Fahamu ilianza kumrudia Leah polepole. Alihisi mikono na miguu yake kisha kufumbua macho taratibu. Alijikuta kwenye chumba cha hospitali, upumuaji wake ukisaidiwa na mashine ya oksijeni. Alikuwa na maumivu makali kwenye maeneo ya shingo na mgongo. Kitu cha mwisho kukumbuka ilikuwa ni sura ya Paul iliyokunjika kama mbogo na sauti nzito iliyomuasa akate tamaa na kuaga dunia.
"Nipo hai?", Leah alijiuliza akilini, "Nipo hai.",
Alijaribu kunyanyuka ili akae kitako lakini alishindwa. Wakati akipepesa macho alikutana na Cecy. Cecy alikuwa kwenye kiti cha matairi. Bado mguu na mkono wake ulikuwa na ogo. Kwa shida kidogo, Cecy alijisogeza mpaka pembezoni mwa kitanda cha Leah;
"Karibu tena duniani.", alisema Cecy, "Fahamu zako zilipotea kwa wiki mbili. Madaktari walijua tumekupoteza.",
"Wiki mbili?", Leah alishangaa, "Kivipi?",
"Daktari anasema ulipofikishwa hospitali, mapigo yako ya moyo yalikuwa yamefifia sana. Walifanya kazi kubwa kuyarudisha. Na mwili wako pia ulikuwa umechoka mno. Ni miujiza kuwa upo hai.",
Leah alikaa kimya kwa muda. Ilikuwa ngumu kuamini kuwa yupo hai.
"What happened nilipokuwa sijaamka?", aliuliza,
"Janat yupo jela, miaka 20.",
"Babra je?",
"Babra na wenzie wamewekwa ndani, miaka mitatu.",
Japokuwa jina lilimtia ukakasi, bado aliuliza, "Na Paul?",
"Paul amehukumiwa miaka 30 kwa kifo cha Montana na mama mwenye nyumba. Bado ana kesi ya kusababisha ajali yangu na kukusudia kukuua. So miaka itaongezeka.",
Lakini habari hiyo haikumpa furaha kama alivyotarajia. Hakutaka kuamini kuwa stori ya mapenzi yao ndio imeishia hapo; yeye akiwa hospitali na mwenzie akiwa jela. Ni jambo la kuhuzunisha, na lilimuumiza. Mume wake wa miaka kumi, mfanyakazi wake wa miaka nane, ndoa yake, msingi wake, vyote vilikuwa vimepotea.
Leah alilia sana bila kujali macho ya mtu. Alilia kwa uchungu, tena kwa sauti. Kumbukumbu zilikuwa kama silaha, hata zile zilizokuwa za furaha.
Cecy hakuweza kumbembeleza kwani alitambua kuwa kuna wakati kutoa machozi ni muhimu. Moyo wa mwanadamu hauna mdomo, hivyo unazungumza kupitia machozi. Huzuni, hasira na majuto huweka uzito moyoni. Ni vyema kulia ili kuondoa mzigo huo. Na ndicho kitu Leah alichokuwa akifanya.
Ukweli ni kwamba alikuwa radhi kufariki kuliko kuishi kwenye dunia iliyojaa maumivu. Hakuona uwezekano wa kusonga mbele huku mambo mengi sana yakimdidimiza. Lakini siku zote kuna njia.
…
Baada ya siku tatu, Leah alipata nafuu na kupewa ruhusa ya kuondoka hospitali. Alipokuwa akijiandaa kwa msaada wa nesi, alipata wazo;
"Nesi.", Leah alianza,
"Abee, kuna kitu unahitaji?", nesi aliuliza,
"Kuna watoto waliozaliwa na kutelekezwa hapa hospitali?",
"Wapo. Wote wanategemea msamalia mwema aje kuwaokoa.",
"Naweza kwenda kuwaona?",
"Bila shaka.", nesi alisema kwa furaha, "Kila mtoto anahitaji familia. Natuamini ukienda utakutana na mtoto ambaye atakuwa familia yako.",
Leah alitabasamu.
...
MWEZI MMOJA BAADAE
Paul alitembea taratibu nyuma ya askari magereza. Aliambiwa kuwa ana mgeni lakini hakujua ni mgeni yupi. Walipowasili dirishani alishangaa kumuona Leah. Leah alikuwa amebadilika na kuonekana mwenye furaha na amani. Paul aliketi bila kupepesa macho.
"Leah?", hakuamini macho yake,
"Paul. Za siku?", Leah aliuliza huku akitabasamu,
"Siku zinaenda. Umebadilika sana.",
"Nimekuwa mama.",
"Unasema?",
Leah alitoa simu yake na kwenda kwenye picha kisha aligeuza simu yake kumuelekea Paul. Kwenye kioo ilikuwa picha ya mtoto mchanga akiwa amelala.
"Anaitwa Giselle. Ametimiza miezi mitatu jana. She's the best thing that's ever happened to me. I'm lucky I found her.",
Paul alilengwa na machozi. Leah alirudisha simu kwenye pochi na kutoa bahasha kubwa. Bila kuchelewa Paul aliikumbuka bahasha ile maana ilikuwa na muhuli wa ofisi aliyokuwa akifanya kazi.
"Nimeweka sahihi yangu.", alisema Leah, "We're finally divorced. Hatudaiani. Nyumba ya Buyuni na magari manne yote nimekuachia. Mama yako yupo anakutunzia. Nahisi sasa hivi ni salama kusema kuwa tumemalizana. I'm happy and I wish the same for you.",
Paul alianza kulia, "Leah, nisamehe mama. Mimi ni mtu mbaya niliyekupa maumivu makali mno. Naomba unisamehe.",
"Paul, yameshapita. Tusonge mbele. Nimekuja tu kukwambia hivyo. Sidhani kama tutaonana tena, but if we do, let's be strangers.",
Leah alinyanyuka na kuondoka. Haikuwa kweli kwamba amesonga mbele na amesahau yote yaliyotokea. Lakini hatua moja huleta nyingine. Taratibu alikuwa akisogelea mwanga. Sasa alikuwa na familia na mtu aliyempa kusudi la kuamka kila asubuhi na kwenda kupambana.
…
Annabella alisafiri kwenda Italia kukutana na binti yake rasmi. Suzy hakutaka kufanya kazi chini ya binamu yake hivyo alianzisha kampuni nyingine na kuapa kuifikisha kileleni. Alijua itachukua muda lakini alijipa moyo na kutokata tamaa.
Kampuni ya Janat ilifungwa rasmi na waziri mkuu alivuliwa madaraka kwa kosa la kuficha dhambi za Janat. Mwishowe kila mtu alibeba kikombe chake na kupiga hatua kwani maisha hayarudi nyuma, bali yanasonga mbele.
***
~MWISHO~