Siku mbili zilimalizika vyema kwa Edrian japo changamoto za uchimbaji katika migodi miwili ya SGC ziliingilia utulivu wake. Pamoja na yote hayo bado aliweza kuhakikisha changamoto zinatatuliwa kwa kusafiri siku mbili kuelekea maeneo ya migodi.
Kwa upande wa Aretha, muda wake wa mapumziko haukuwa mapumziko bali aliutumia kurudia kile ambacho kilifundishwa kila siku na kufanya maswali aliyotakiwa kuyafanya. Siku hizi ambazo Edrian alisafiri, walitumia muda mrefu wakiongea kwa njia ya simu nyakati za usiku huku mara zote, Aretha alilazimisha kukata simu kumpa nafasi mwenzie aweze kupumzika japo yeye hakutaka.
Kama ambavyo Bwana Ganeteu alishauri Charlz alifungua kesi ya utekaji na udhalilishaji kwa Bruno na wengine waliokamatwa kwa kuhusika. Kesi ilisubiri kupangwa kwa tarehe.
Yassin na Derrick waliendelea kuandaa onesho la Beruya ambalo kutokana na uharibifu uliotokea kwanza ilihitaji muda wa takribani wiki mbili kukamilisha kila kitu. Damian alijaribu kumzuia Beruya kuendelea na onesho kwa kisingizio cha afya yake bado inahitaji kuimarika. Pamoja na kwamba Beruya alilazimika kurudi nyumbani kwake, lakini bado Damian alimfuata huko na jana alikuja na begi akimwambia ameona akae hapo ili ajue kama yuko salama au la! Beruya sasa alianza kuona shida kuendelea na uchoraji. Mara zote alimwambia anapoteza muda na sanaa isiyo na faida...
Joselyn alibaki ndani kama ambavyo baba yake alimwambia akikosa mawasiliano ya simu. Martinez kwa kutumia wakili aliyemfahamu aliwatembelea akina Bruno na kuwaahidi usaidizi ikiwa watakataa kuhusika kwa Joselyn kwenye suala la utekaji wa Charlz na Aretha. Inspekta Sunday aliendelea na upelelezi wake, akijulikana kwa kusimamia haki wakati wote. Bado mazingira ya kesi hii yalimpa wakati mgumu kwa kuwa alimfahamu Edrian kuwa ni mtu asiyependa kuweka mambo yake wazi na mara zote hutafuta kuyamaliza mambo yake kiakili zaidi.
***************
Hatimaye jumamosi, Edrian akiwa amerejea kutoka G-Town pamoja na Allan, mara waliposhuka kwenye ndege alfajiri hii alielekea nyumbani kwake. Aliwasiliana na mama yake ambaye alimhitaji afike nyumbani USA Estate mapema ili waweza kuongea.
Alipoingia chumbani kwake kabla ya kujiandaa kwenda bafuni simu yake ikaita, alipoangalia akatabasamu na kuketi kitanda huku kichwa akiegama kwenye ubao,
"Hellow mpenzi wangu" akapokea kwa sauti tulivu kabisa
"Rian umeshafika eeeh?" sauti ya Aretha ni wazi alikuwa na wasi wasi
"Ndio nimefika, mbona una wasi wasi wakati tumeongea masaa mawili yaliyopita eeeh!" Ed akauliza kwa mshangao
"Aaaah ni wasi wasi sababu uko safarini" Aretha akajibu kwa furaha
"Ulidhani ndege ingeanguka haaaa?" Edrian akamtania
"Acha kusema hivyo Rian" akalalamika
"Ooooh sorry princess. Niko salama. Kwa hiyo haujalala tangu muda ule?" Akauliza
Edrian huku tabasamu lake likiwa wazi
"Eeeeeh ila nitalala sasa"
"Mpenzi wangu kumbe unanipenda hivyo na kuniwazia" Edrian akasema kama mtu aimbae
"Rian hahaha acha kuimba huwezi" sauti ya Aretha akicheka ikamfanya Ed aache
"Hahahaha sijui kuimba ila najua kukupenda"akamtania
Aretha akacheka na wakaendelea na maongezi huku wakikumbushana kuhusu ugeni ambao ungeenda leo nyumbani kwao.
"Rian kwani lazima mama aje!" Akauliza Aretha
"Hahahaha najua unajaribu kunishawishi asije. Mimi nitahakikisha anakuja leo. Najua akija lazima nisafiri na mke wangu mtarajiwa" Edrian akamwambia huku akicheka
Baada ya maongezi kuendelea wakashtuka ikiwa imefika saa mbili asubuhi. Wakaagana, Edrian akaamua kupumzika kwa saa moja kabla ya kujiandaa kuelekea kwa mama yake.
****************
"Mama, wewe unajua haya ni maamuzi ambayo siwezi kuyabadili. Kuamua kuishi na Aretha ni jambo nililihisi mara nilipomshika mkono kwa mara ya kwanza."
Edrian akamwambia mama yake kisha akarudisha macho kwa mjomba na shangazi yake
"Ninyi mnajua sitarudi nyuma ninapoamua jambo. Nawahakikishia Aretha ni mwanamke sahihi kwangu."
"Ed, sisi hatupingani nawe, ila tunaona kama imekuwa haraka sana ikiwa hamna hata miezi mitatu" shangazi Edna akamwambia huku akirudisha macho kwa mjomba aseme kitu lakini akaachia tabasamu