Chereads / penzi la bahati / Chapter 52 - chapter 51

Chapter 52 - chapter 51

Imekuwa ni siku nne Sasa tangu Nzagamba aondoke mawindoni,Tulya anatumia muda mwingi kufinyanga vyungu na shughuli zingine asije akaanza kulia kwa kumkumbuka,na wasiwasi kuwa atakuwa anaendeleaje huko aliko.Akiwaza hilo linampa huzuni zaidi kwani hali anaijua mwenyewe haitaji mtu amwambie.

Ana nawa mikono yake anachukua kibuyu anachowekeaga maji Ili anywe anaambulia patupu.Anajikongoja pale chini anatoka kwenye kibanda Chake Cha kutengenezea vyungu kuelekea ndani akachukue maji kabla hajapiga hatua zaidi anasimama na kukunja uso akiangalia chini ya mti alipokuwa amekaa mama mkwe wake." kaenda wapi?" anajiuliza akiangalia huku na kule.

Anajiuliza kama mawazo yake yalikuwa mbali kiasi hicho asimuone akipita alipo maana kama Bibi sumbo atakuwa ndani ni lazima angepita alipo na ni sio rahisi yeye asimuone.

" mama" anaita akielekea ndani kwa hatua za haraka.Anaingia ndani kwa Bibi sumbo lakini hamuoni,anajaza maji kwenye kibuyu na mengine anakunywa " kaenda wapi?" anaongea akiingiwa wasiwasi maana Bibi sumbo amekuwa hayuko vizuri tangu Nzagamba aondoke na amemshauri akae nyumbani lakini mama mkwe wake miguuni kama muuza chumvi anahofia asipouza watu watakula vipi chakula.

Anatoka ndani mkono wake wa kulia ukifuta mdomo wake mwingine umeshikilia kibuyu macho yake yakiangaza huku na kule kama atamuona mama mkwe wake lakini yanatua kwa mtu mwingine akiwa amesimama karibu na mlango mkubwa wa uani. licha ya kumpatia mgongo Tulya anajua tu ni nani.Anaendelea kumwangalia mtu huyu akijiuliza aingie au asiingie " amefata nini tena huyu?" anajiuliza sura akikunja kwa maswali na kuanza kupiga hatua aliposimama mtu huyu.

" Lindiwe?!" anaita na Lindiwe anashtuka kama kakamatwa akiiba asali ya Babu akijiambia ni mara ya mwisho Leo lakini inaibuka kuwa ni arobaini yake.

" unashtuka nini?" Tulya anamuuliza na Lindiwe anashika moyo wake akijaribu kuweka sura sawa." umenshtua" anaongea akiangalia huku na kule. " umekosa au? na unamwangalia nani?" Tulya anamuuliza baada ya kumuona macho yake hayatulii.

" mhh? amna kitu." anamjibu.

" nilikwambua vyungu bado,nikichoma nitakuitia au nitakupa taarifa siku kabla ya kuchoma Ili vikipoa uje kuangalia" Tulya anamjibu akikumbuka siku mbili zilizopita Lindiwe alikuja kutafuta vyungu na kumfanya Tulya ajiulize siku zote alikuwa ananunulia wapi na ilikuwa kama hivi.

" hodi" Tulya akiwa ndani kwake anasikia sauti ndogo ikitokea karibu na mlango wake. mwanzo anahisi anasikia vibaya anaendelea na kazi yake ya kushona kaniki rubega ya mume wake." hodi" sauti inajirudia tena anaweka kaniki yake kitandani na kutoka sebuleni na kusimama mlangoni akichungulia nje anamuona msichana mrembo hajawahi kumuona hapa kijijini tangu aje.

" karibu" anajibu akimwangalia msichana huyo mwenye sura nzuri rangi yake sio nyeusi Wala sio nyeupe sana ngozi yake ya kuteleza. sketi yake iliyotengenezwa kwa ngozi ya pundamilia ikiwa imemkaa vizuri kiunoni ikiwa imefika juu ya magoti yake kifuani saa sita ikiwa imetulia na kama kufanya makusudi hajayakaza kwa kitambaa chake.

" asante" ukaguzi wake unasitishwa na sauti hiyo ndogo na tamu macho yake yanaenda juu na kumwangalia usoni " ni mrembo" anajisemea moyoni.

" habari za hapa?" anauliza msichana akishika shika vidole vyake macho yake yakiwa na aibu na Moja kwa Moja Tulya anajua hajazoea kuongea na watu au ni mpole kupitiliza au Kuna kitu kingine zaidi.

" nzuri karibu" anamwitikia akiwa bado kasimama mlangoni pasipo kumkaribisha Ndani.

" habari yako?" anasikia sauti nyingine na macho yake kukimbia haraka kwa mtu mwingine ambaye alikuwa hajamuona mda wote huu.Lindiwe.

" nzuri, karibuni" anaitikia akitoka nje kabisa akijaribu kuficha mshangao wa kumuona Lindiwe nyumbani kwake akiwa na mtu asiyejulikana. macho yake yanatoka kwa Lindiwe na kurudi kwa msichana aliyengozana nae au anayeonekana kama ni mkuu wa msafara.

" Mimi naitwa Tausi" anajitambulisha msichana kama kumkumbusha Tulya jina lake.Tulya anajaribu kufikiri alisikia wapi jina hili lakini bado hakumbuki.Msichana anamuona Tulya akihangaika kumkumbuka anaamua kumpunguzia ghadhabu.

" ni mke wa Mkita"

Macho yanamtoka pima Tulya " ohh mizimu ya baba yangu mzazi,yule chizi Mkita alihonga nini mizimu mpaka kuibuka na mke kama wewe " Anaongea Tulya kwa sauti pasipo kujua na kumfanya Tausi kuangalia chini kwa aibu.

" aaa usijisikie vibaya namaanisha wewe ni mrembo sana.." anatulia kidogo "....na uko tofauti na mumeo,nimekusikia mara nyingi lakini umekuwa tofauti na nilivyokuwa nakufikiria kichwani" na uko tofauti na mumeo mdomo kama chujio anawaza Tulya kichwani kwake.

" asante" anajibu Tausi akijaribu kumwangalia Tulya machoni lakini inakuwa ni kazi ngumu anaishia kuangalia kidevu isitoshe Tulya anamzidi urefu kidogo.

" we hujamuona mke wangu,ni mrembo kama kashuka duniani" Tulya anakumbuka maneno ya Mkita ambayo siku zote alikuwa anayaona kama bwabwaja zake za Kila siku tu.Tabasamu linatokea mdomoni kwake akifikiria maisha Yao wanaishije mwingine anaongea kama debe la kukimbizia nyani asile mahindi na mwingine mdomo mzito kama kang'atwa na nyuki.Anauhakika kwa wazo lake angekuwa peke yake angecheka kwa nguvu kama chizi lakini anaamua kucheka baadae kwa sasa asiwatishe wageni wake.

" nakuja" anawaambia na kuelekea nyumbani kwa mama mkwe wake na baada ya dakika anatoka na mkeka.

" njoeni huku nyuma Kuna kivuli" anawaambia na kwa kuwa ilikuwa ni jioni anaona ni bora wakarithi kivuli Cha Bibi sumbo kwa mda kwa kuwa hayupo.

"sisi hatukai" anajibu Tausi lakini Tulya kama Tulya tayari alishaingia kwenye kibarua Cha mjue mke wa Mkita kwa hiyo hakuwa tayari kukiacha.mwanamke mpole Kijiji kizima kumuona ni mpaka kakakuona atoe maono na Leo ndio siku yenyewe.

" haraka ya nini wakati najua utaenda kujifungia ndani kwako tu,njoeni tuongee huku kidogo" anaanza kutembea kuelekea uani macho yake yakienda kwa Lindiwe akijiuliza amefuata nini.

Baada ya maongezi Tausi anamwambia kuwa Mkita alimwambia wakiishiwa chakula aje hapa.

" yule mshenzi Mkita utadhani aliacha ghala hapa" anawaza Tulya moyoni.Mkita alifanya hivyo kwa sababu alijua Tulya hawezi kumnyima mkewe chakula.

Anamtolea mtama na wote watatu wanasaidiana kusaga kwenye jiwe na kumfanya Tausi awe na unga wa kulisha familia yake kwa siku tatu.

" una mboga?" Tulya anamuuliza na Tausi anatikisa kichwa kukataa.Tulya anamtolea ndege waliokaushwa na kumpatia. Lindiwe nae akimwambia apitie nyumbani kwake akamuongezee.

" nimekuja kutafuta chungu" Lindiwe anaongea baada ya kumuona Tulya akimwangalia sana.Lakini ukweli ni kuwa alimuona Tausi akipita nyumbani kwake akamuuliza anaenda wapi alipomwambia anakuja huku akaamua kuongozana nae.

Tulya anamjibu kuwa bado anatengeneza akichoma atamwambia aje kuangalia.Hivi ndivyo walivyoishia.

Kwa Sasa Tulya anaendelea kumwangalia Lindiwe aliyesimama mlangoni kwake pasipo kumkaribisha Ndani.

" nimekuletea hii" Lindiwe anampatia mfuko wa kaniki na Tulya kumwangalia kwa maswali anaweka kibuyu chake chini anachukua mfuko na kuangalia ndani anakutana na shanga zilizotungwa tayari.

" nini hiki?" anamuuliza

"nilibadilishana shanga na mama Nsio,nimetengeeza zangu zikabaki nikakutengenezea na wewe" anajieleza Lindiwe.

"kaja na mpango gani huyu?!"anajiuliza Tulya moyoni akiendelea kuziangalia shanga.

Kama kumsoma mawazo Lindiwe anaongezea " usinielewe vibaya,nimekuletea ni kama shukrani tu kwa siku ile mtoni"

Tulya anamwangalia nakusema " siku ile niliongea kwa sababu kilichokuwa kinaendelea hakikuwa Cha kiungwana hata angekuwa mtu mwingine ningeingilia walichokuwa wanakifanya hakikuwa utu kabisa,kwa hiyo haina haja ya kuniletea hivi vitu kwa sababu ya hilo,chukua na uondoke nyumbani kwangu,nikimaliza vyungu nitakwambia uje kuchukua ikiwa bado unataka"

Anampatia mfuko na kugeuka kuondoka lakini anasimama baada ya Lindiwe kuongea " sina mtu wa kuongea nae,naweza kuwa rafiki yako"

Tulya anageuka na kumwangalia na anashukuru mungu alikuwa hajabeba kibuyu chake kwani anauhakika ingekuwa ni siku yake ya mwisho maana angekiangusha kwa mshtuko.

" unanitania au?!" anamuuliza na Lindiwe anatikisa kichwa kukataa machozi yakimlenga.

" hivi umesahau uliyonifanyia au umeamua kujitoa ufahamu?"

" hapana sijasahau,na naomba unisamehe sana lakini Sasa kweli nataka kuwa rafiki yako"

Kipigo kitakuwa kimefika kwenye ubongo na akili zimeanza kuyumba anawaza Tulya moyoni akiendelea kumwangalia Lindiwe kwa kumpima.