Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 201 - SHANGAZI MKALI

Chapter 201 - SHANGAZI MKALI

"Nadhani hatuna haja ya kufanya mjadala kwa jambo ambalo limefanyiwa maamuzi shemeji. Ninachoamini ni kuwasaidia waweze kuanza safari yao salama. Kwanza hatuendi kutoa mahari. Kuna kitu mpwa wangu anataka kufanya basi sisi tusiwe kwazo kwao. Nitaongea na Ed ninyi kaonaneni na mama wa huyo binti. Muulizeni utaratibu wao kisha tutajua wapi tuanzie." Mjomba Muzili akamaliza

Edrian akatabasamu, "Asante mjomba"

"Hahaha leo umesema 'asante mjomba' kisa huyu binti" wakacheka wote

"Twende huku tukaongee uniambie vizuri wewe na huyo mwali" mjomba akainuka wakatoka na Edrian kwenda kuketi kwenye viti vilivyowekwa kwenye bustani

"Wifi, unamfahamu vyema huyo binti, maana asije akawa anamsogelea tu kijana wetu ili ampukutishe hizo pesa zote." Shangazi Edna akamwambia mama yake Ed. Huyu ni dada aliyefuata baada ya baba yake Edrian kuzaliwa.

"Wifi, kwa mara ya kwanza nimemuona huyu binti nilihisi hivyo sababu wakati huo mwanao alikuwa na mwanamke mwingine ambaye walipishana" mama yake Ed akamwambia

"Unajuaje wifi, je kama ni huyu binti aliwafarakanisha?" Akauliza shangazi Edna

"Hapana wifi, kwa namna nilivyomuona mara ya pili na ya tatu hana akili hiyo. Ninapomuona Ed na furaha na akipambana awezevyo asimpoteze najua anampenda sana." Mama yake Ed akamweleza

"Mhhhhh haya, ngoja tujue ametoka familia gani, na yule mwanamke mwingine yuko wapi?" Akauliza shangazi.

"Ukitaka ugombane na mwanao umuulize juu ya huyo mwanamke, mimi niliacha maana ukali ule kama wa baba yake."

"Aahahah anakukaripia wewe mama yake, akijaribu kwangu ndio atajua shangazi ni baba" shangazi Edna akajitapa

"Hahahaha wifi nimekuonya mapema. Huko tunakoenda ni kwamba mama yake anataka kujua kama binti yake atakuwa salama akisafiri na mwanetu. Sasa usijaribu kupekenyua mambo. Mimi nafurahia hatua hii" mama Edrian akamtahadharisha wifi yake.

"Hahaha wifi unamuogopa mwanao nawe" shangazi Edna akamtania

"Hahahaha kama wewe ulivyokuwa ukimuogopa kaka yako eeeh." Mama yake Ed akamjibu wakaangaliana kisha wakainuka kila mmoja akielekea mwelekeo wake

*************

Aretha aliamua kuelekea chumbani kwake akiketi huko mara baada ya wageni kufika na kupokelewa na mama yake. Aliwahi kukimbilia chumbani wakati mama yake alipotoka nje. Akabaki akiwachungulia dirishani huku akimtambua mama yake Edrian. Akachukua simu yake na kumpigia Edrian, haikuchukua sekunde ilipokelewa

"Vipi mpenzi?" Edrian akauliza kwa wasi wasi

"Rian huyu ameongozana na mama ni nani? "

"Hahahahah Retha unafanya nini mpenzi mbona nasikia hadi moyo wako unavyodunda!"

"Rian" akaita kwa msisitizo

"Ni Edna, shangazi yangu. Kuna nini?" Akauliza Ed akiacha kumtania

"Aaah basi sawa. Haya baadae" Aretha akaaga na kukata simu akaketi kitandani huku akijaribu kupoteza mawazo kwa kucheza na simu yake hadi aliposikia mlango wa chumba chake ukifunguliwa.

"Wewe sasa umekuja kujificha huku binti yangu. Njoo usalimie wageni" kisha akamwacha

Aretha akiwa amevaa suruali na fulana pana akatoka kuelekea sebuleni..

"Shikamoo mama" akamsalimia mama yake Edrian kisha akamsalimia shangazi Edna.

"Marhabaa mwanangu" akaitika mama Ed

"Marhaba mwali" akaitika shangazi Edna huku akimuangalia kama mtu anayefanya ukaguzi

"Njoo ukae hapa mwanangu" mama Ed akamuita akae pembeni yake

Aretha akaelekea kukaa pale huku macho yake yakibaki kutazama zuria lililowekwa sebuleni kwao kama kwamba ni mgeni.

"Lini utakuja tena binti yangu tufanye kazi pamoja maana yule binti yangu anapenda kula nyama lakini who kuandaa"

"Aah mama nitakuja. Nitakwambia mapema" akajitahidi kujibu.

"Haya mwali tuandalie huko jikoni, tuongee na mama yako " shangazi Edna akamwambia

Mama Aretha akatabasamu "hata usijali kila kitu kiko tayari huyo muache aende akajifiche chumbani kwake tusinong'one hapa."

Mama yake Ed akaunga mkono, "Nenda binti yangu najua mnachat huko mkituteta na mwenzio"

"Hah hapana mama" Aretha akacheka na kisha akaondoka kuwapisha huku sura ya shangazi ikimtisha

"Rian shangazi ni mkali eeeh" akamtumia meseji Ed

Hakujibiwa badala yake simu iliita, akapokea

"Retha kuna kitu amefanya?" Edrian akauliza