Chapter 238 - BABA YAO

Kichwani akakumbuka maneno aliyomwambia BM siku ile alipoonana na Ed

"Yule kijana anakufaa, usimuache"

"Oooh Mungu wangu haipaswi Allan kunipenda" akawaza

Lakini alipoendelea kusikiliza, mapigo yake yaliongezeka na bado alihisi joto japokuwa kulikuwa na kiyoyozi. Mwisho kama mtu asiyejielewa akainuka akisahau kuwa siri yake sasa ilikuwa kwenye hatua ya kufichuliwa

Akaelekea ofisini kwa Allan huku moyoni hisia za mapenzi zikimrarua kama simba anavyorarua mawindo aliyokamata

************

Edrian na Aretha walitumia muda uliobaki kufurahia maisha kwa kufanya mambo waliyopenda kufanya kwenye milima hii ya Bluu. Walijifunza kuteleza kwenye barafu, kucheza muziki kwenye barafu na mengine mengi.

Aretha alikuwa mwenye furaha ipitayo maelezo na mara zote yeye ndie alimkumbatia Ed, akambusu hadharani, akimuomba mara kadhaa walale pamoja japokuwa walikusudia kutoruhusu tendo la ndoa kabisa hadi watakapotambulisha uchumba wao. Wakawekeana ahadi iwapo wangetimiza hilo basi kila mmoja angemfanyia mwingine kitu ambacho atakitaka.

"Kwa hiyo unataka tutangaze uchumba tukifika eeeh?" Ed akamuuliza huku akiegama kwenye kiti katika mgahawa uliokuwa pembeni kidogo ya eneo la michezo ya barafu hapo Blue Mountains. Walitumia muda huu wa jioni kutoka pamoja baada ya mizunguko ya mchana kutwa.

Aretha akatikisa kichwa kukubaliana na kile Edrian alichosema kisha akaachia tabasamu..

"Retha, unajua nikitangaza uchumba unatakiwa kuwa tayari kwa harusi mwezi mmoja baadae eeh?" Akauliza Edrian pasipo kuondoa tabasamu lake usoni ni wazi alitaka kuhakikisha Aretha anafanya maamuzi ambayo hatayajutia wala kuona kama anasukumwa sukumwa

"Rian, kwani kuwa mke wako ni jambo la kufikiri sana kwangu! Hapana. Tufanye tunachoweza kufanya ubaya usije ukatafutwa kutuzuia" Aretha akamjibu

Edrian akamnyooshea mkono naye Aretha akampatia wake "Hujui ni kwa kiasi gani maneno haya uliyosema yananipa kujiona ni mwanamume bora sana kukupata wewe"

Aretha akatabasamu aliposikia maneno hayo

"Tukirudi Retha, maisha yangu yatabadilika sana na hakika na kwako pia. Uwe tayari, dunia yetu inatusubiri!"

'Excuse me sir, your order is here" mhudumu wa kiume alisimama pembeni yao na kusababisha wakatishe mazungumzo yao..

Edrian akampa ishara aendelee kuweka mezani huku akimtazama Aretha kwa tabasamu la furaha.

Wakaendelea na chakula hadi walipomaliza

"Rian" Aretha akamuita

Akamtazama na kumpa ishara aendelee

"Naogopa iwapo ndugu zako watauliza kwa habari ya baba yangu" Aretha akamwambia akionesha wazi wasi wasi aliokuwa nao japo alitaka kwa hali zote awe na Edrian..

"Retha kwa nini uwaze hivyo? Mama alikuuliza?" Edrian akauliza huku akiweka mikono yake juu ya ule mmoja wa Aretha

"Hapana Rian lakini inawezekana wakauliza, lazima kuwa na jibu la kuwaambia"

"Sio lazima wajue, na kama watauliza mama atawapa majibu" Ed akamjibu

"Mama, aahmm kweli japo sijui kama watafurahia majibu yake linapokuja suala la baba" Aretha akainama chini

"Lakini bado una nafasi Retha yaku__"

"Hapana Rian, sio sasa" Aretha akamkatisha Ed kabla ya kumaliza

Ed akashusha pumzi "Basi sawa"

Aretha akashtuka, "nisamehe Rian"

"Hujanikosea hata kidogo, ulikuwa unanielezea kile unachojisikia. Nimekuelewa princess" Ed akamjibu kumuonesha hakuwa na shida yoyote kwa namna alivyomjibu..

"Retha unapenda kuwa na watoto eeeh?" Akauliza Ed

"Eeehm" Aretha akamtazama kama mtu ambaye hakuelewa alichoulizwa

"Watoto wetu Retha" akatabasamu

"Oooh aaah napenda watoto ila sijui kama ninaweza kuwa mama mzuri" Aretha akajibu

"Kwa nini usiwe mama mzuri wakati una mama mzuri anayekulea?"

"Hhaaa huwa sijui kuwa rafiki wa watoto, nahisi ile kazi ya kumnyamazisha mtoto sijawahi kufanikiwa" Aretha akawa muwazi kwa Ed. Ni kweli katika mazingira ya ukuaji wake alikuwa na ushuhuda mbaya juu ya kubezwa na kuchekwa na watoto wenzie. Mwanzoni alijaribu kufanya marafiki kadhaa lakini walipojua changamoto yake katika kuzungumza ndipo walianza kumzomea na kumcheka. Akaamua kukaa mbali na watoto, hivyo akawaogopa.

"Hautakuwa peke yako lakini, baba yao nitakuwepo" Ed akamwambia huku akitabasamu