson ni msanii aliyebobea hata asingelijitaabisha ama kweli kupenda karaha ambazo huna budi kufunga kibwebwe ili kuzikabili.

Maisha yanazidi kupamba moto Jackson haachi kumtafuta Athalia kwenye simu. Siku moja alibahatika kumpata Athalia na kumweleza hali ilivyo. Athalia ana hekima akamjibu Jackson kuwa yeye anatumia mitandao mitatu, siku hizo ambayo ni heko, ingia na toka. Jackson alidai kuwa yeye alimtafuta kwenye mtandao wa ingia. Athalia alimjibu kuwa muda mwingi anatumia mtandao wa heko na toka. Lakini alimpa namba zake za simu mbali na kwamba wazo la kurudiana nae halipo kabisa akilini.

Athalia ni mwanamke wa shoka na nyundo kwani alipoona dunia inabadilika rangi katika suala la mapenzi aliamua yeye kujikita katika shughuli zake za kiuchumi. Kila mwaka Athalia analima viazi na hufanya hivyo kitaalamu kabisa. Katika harakati za kupambana na maisha yeye hashtuki kwani kishazoea mazingira magumu na ya amani. Aliona ni afadhali aendelee na shughuli za kilimo mbali na kuwa yeye ni mfanyakazi. Si hivyo tu bali pia anafikiria kuyafikia malengo yake ya kuwa profesa.

Athalia akiwa ametimiza miaka mitano kazini, akafanikiwa akajiunga na chuo tayari kwa masomo. Daktari Mabumo na Mikidadi wakafurahi sana kuona tunu yao inaendelea kuimarika katika ulimwengu wa taaluma. Athalia alijikita katika sayansi ya lugha ya Kiswahili mbali na kwamba amewahi kuandika vitabu vya simulizi. Athalia ana mapenzi ya dhati na isimu ya lugha yake ya taifa la Mafanikio.

Shule ikaanza, pilikapilika nyingi Athalia hazimuishi, yuko busy sana, mara kwenye mihadhara, mara kwenye midahalo, mara maktaba, yote hii ni kutimiza azma yake ya kuwa profesa. Semista ya kwanza inayoyoma kwa kasi, akigeuka huku majaribio mara mazoezi mbalimbali na vyote vinatakiwa kufanywa ili kukamilisha tamrini. Hata hivyo ugumu wa shule kwa Athalia ilikuwa ni sululu ya kumwezesha kuipata lulu iliyofumbatwa na walimwengu wanaoihangaisha akili yake.  Alikomaa kama mama ajifunguaye leba na kufanikiwa kutoka na mtoto ambaye alimsahaulisha masaibu yote. Athalia aliibuka na mtoto wa matokeo mazuri yaliyotikisa nyavu za wahadhiri wake.

Wakati Athalia akiwa anasoma shahada ya umahiri Johnson alikuwa tayari amekwishamaliza shahada yake ya pili ya umahiri mwaka mmoja kabla ya Athalia kujiunga chuo.  Mbali na kwamba Johnson alileta mapozi wakati fulani lakini baadaye aligundua kuwa Athalia alikuwa mtu muhimu sana katika maisha yake.  Johnson aliogelea katika bahari ya mapenzi na ujana akaona hana budi kurudi alikotoka. Alimtafuta Athalia kwa njia ya simu na kumweleza kwa kirefu kuhusu ukweli wa mutima wake.

Ingawa Johnson alieleza kwa kirefu yaliyokuwa moyoni mwake na hisia zake juu ya Athalia, lakini mtu haachi asili yake. Athalia alijihisi ni mtu mwenye mkosi sana kwani kila mwanaume anayekutana naye ana tatizo la hasira na akikasirika anakata mawasiliano. Maelezo ya Johnson kwa Athalia yalikuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Ilimgharimu sana Johnson kumshawishi Athalia mpaka amwelewe. Aliyeumwa na nyoka siku zote hata akiguswa na jani anahisi ni nyoka yuleyule amerejea. Athalia hakuwa na imani tena na Johnson licha ya kuwa na mlolongo wa hoja kama mabehewa ya treni. Athalia alishaumwa na nyoka hata kama Johnson akimaanisha ni kazi bure moyoni mwake anasema tutaona kama kuna ukweli wa mambo, vijana wa siku hizi mna maana kazi kurambaramba asali. Lakini dawa yenu ni sisimizi waliojitwalia eneo la mechi ili mpunguze hiyo rambaramba.

Athalia alimpiga maswali Johnson kama kituo cha polisi, Johnson kwa kuwa anatafuta almasi inayotaka kumponyoka kwa uzembe wa utandawazi akawa mpole mithili ya kondoo aendae kuchinjwa. Athalia akamjibu Johnson kwamba ataamini hayo anayoyanena kwamba ni ya kweli siku ndoa itakapofungwa. Huu ulikuwa mtihani mzito kwa Johnson.

Siku zikaendelea kuyoyoma mithili ya zabibu zitokapo katika msimu fulani kwenye shamba la mizabibu. Athalia aliendelea na shughuli zake za ujenzi wa taifa lake la Mafanikio na uchumi wake. Akiwa kwenye semina ya utumishi wa umma kwa ajili ya kazi maalumu ya uwezeshaji watengenezaji wa taifa la wasomi, alipokea simu. Johnson alimpigia simu Athalia ili kumjulia hali anaendelea vipi. Athalia aliendelea na kazi huku akimjulisha Johnson kila jambo alifanyalo.  Johnson aliamini sasa ameokoka kutoka katika giza la utusitusi mwingi wa mawazo. Johnson kila wakati alituma ujumbe na kupiga simu kwa Athalia kuhakikisha mapenzi yanachipua upya na kurudi katika hali ya awali yakikaza mizizi.

Athalia moyoni mwake ana mawazo lukuki maana kila akiwaza Johnson yuko mbali je anayoyasema yana ukweli wowote? Athalia yuko katikati ya dimbwi la mawazo japokuwa Johnson kila siku anamtia moyo kwa ujumbe na kumpigia simu.

*********************************************

Athalia akiwa katika mwaka wa kwanza chuoni Highway akisomea shahada ya umahiri alifunga pingu za maisha na kijana mtanashati Johnson. Johnson sio kwamba hakumpenda Athalia bali ni ujana uliokuwa ukimsumbua, ama kweli ujana maji ya moto.  Lakini baada ya ndoa yao walipendana kama kumbikumbi.

Waswahili wa Mafanikio husema kila jema lina mapito yake, Athalia aliteseka katika kipindi cha mahusiano yake na Johnson lakini avumiliaye mwisho hushinda. Athalia alipenya katika tundu la sindano hatimaye alifanikiwa kuishi na Johnson jambo ambalo lilionekana kama ndoto. Johnson akifikiria akilini mwake dah! Nilitaka kupoteza hazina ya maisha. Johnson na Athalia sasa ni mke na mume.

Athalia akiwa mwaka wa pili wa masomo yake ya umahiri akabeba mimba na mwishoni mwa semista ya pili akajifungua mtoto wa kike. Familia ya Johnson na Athalia ikaongezeka. Ni furaha ilioje kwa wanandoa hawa. Mungu amejibu maombi yao.

Athalia alipokuwa mjamzito, Johnson alikuwa na kazi ya kumpeleka mkewe chuoni Highway na kwenda kumchukua baada ya masomo, licha ya kuwa alikuwa tayari amemnunulia gari lake. Hata hivyo Athalia licha ya kuwa alikuwa mjamzito lakini alikuwa akifanya kazi yake ya utafiti kwa nguvu na kwa ufanisi mkubwa. Alikuwa akilala saa nane bila hata kuchoka. Hakika mchwa ni mchwa hawezi kulala nje eti kwa kuchelea kachoka bali lazima nyumba isimame tu na yeye ajistiri.

Muda haugandi bali huyoyoma mithili ya mvua ishukavyo toka juu kwa Mungu, Athalia alipomaliza tamrini yake, alianza kuandika pendekezo la utafiti, alijituma na profesa aliyemsimamia alimwelekeza na kumfundisha kwa utashi namna ya kuandika pendekezo na namna ya kuhoji na kujenga hoja. Ama kweli nyota ya mtu haiwezi kuzuiliwa na mtu kwa namna yoyote ile. Athalia alijengewa misingi ya kuhoji vitu hadi akaona kweli taaluma imeiva. Pendekezo likakamilika, akaruhusiwa kwenda kukusanya data uwandani.

Athalia akiwa na ujauzito wa miezi mitatu alianza kukusanya data katika wilaya ya Chanua huko alikutana na Wanyacha. Alikusanya data zake zilizohusu usemaji wa lugha ya Kinyacha. Wazee wa Kinyacha hawakufanya hiana wakafanya kweli, wakampatia data lukuki binti yao na baraka tele katika masomo yake. Miezi miwili Athalia alikusanya data, kisha akarejea chuoni.

Athalia ni jembe, akiwa uwandani akikusanya data alikuwa akiendelea na uchakataji wa data, baada ya kurejea chuoni aliendelea kuingiza data kwenye ngamizi. Hakika kweli penye nia pana njia, tumbo limeanza kuwa kubwa Athalia wala hashituki, yeye na ngamizi, ngamizi na yeye.

Athalia akaandika tasnifu ya utafiti wake akaikamilisha, na kuiwasilisha kwa profesa wake anayemsimamia. Kisha akarejea nyumbani kwake tayari kwa kujifungua. Hakika hesabu nazo zinapanda kichwani mwa Athalia. Alipomaliza tu kuandika tasnifu ya shahada ya Umahiri siku za kujifungua zilikuwa tayari zimetimu.

Athalia alijifungua mtoto wa kike sura na rangi ya baba yake. Hata huulizi mtoto huyu ni wa nani. Like father like daughter. Athalia akaingia chama cha wamama, mambo ndani ya nyumba kuna kichanga, cheupeeeeeeeeee! Jamani kitoto hiki kimezaliwa katika wakati muafaka, mama imebaki kazi ya kufanya marekebisho tu. Kweli malaika huyu kaleta neema ya pekee kwa familia hii. Johnson anampenda mkewe kupita kawaida. Mtoto alipewa jina la Furaha, kwani alionekana faraja kubwa kwa wazazi wake.

Athalia alihitimu shahada yake ya Umahiri kwa daraja la A, huku mumewe akiwa anasubiri kujiunga shahada ya Uzamivu nchini Ukarimu katika chuo kikuu cha Karimiwa. Johnson anaendesha mambo yake kwa mpangilio maalumu. Nafasi za upendeleo kwa akina mama mpaka kwenye familia. Johnson aliahirisha kuunganisha shahada ya tatu mpaka mkewe amalize na kukuza mtoto. Haahaahaaaa! Ama kweli mapenzi moto wa kuotea mbali, Johnson kawa mdogo balaa kwa Athalia anataka kila mahali wawe pamoja.

Katika mwaka wa nne wa ndoa yao, Athalia alikuwa tayari amekwisha kukuza mtoto wake Furaha. Na hivyo alikuwa akijiandaa kwenda kusoma shahada ya uzamivu. Furaha akiwa na miaka mitatu, baba yake alikuwa akimalizia shahada yake ya uzamivu nchini Ukarimu. Familia ya bwana Johnson na mkewe Athalia wanaamini kuwa fahari ya maisha ni taaluma si kwa maana ya kipato bali kuujua ukweli na kuutetea daima. Kwani licha ya kuwa wasomi wanaamini mabadiliko ni sera na utekelezaji wake juu ya kile unachokiamini. Familia hii wanatiana moyo sana katika elimu kama watianavyo moyo wasafiri wa kwenda mbinguni.

Katika kusoma kwake Johnson amewahi kusoma katika nchi ya ukarimu na nchi ya Mpende Jirani. Akiwa nchini Ukarimu alisoma shahada ya Umahiri ya Elimu Maalumu. Huko nchini Mpende Jirani alisomea shahada ya Umahiri ya Mitaala ya Elimu katika nchi zinazoendelea. Mkewe alijikita katika taaluma ya lugha Kiswahili ya taifa la Mafanikio pamoja na lugha nyingine za Asili zinazozungumzwa nchini Mafanikio.

Johson alisoma shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Highway. Mbali na hilo yeye ni mtaalamu wa sayansi ya viumbe wa zamani. Huko ndiko walikokutana na Athalia na kuanza safari ndefu mno ya maisha. Athalia na Johnson wamepitia mambo mengi, katikati ya bahari yenye dhoruba na mawimbi yasiyo kifani, milima mithili ya ukuta wa Yeriko au Sobibo wamepanda, mabonde wamepita lakini mwisho wa yote wanaishi pamoja.

Furaha naye sasa ni maneno tu, mara mom I need some chips, mara I want to go to school. Hakika ulezi shughuli ni vurumai kubwa lakini ndilo jukumu ambalo Mungu kampa mwanadamu. Jukumu lisiloachanika kwa mzazi na mtoto lenye hazina ya upendo ambao umejengwa na kuimarishwa kutokana na uzazi wa uchungu. Athalia na mumewe walipoona Furaha maneno yamezidi waliamua kumpeleka shule ya awali ya st. Helen aendelee kujifunza huko. Furaha ana akili na mjanja mithili ya sungura na walimu wake wanampenda sana kwa sababu ni mwepesi wa kuelewa. Furaha ana maswali mithili ya askari upepelezi kama mama yake. Furaha ana umbo la mviringo kama wazazi wake ila sura ya baba yake. Ukimwona Furaha utajua Johnson huyu hapa, tofauti yao ni kwamba Furaha ni mdogo, wa kike na Johnson ni mtu mzima.

Athalia ana mapenzi ya dhati kwa mumewe na mwanawe. Kila asubuhi aendapo kazini lazima awe tayari amemwandalia mumewe kifungua kinywa pamoja na chakula cha mwanawe. Athalia anaelewa mwanawe Furaha anapenda chapati na maziwa, lakini kama mama lazima ampe na yai moja kila asubuhi. Mumewe ni mpenzi wa ndizi mzuzu zilizopikwa kwa nazi. Asubuhi huwa anapenda apate kifungua kinywa maziwa na ndizi mzuzu. Hivyo Athalia huandaa kwa ajili ya familia yake.

Athalia akiwa na majukumu hayo yote lakini aliweza kuihudumia na kuitunza familia na kukusanya data za utafiti wake na kukamilisha uandishi wa tasnifu yake. Tasnifu ilikubaliwa na maprofesa pamoja na madaktari alipoiwasilisha kwao. Athalia alifanya vizuri sana katika shahada yake ya pili. Lakini bado ndoto za Athalia hazijatimia kwani anataka kuwa profesa, hali ya upepo inaashiria wazi kuwa siku moja atafikia uprofesa kwani ana bidii ya mchwa.