"Mama nashukuru sana kulipokea wazo langu. Asante pia kwa kuwaonesha ukarimu mkubwa mama na shangazi" Ed alimshukuru mama yake Aretha mara baada ya kumrudisha nyumbani..
"Aaaaah mwanangu nashukuru pia kwa kunisikiliza na kuwashirikisha maombi yangu. Kwa hiyo safari ni kesho saa ngapi?" Akauliza mama yake Aretha
Ed akamwangalia Aretha ambaye aliingia ukumbini baada ya kumaliza kuingiza mifuko ya manunuzi chumbani kwake, "Tunatakiwa kufika saa tano usiku wa kesho lakini safari itakuwa saa tisa kasorobo usiku"
"Eeeh" akashangaa mama, "kumbe mtaondoka usiku sana" kisha akamgeukia binti yake "Panga vitu vyako mapema."
Baada ya muda mchache Edrian alikuwa njiani akielekea nyumbani kwake kabla ya kupokea simu kutoka kwa wakili Bwana Ganeteu akimjulisha kuwa Bruno na rafiki zake wamepewa dhamana ya nje. Na wiki itakayofuata tarehe ya kesi itatajwa kama alivyojulishwa na Inspekta Sunday.
Alipomaliza kuongea ghafla picha ya Aretha ikamjia akilini namna alivyomkuta kwenye ile nyumba, kitu kama mshale kikachoma kwenye moyo wake. Akakunja viganja vya mikono yake kwenye usukani wa gari kwa nguvu zote hata vifundo vya vidole vikasimama kama misumari.
Wakati akitafakari hilo ghafla mbele yake gari ikaingia ambayo hakuiona kabisa kwenye kioo cha pembeni na kumsababishia kukanyaga breki kwa ghafla kitu kilichosababisha gari iliyokuwa nyuma yake kumgonga kwa nyuma. Lakini ile gari iliyoingia kwa ghafla mbele yake haikusimama. Akashusha pumzi kwa nguvu huku akishangaa ile gari ikipotea machoni pale mpaka aliposhtuliwa na mtu aliyegonga kioo chake...
Akashusha kioo na macho yake yakakutana na sura ya mwanaume ambaye alionekana kuwa na mshtuko kama aliokuwa nao...
"Uko salama?" Akamuuliza kwa hamaki
Akaitikia kwa kichwa "samahani sana ndugu yangu"
"Huna haja ya kuniomba msamaha, ile gari niliiona ikitokea kwa nyuma mara kadhaa ikijaribu kukufuatilia. Mnafahamiana?" akauliza
"Hapana, sifahamu kama ilikuwa ikinifuata" Ed akaamua kushuka kwenye gari ili kuona kama kulikuwa na uharibifu kwenye gari iliyokuwa nyuma yake.
Wakaelekea nyuma ya gari, Ed akaangalia gari ya yule bwana akaona ilipata uharibifu kwa chini upande wa kushoto. Wakaongea kabla ya kumhakikishia kuwa atafanya matengenezo kwa uharibifu ule ambao haukuwa na madhara yeyote kwenye gari yake. Yule bwana akajitambulisha kwa jina la Job kisha wakabadilishana kadi za mawasiliano.
Edrian akarejea kwenye gari na kuondoka.
**************
Jumatatu hii Ed aliingia kazini alfajiri na mapema na kumalizia kila kazi ambayo alitaka kuikamilisha kabla ya safari yake. Kila ripoti iliyotakiwa kupata uthibitisho wake aliipitia hadi aliposhtuliwa na mlio wa simu yake ya mkononi
"Hellow Captain" sauti nzito ya Ed iliitikia baada ya kupokea simu...
"Ile gari haina usajili rasmi, ila nimeifuatilia ilielekea Deluxe hotel. Wanaume wawili walishuka kwenye gari na kuingia ndani ambapo hawakutoka tena tangu walipoingia na wala hawakuandika majina yao. Ninaendelea kufuatilia na nitakujulisha mara mtu wangu atakaponipasha habari." Sauti ya Captain ilisikika akitoa maelezo
"Sawa. Nashukuru" Ed akakata simu, akainuka na kujinyoosha kisha akarudi kuketi, akamkumbuka Aretha na mambo yote yaliyoendelea alipokuwa chumbani kwake. Akatabasamu na kuchukua simu akampigia Aretha, simu ikapokelewa kwa haraka
"Mmmh ulikuwa unasubiri nikupigie eeeh" sauti ya upole ya Ed ikamwitikia Aretha mara alipopokea simu...
Akacheka "Hapana simu iko karibu nami, vipi uko salama mpenzi?" akauliza Aretha huku akiiminya ile mpenzi isisikike lakini alichelewa maana tabasamu la Edrian lilikuwa wazi usoni kwake
"Niko salama mpenzi, nimekusikia, asante" Edrian akamjibu
Wakendelea na maongezi huku akamkumbusha muda wa kuondoka na vitu vya msingi anavyopaswa kuwa navyo karibu..
Muda wa mchana Ed alikuwa na kikao na viongozi wa Idara zote ambacho kilienda vyema huku akihakikisha wiki mbili ambazo hatakuwepo kila kitu kinabaki vile vile.
Walipomaliza wakatoka kwenye ukumbi akifuatana na Allan lakini kabla hawajafika kwenye mlango wa kuingia ofisini walikutana na Renatha ambayo alionekana kutaka kuingia ofisini..