"Habari ya mchana Renatha" Ed akamsalimia Renatha huku akishika mlango kuingia ndani.
"Salama Mr Simunge" Renatha akamjibu na kugeuka kumwangalia Allan ambaye alimpa ishara ya kumfuata ofisini kwake. Renatha akamuangalia kumuonesha mshangao lakini akaamua kumfuata Allan ambaye alitangulia akielekea ofisini kwake huku akiachana na Ed ambaye alielekea ofisini kwake.
**************
"Unataka kuniambia nini Allan?" Renatha akamwambia Allan mara alipoketi ofisini kwa kwake
"Renatha, naamini hakuna jambo unataka liendelee kati yako na 'brother' Ed" Allan akamwambia huku akimtazama kwa umakini
"Kwa nini unaniuliza hivyo? Na ni nini kinakusumbua wewe?" Renatha akamuuliza Allan huku jeuri ikiwa usoni kwake
"Mmmh, Renatha najua hauko hapa kikazi ila kwa kuwa huniamini, nataka nikushauri kidogo tu, usiusogelee mzoga uliozungukwa na tai" Allan akamwambia huku akimtazama kwa makini
"Unamaanisha nini" Renatha akamuuliza huku uso wake ukibadilika kutoka kwenye jeuri na kutaka kujua kile alichomaanisha Allan.
"Nenda katafakari. Kelele za tai zinatosha kukufanya ujue mzoga huo ni mali yao." Allan akamwambia kisha akaegama kwenye kiti
"Usiniongelee mafumbo Allan, na kama unawaza nina ajenda nyingine uko sahihi ila ni kwa faida yangu" Akainuka Renatha akaelekea mlangoni lakini kabla ya kufika akageuka na kumwambia
"Una macho yanoyoona vyema. Ila kuwa makini yasije kutobolewa" Akatabasamu na kuondoka huku akiacha tabasamu lile lile usoni kwa Allan
*****************
Mida ya saa tano usiku Ed aliketi kiti cha nyuma kwenye gari ambayo dereva kwenye usukani alikuwa Linus. Aliangalia simu yake mara kadhaa kuhakikisha mambo aliyohitaji kuyafanya kwenye orodha yake yalikuwa yamekamilika. Safari ilielekea nyumbani kwao Aretha ili kumpitia tayari kuelekea safari ambayo kwa Ed ilibeba majukumu mawili, moja likiwa la kikazi zaidi, lakini huu ulikuwa ni mwanya kwake pia kumpa matembezi Aretha.
Edrian aliamua kufanya hivi, kwa kuwa mambo ambayo Aretha aliyapitia katika mfululizo wa wiki tatu yalikuwa mazito kiasi cha kuhitaji mapumziko. Na kwa upande wake aliona ingekuwa ni fursa nzuri kwa Aretha kuona maisha kwa upande mwingine.
Mara kadhaa alitabasamu mara wazo la kuwa pamoja safarini lilipogonga ķichwani mwake. "Oooh Mungu wangu kuishi pamoja kwa wiki mbil...its going to be funny" ki" Aliwaza mambo kadhaa aliyoandaa kuyafanya na Aretha watakapofika huko.
Gari ikasimama mbele ya geti la akina Aretha, Edrian akapiga simu kumjulisha kuwa wako nje wanamsubiri. Dakika chache baadae geti likafunguliwa, mama akatangulia kutoka akifuatiwa na Frans ambaye alibeba begi la Aretha.
Edrian akashuka kwenye gari pamoja na Li, naye Aretha akatokea, alivaa suruali rangi ya bluu na blauzi nyeusi yenye maua mekundu na njano, huku akivaa koti ambalo lilikuwa na sufi kwenye mikono na shingo yake. Edrian akamtazama na kutabasamu kisha akamsalimia mama, naye Li akifanya vivyo hivyo kisha akapokea begi kutoka kwa Frans na kuliweka kwenye buti ya gari.
"Mwanangu nawatakia safari njema. Usisahau tuliyoongea." Mama akamwambia Ed huku akitabasamu.
"Sawa mama nitafanya hivyo" Edrian akaitikia kisha akageuka na kumuaga Frans
"Bro nawatakia safari njema." Frans akamwambia huku akinyoosha mkono kwa Ed ambaye aliupokea kwa furaha.
Wakaelekea kwenye gari na kuketi kiti cha nyuma wakimuacha Li mbele peke yake.
"Una uhakika hujasahau kitu?" Ed akamuuliza Aretha ambaye alimjibu kuwa hujasahau.
Safari ha kuelekea uwanja wa ndege wa A- Town ilianza. Walizungumza mara kadhaa huku Aretha akimnong'oneza Ed ajue wanaelekea wapi lakini aliambiwa atajua mara wakifika uwanjani.
Baada ya mwendo wa nusu saa waliingia Ferrento International Airport, uwanja mkubwa ambao ulikuwa nje kidogo mji huu wa A. Wakaelekea upande wa pili ya uwanja. Wakiwa wanashuka kuelekea sehemu ya kusubiri simu ya Aretha ikaita, alipoangalia ilikuwa ni namba aliyoijua
"Hellow" akaitika
Upande wa pili sauti ikasikika kwa mbali ikinong'ona kiasi cha kumfanya Aretha kumuomba aongeze sauti.
"Nisaidie naomba mimi ni Beruya. Damian amenileta mahali sipajui na hataki niondoke."
Aretha akashtuka na kusimama