Chapter 213 - DARASA

Aretha alifurahia sana kuwepo kwa wanandoa hawa. Waliketi mezani kupata chakula ambacho Rose alikiandaa baada Edrian kumtaarifu asubuhi kuwa angekuja na mgeni.

"Mke wangu jamani hebu keti nitakuchukulia hiyo pilipili" Brian alimwambia Rose ambaye alitaka kuinuka

"Basi ninazuiwa jamani Ed hebu mwambie rafiki yako mimi si mgonjwa. Kaanzia jikoni hataki nipike" Rose akamlalamikia Ed

"Hahahah bila shaka, tutakuwa na kikao cha dharura baada ya chakula" Ed akamjibu

"Hahaha kama mna kikao chenu, nasi tutafanya chetu Aretha, sawa eeeh" Rose akamwambia Aretha, yeye akacheka

Wakashiriki chakula kwa pamoja, na Aretha alikuwa wa kwanza kukisifu chakula kuwa kitamu.

"Ila umejifunza lini Rose maana nakumbuka ulikuwa hupendi kabisa mambo ya kujibu?" Ed akamtania

"Hahaha mmesahau mmekula sana Tambi zangu nilizowapikia chuoni" Rose akajitetea

Walipomaliza kula Bri na Ed walitoa vyombo na kuelekea jikoni kuosha.

"Aretha acha wakaoshe twende zetu tukakae huku barazani" Rose akamwambia huku akiinuka baada ya Aretha kutaka kuwazuia..

Wakaelekea barazani mahali penye viti wakaketi hapo,

"Aretha" Rose akamuita

"Abeeee" akaitika Aretha

Rose akashusha pumzi, "Nimefurahi sana kukuona, imekuwa ni moja ya mambo ambayo tuliyasubiri kuyaona kwa Ed. Tulitamani kumuona Ed mwenye furaha, unajua tangu baba alipofariki ilikuwa mara chache sana kumuona katika hali hii."

Rose akauvuta mkono wa Aretha, "umemrejesha yule Ed tulikuwa nae chuoni. Asante sana Aretha. Najua kuna mambo huyafahamu kuhusu Ed, lakini nakuambia kama mwanamke mwenzangu na mdogo wangu, anakupenda kwa dhati. Tulikuwa na wasi wasi sana tangu alipotujulisha habari za Joselyn mara tu alipokuwa nae!"

"Dada Rose, samahani lakini...." Kabla Aretha hajamaliza Rose akamuwahi

"Najua hupendi nimzungumzie, samahani sana, lakini nataka ujue kuwa Joselyn tofauti yake ni kuwa alikuwa na ajenda nyuma ambayo hatukuijua lakini tulishtuka mapema. Mara tu tulipofahamu habari zako tulimuona Ed ambaye tulikuwa na muda hatujamuona. Nakuomba mpe nafasi ya kukosea na wewe pia ukubali kuwa unaweza kukosea. Mkifanya hivyo mtakuwa na mengi ya kujifunza pamoja." Rose akachukua glasi ya maji na kunywa..

Aretha akashukuru kusikia maneno yale kutoka kwa Rose...

Hahaha naomba niwe dada yako wa hiyari.. namfahamu Ed na amekuwa rafiki yetu kabla hata sijaolewa na Bri. Maisha yake yana muingiliano na biashara anazofanya. Hivyo nakushauri jitahidi kumsikiliza.....haha ila sio ukose uhuru wako"

"Sawa, nimekuelewa..." Aretha akamjibu huku akiangalia glasi ya maji!

Rose akamnong'oneza "najua bado ni kinda kwenye suala la mapenzi ila anajua kujali. Usimkimbie Aretha"

Aretha akaona aibu nakucheka huku akiitikia kwa kichwa..

"Umemchekesha nini!" sauti ya Ed akitoka iliwashtua Aretha na Rose na kuwafanya waangalie mlangoni.

"Nimemfurahisha" Rose akamjibu huku akiachia tabasamu la utani

"Retha usimsikilize huyu mwanamke wa Brian" Edrian akavuta kiti na kuketi karibu na Aretha

"Kwa nini asinisikilize na mie ndie mwalim wake!!"

"Aaaaah nitastaafu mapema, ikiwa mwalim ni wewe!" Ed akamjibu kisha akamnong'oneza sikioni Aretha

"Darasa lake sio zuri"

"Hahahahha nimesikia unamsema mke wangu" Brian akamwambia huku akimsogelea Rose na kuvuta kiti huku akiinua miguu yake

"Hebu weka hapa miguu jamani si uliambiwa unyooshe miguu"

Edrian akacheka alipoona Brian akiweka miguu ya Rose ambaye naye alikuwa akicheka huku akitikisa kichwa

"Yameanza lini haya mambo?" Ed akauliza huku akicheka

"Aretha huyu Ed atakuwa zaidi yangu nakwambia jiandae" Brian akamwambia Aretha aliyekuwa akicheka kwa vituko vilivyokuwa vikiendelea.

Wakazungumza kwa muda mchache kabla ya kuwaaga

Brian akamshika begani Aretha kabla ya kuingia kwenye gari

"Aretha naamini safari yenu itawapa nafasi ya kufahamiana vyema. Makosa yatawapa nafasi ya kufahamiana vyema. Hakika tunafurahi kuwaona pamoja."

"Asante kaka Brian. Nashukuru na nimefurahi kufahamiana nanyi" Aretha akamshukuru kabla ya kushtuliwa na honi ya gari

"Haya ingia kwenye gari maana ashanionea wivu daaah!" Brian akamuacha Aretha akiingia kwenye gari..