Reuben na Joy waliwasili hospitali jioni. Mida ya kuona wagonjwa ilikuwa imekwisha lakini wao walikuwa na kibali maalumu. Walitembea nyuma ya Paul taratibu wakimfwata kuelekea chumba cha Cecy. Paul alikuwa na uchovu ila alijitahidi kutokuonesha. Walipita wodi mbalimbali kabla ya kumfikia Cecy.
Paul alimlipia chumba cha peke yake. Kilikuwa na ubora kuliko vyumba vingine. Kitanda cha Cecy kiligeukia dirisha na muda walioingia alikuwa akitazama jinsi mwezi ulivyokuwa ukichukua nafasi ya jua.
Wote walijongea kitandani, Paul akiwa msitari wa mbele;
"Cecy.", aliita taratibu, "Una wageni.",
Cecy hakuweza kugeuza shingo hivyo ilibidi Reuben na Joy wasogee karibu ili waweze kuonekana.
"Pole kwa ajali, Cecy. Naitwa Reuben, mpelelezi mkuu wa serikali. Huyu ni msaidizi wangu, anaitwa Joy.", Reuben alifanya utambulisho,
"Nashukuru kwa ujio wenu.", alisema Cecy,
"Paul anasema kuna kitu muhimu unataka kutuambia.",
"Ndiyo. Ni kuhusu aliyesababisha ajali yangu.",
"Nani?",
"Leah.",
Reuben alivuta pumzi na kusogea karibu zaidi, "Kwanini unahisi ni yeye?",
"Naomba nimjibie hilo swali kwasababu hatoweza kuzungumza kwa muda mrefu, ila atanikosoa nikikosea.", alisema Paul,
"Endelea.", Reuben alimruhusu,
"Okay. Mlisikia habari aliyotangaza Montana kuhusu Leah?",
"Kwamba mnapeana talaka?", Joy aliuliza,
"Ndiyo, na sababu aliyotaja ni kuwa nampenda mwanamke mwingine. Mwanamke huyo ni huyu hapa, Cecy.",
"Tulisikia kuwa alikuwa jela.", alisema Reuben,
"Ametoka leo asubuhi na ndipo ajali ilipomkuta.",
"Ripoti inasema gari iliyomgonga ilikimbia hivyo hakumuona dereva. Kwanini anahisi ni Leah?",
"Siku chache zilizopita Leah alikwenda jela kumuona Cecy. Leah alimjaza mwenzie uongo na kuna vitu alimtishia vilivyopelekea Cecy kutaka kuvunja mahusiano yetu. Leo asubuhi Cecy alipotoka jela alipokea ujumbe huu kutoka kwa Leah.",
Paul alifungua ujumbe ule na kumkabidhi simu Reuben. Reuben alisoma ujumbe ule kwa makini bila kuonesha ishara yoyote ya mshangao. Alipomaliza alimpatia simu ile Joy,
"Mna uhakika namba hiyo ni ya Leah?", aliuliza,
"Naijua namba ya mke wangu, detective. Hiyo ni namba yake.",
Ila bado Reuben hakuonesha kuridhishwa na maelezo. Moyo wake ulikuwa mgumu.
"Paul, naomba nikuulize kitu.", alisema,
"Uliza tu, detective.",
"Mahusiano yako na Leah sasa hivi yapoje?",
"Hatupo sehemu nzuri.",
"Mnalala chumba kimoja?",
"Hapana. Tunaishi nyumba tofauti.",
"Mara ya mwisho kukutana nae ilikuwa lini?",
"Siku nne zilizopita kwenda kutaka kujua ni nini aliongea na Cecy.",
Reuben alimgeukia Cecy, "Mama, samahani, ila unaweza kutuambia ni nini Leah alikwambia?",
Cecy alimtazama Paul kwanza kabla ya kurudisha macho yake kwa Reuben, "Leah aliniambia kuwa Paul hanipendi bali anataka kunitumia.",
Paul aliumizwa na hiyo kauli.
"Aliniambia kuwa ananijali mimi kama mwanamke mwenzie na ndio maana amenionya. Pia aliniahidi kunipa kazi nikitoka jela ila sharti lake lilikuwa ni mimi kuvunja mahusiano na mawasiliano yote na Paul. Akanipa namba yake na kuniambia nimtafute mara tu nitakapokuwa huru.",
"Ukiachana na hiyo message, Leah amekutafuta tena?",
"Hapana.",
"Asante mama angu, pumzika.",
Reuben alimuonesha ishara Paul ya kuwa watoke nje. Walimwacha Cecy na Joy ndani. Walisimama koridoni, nje ya chumba cha Cecy;
"Paul, niambie ukweli. Unampenda Cecy?", Reuben aliuliza,
"Ndiyo, sana.",
"Mke wako je?",
"Kitu nachoweza kusema ni kwamba nilikuwa namjali sana mke wangu, lakini baada ya yeye kuonesha huu upande wake, sina hata chembe ya upendo kwake tena.",
"Tukifanya uchunguzi na kugundua kuwa Leah ndiye amesababisha hii ajali ya Cecy kwa lengo la kumuua, ataenda jela kwa kipindi kirefu sana. Upo tayari kumuona mkeo akipitia hayo?",
"Kama ameweza kutaka kumuua binadamu mwenzie, basi anastahili kuadhibiwa.",
Reuben hakuwa na lingine la kusema. Kesi ilikuwa inaenda ingawa matawi yake yalikuwa ni mengi.
…
Cecy alishituka kutoka usingizini baada ya kuota ndoto mbaya. Kwenye ndoto alikuwa akikimbizwa na simba mkubwa mwenye muungurumo mzito. Kila alipokuwa akigeuka nyuma, simba yule alionekana kumkaribia. Bahati mbaya Cecy alijikwaa kwenye mzizi wa mbuyu uliochipuka kwenye njia. Alianguka kifudifudi na kuanza kutambaa kama mtoto huku akipiga mayowe ya msaada.
Alipogeuka nyuma alishangaa kuona simba amesimama akimuangalia kwa macho ya ukali na ghafla mwili wa mnyama yule ulibadilika na kuwa mwanadamu. Cecy alipigwa na bumbuwazi. Ni uchawi wa aina gani huo? Mtu yule alisimama kwenye mwanga na kujidhihirisha kuwa ni Leah. Alikuwa akitabasamu, mkononi akiwa ameshika bastola.
Cecy alipiga magoti huku machozi yakitiririka;
"Nisamehe. Naomba usiniue.", Cecy aliomba toba,
Leah alinyanyua mkono na kutegesha bastola kwenye kichwa cha Cecy, "Muda wako umekwisha.",
Leah alipofyatua bastola ndipo Cecy aliposhtuka kutoka usingizini. Mwili mzima ulilowa jasho. Neva zake zilisisimuka kama kapigwa shoti ya umeme. Bado alikuwa hospitali na hakuweza kunyanyuka kitandani. Ilibidi tu ajitulize mwenyewe. Miale ya jua ilipenya na kufanya mwanga chumbani. Tayari ilikuwa asubuhi tena iliyochangamka.
Hodi ilibishwa mlangoni. Cecy alijua kuwa ni nesi wake amekuja kumjulia hali. Mlango ulifunguka kisha kufungwa. Sauti iliyofuata haikuwa iliyozoeleka. Masikio yake yalikamata sauti ya skuna zikigongasakafu ile yenye marumaru. Kwa ujuzi wake, hakuna nesi duniani aliyevaa skuna akiwa zamu. Ni mgeni gani huyo? Alishindwa kugeuza shingo yake hivyo hakuwa na budi kusubiri mgeni huyo ajioneshe mwenyewe.
Hatimaye Leah aliwasili kwenye kitanda cha Cecy na kusimama mbele yake. Alivaa mavazi ya kupendeza huku akiwa na amebeba maua aina ya mawaridi meupe na mekundu. Cecy alitoa macho kama mjusi aliebanwa na mlango. Kwa mara nyingine tena alikumbuka ndoto yake. Je, Leah amekuja kummaliza kama alivyoota? Mshtuko ulimfanya ashindwe kufungua mdomo wake.
Leah hakuelewa kwa nini Cecy alimtazama kwa hofu.
"Nini shida, mamy?", aliuliza Leah kwa upole, "Nimekuja kwa nia nzuri.",
"Na-nakuomba usini-usiniue.", Cecy aliongea kwa woga na sauti yake ilikuwa ya chini hivyo Leah hakusikia,
"Nimepiga simu jela nikaambiwa ulitoka jana. Pole sana na ajali, mamy. Yani umekaa jela kipindi kirefu mpaka umesahau sheria za barabarani?", Leah alitania, lakini alishangaa kuona Cecy akibubujikwa machozi.
Leah aliweka maua dirishani na kumsogelea Cecy karibu,
"Cecy, nini tatizo? Nikuitie daktari?",
"NISAIDIENI!", Cecy alipayuka kwa nguvu, "NAKUFAA! NISAIDIENI!",
Leah alijaribu kumtuliza Cecy kitandani akifikiri labda ni dawa anazopewa ndizo zilizopelekea awe namna ile. Lakini bado Cecy alipiga yowe mpaka watu walipowasili. Alikuja daktari mmoja na manesi wawili, nyuma yao alikuwa Reuben na Joy na askari wachache.
Leah aliachilia mikono ya Cecy na kusimama wima, "Sijafanya kitu.", alijitetea kujiweka sehemu salama,
Huku daktari na manesi wakifanya juhudi kumuhudumia Cecy, Leah alijikuta kwenye mikono ya askari. Alipigwa na butwaa, usoni alivaa swali, "Nini kinaendelea?", aliuliza,
"Leah Shahidi, upo chini ya ulinzi kwa kusababisha ajali ya Cecilia.", Reuben alitamka huku akiifunga mikono ya Leah kwa pingu,
"What?", Leah alishangaa, "What are you talking about?",
"Tunza maelezo yako. Utatuelezea kituoni.",
Askari walimswaga Leah nje ya wodi mpaka kwenye difenda. Watu walichukua video kwenye simu zao na kuzirusha mtandaoni. Baada ya muda mchache, habari za Leah kukamatwa na jeshi la polisi zilikuwa zikisambaa nchi nzima kwa kasi.
***