Derrick alikutana na Yassin kwa safari ya kumuona Beruya, wakitumia pikipiki la Derrick walifika kwenye nyumba anayoishi. Waliamua kwenda kumuona baada ya simu yake kutopokelewa kabisa au kupokelewa na mchumba wake akiwaambia Beruya amepumzika.
Baada ya kugonga kwa muda mrefu akatoka mtu ambaye walimfahamu sura yake. Damian mchumba wa Beruya.
Kwa namna alivyofungua mlango, ilionesha wazi kuwa hawakukaribishwa kuingia ndani. Maana Damian alitoka kisha akaurudisha mlango na kusimama nje. Alivaa fulana ya kijani na kaptula fupi ikionesha hakuwa na ratiba ya kazi
"Habari yako Dokta" Yassin akamsalimia lakini Derrick aliposikia sauti ya salamu hii ilikuwa wazi kwake kuwa hawa wawili zilikuwa haziivi chungu kimoja.
"Unataka nini hapa?" Damian akauliza huku akiendelea kusimama na mikono akiikunja kifuani.
Derrick akaona aingilie kati, "samahani Dokta, tuko hapa kwa kuwa tuna nia ya kuzungumza na Beruya"
"Hayupo" akajibu kisha akaangalia dirishani
"Bbbb" Yassin akaita kwa sauti kiasi cha kuwashtua Derrick na Damian
"Nilikukataza usije hapa lak___" lakini kabla ya Damian kumaliza sentensi yake tayari Yassin akamuita tena "Beruyaaa"
"Hayupo naomba muondoke" Damian akajibu sasa
"Yuko wap_" Derrick hakumaliza kuzungumza mlango ukafunguliwa, Beruya akatoka akiwa amevaa gauni ambalo juu yake kulikuwa na kitambaa kilichofungwa vyema kuonesha alikuwa jikoni.
"Yassin" Beruya akamuita Yassin kisha akageuka na kumuona Derrick, "Habari D" akamsalimia
"B mbona simu hupokei?" Yassin akauliza huku akishindwa kuficha wasi wasi aliokuwa nao juu yake
"Sipokei, simu yangu ilipotea tangu siku ile na hapa nasubiri niweze kukabili uharibifu ule nitatafuta simu mpya"
Yassin akamuangalia Damian huku Derrick naye akimshangaa Beruya,
"Ber tafadhali twende ndani ukae_" kabla Damian hajamaliza Beruya akamuwahi
"Hapana Dami inawezekana tukaongea na Yassin kujua kosa langu hasa ni nini hata akatae kufanya kazi nami" Beruya akamshika mkono Damian ambaye alitaka kumrudisha ndani
Yassin macho yalimtoka akishangaa maneno aliyosikia kwa Beruya,
"B, unamaanisha nini kusema mimi nimekataa ku__" Damian akamkatisha na kumshika tena mkono Beruya
"Ber mimi ni daktari nadhani mazungumzo haya hayafai kwa__"
"Damian shut up" Yassin akamkaripia
"Wewe ni nani hata unifokee nyumbani kwangu mwenyewe" Damian akapiga hatua kumsogelea Yassin ambaye naye akimsogelea kabla ya Derrick kuingilia kati
Beruya alibaki kwenye mshangao kwa sekunde kadhaa hadi Damian alipomshika begani "Twende ndani". Beruya akageuka ili kuondoka lakini alichosema Yassin kikamfanya asimame
:B, tunakuandalia onesho lako tena na sasa anayelilipia sio wewe"
Akageuka ili kumsikiliza, lakini mkono wa Damian ukamkaba kwa nguvu waingie ndani. Machozi yalionekana wazi kwenye macho ya Beruya, "Niache Dami unaniumiza"
Derrick ambaye alinyamaza kwa muda akamwambia "Dokta nadhani huna haja ya kufanya haya mambo yaende kwenye mkono wa sheria. Tutaongea na Beruya ikiwa atakubali kutusikiliza na akikataa tutaondoka. Usitumie nguvu kumzuia"
Damian akageuka amwangalie Derrick, akataka kusema kitu akanyamaza akarudisha macho kwa Beruya ambaye aliutoa mkono wake kwenye kiganja chake kiliçhokuwa kimemshika kwa nguvu. Akawaelekea kina Yassin.
************
Hellow Ivan" Edrian akaongea huku akizungusha kalamu mkononi mwake
"Mr Simunge, Habari yako?" Dokta Ivan akamsalimia
"Mimi ni salama kabisa. Samahani sana kukupigia masaa haya" Edrian akaongea
"Bila shaka rafiki yangu. Nikusaidie nini leo maana tangu juzi unatutembelea sana hahaha"
"Hahahaha acha tu rafiki yangu. Naomba nipate taarifa za daktari wako hapo"
"Hahaha hapo unaniingilia miiko ya kazi rafiki yangu, daktari yupi huyo, Brianna! Ila huyo atakwambia mwenyewe"
"Hahaha hapana. Nahitaji tu ufahamu wa awali wa Dokta Damian" Edrian akamfahamisha
Dokta Ivan akakaa kimya kwa sekunde tano kisha akaendelea "Damian hapa tunao wawili sasa ni yupi?"
"Hapo sijapewa jina lake ila nikutajie muonekano wake" Edrian akamtajia muonekano, alipomaliza
"Dokta Damian Bernard, unataka kujua nini hasa?"
"Historia yake tu rafiki yangu"