Ilichukua masaa manne kwa Li kupumzika, mara alipoamka akakimbilia chumbani kwa Beruya kuangalia hali yake, lakini hakuwepo chumbani. Mapigo ya moyo ya Li yakaongezeka hakuangalia popote akatoka na kushuka ngazi huku akiita
"Mama"
Mama yake akaitika kutokea sebuleni naye Li akafuata muelekeo wa sauti na alipotokea sebuleni mama yake alikuwa ameketi kwenye kochi huku macho yake akiyaelekeza kule Li alipotokea
"Mama, Beruya ameondoka?" Akauliza huku akionesha wasi wasi
"Li umekurupuka ndotoni au aisee" mama akamwambia huku tabasamu lake likionesha utani, Li akashusha pumzi kuonesha hakuwa tayari kufanya utani akaita kwa sauti
"Mama, Beruya yuko wa__" kabla ya kumaliza mlango wa jikoni ukafunguliwa na Beruya akaingia akiwa amebadilisha nguo na kuvaa nguo ambazo Li aliziagiza kwa ajili yake kabla ya kulala. Alivaa gauni rangi ya kahawia ambalo lilikuwa si refu sana. Nywele zake alizichana na kuziachia zianguke kwa nyuma. Japokuwa hali ya uso wake bado ulikuwa na dalili za athari ya ile dawa lakini alionekana bora zaidi ya alivyokuwa amelala.
Li akamtazama alipopiga hatua akisogea alipokuwa
"Huyo hapo maana unataka kunirarua na sijui kosa langu ni kumpokea Beruya au"
Li akarudisha macho kwa mama yake huku akijaribu kuwasiliana na mama yake abadilishe mazungumzo..
"Mama asante sana kwa chakula" Beruya akamshukuru mama
"Aaah asante sana binti yangu hebu keti hapa" mama akamuelekeza kwenye kochi jirani naye huku akimuacha Li kwenye mshangao wa hilo neno "Binti yangu"
Beruya kabla ya kuketi akageuka na kumwambia Li "nashukuru sana kwa kunisaidia"
"Ahm sawa. Unaendeleaje sasa?" Li akajibu huku akibaki amesimama
"Najisikia vyema kwa sasa" akaketi huku akimwangalia Li ambaye uso wake ulikunjuka kwa kusikia hivyo
"Li hebu keti basi mwanangu, si umeshamuona Beruya au una wasiwasi gani?" Mama akamwambia na kumfanya Beruya ainame kwa kuona aibu
"Mama, naenda kujiandaa kwenda ofisini" akageuka na kuelekea chumbani lakini kabla ya kupanda ngazi sauti ya mama yake ikasikika iliyomfanya ashushe pumzi kwa nguvu
"Nimemwambia Samir unajisikia vibaya utaenda kesho"
"Mama!!!" Akageuka na macho yake yalibeba mng'ao wa kukasirika lakini hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo kwa mama yake
"Unataka nini Li, wewe na kaka yako hamjui kujipatia muda wa mapumziko, mnafanya kazi kila wakati. Kapate chakula kipo tayari"
Mama akalalamika pasipo hata kugeuza shingo kumtazama..
Li akapandisha ngazi ili akavue pajama alizovaa kwa ajili ya kulala. Akaingia kwenye chumba chake mahali alipolala Beruya huku yeye akilala kwenye chumba cha Ed. Akaingia iIi kuangalia nguo kwenye kabati lake ndipo akagundua mfuko ulioandikwa "V style & design" ukiwa pembeni karibu na mlango
:Alipoamka atakuwa alioga"
Akatafuta nguo kwenye kabati lake, alipomaliza akatoka na kuelekea chumba alichokitumia. Akabadilisha nguo na kuvaa suruali ya kawaida na shati ya mikono mifupi. Akatoka na kuelekea sebuleni ambapo alimkuta mama akiwa na Beruya wakizungumza, akaelekea jikoni kupata chakula.
Baada ya chakula akaamua kuketi kwenye baraza iliyokuwa karibu na bustani ya maua. Beruya akamfuata na akaketi kwenye kiti kilichokuwa pembeni kidogo ya alipoketi Li.
Akiwa ameshtushwa kidogo akamwangalia
Akainuka na kusimama akielekea mlangoni kisha alipofungua mlango akamuita Annie.
"Baki hapa na mgeni kwa muda mfupi" akamwacha na kuingia ndani akiwa ameshika simu yake
Akaingia jikoni akachukua kitambaa na kufunga shingoni na tumboni. Akakata mikono kisha akachukua karoti, tango na tufaa. Akamenya na akaviweka kwenye jagi la kusagia. Akasaga na kisha akachuja huku akijaza jagi dogo. Akasafisha vifaa alivyotumia wakati huo akiweka kwenye juisi ile kwenye jokofu kwa ubaridi kidogo.
Akachukua simu na kumpigia Edrian,
"Hello brother" Li akamsalimia mara alipoona sura ya kaka yake kwenye kioo cha simu yake.
"Li, uko jikoni? Salama huko?" Akauliza Edrian huku akitabasamu
"Tuko salama, naona usoni una furaha! Vipi Sidney?" Akauliza
"Tuko salama kabisa, am into business this morning" Edrian akamwambia
"Aretha?" Akauliza Li
"She is here with me." Ed akajibu