Alipomaliza kuongea na Dokta Ivan, Edrian akarudi kuitazama ile picha ya video, huku akiunganisha maelezo aliyopewa na kile alichokiona kwenye picha,
"Huyu ni mtu hatari kama anaweza kumfanyia hivi mtu anayempenda, hakika atakuwa na shida kidogo ya akili"
Kwenye video ile alionekana Damian akiwa anaingia kwenye jengo la Southern Pole. Akashuka kwenye gari na kuelekea ndani, baada ya muda mfupi akatoka akiwa amemshika Beruya ambaye alionekana kuchoka akampeleka hadi kwenye gari yake. Cha kushangaza alipomfikisha akamweka vizuri, kisha akachukua mfuko kwenye buti ya gari akarudi tena ukumbini.
Ilipita dakika kumi bado Damian hakuwa amerejea. Mara akarudi kwa haraka akaingia kwenye gari huku ule mfuko akiutupia kiti cha nyuma. Akaondoka eneo la ukumbi.
Edrian alipomaliza kuangalia akashusha pumzi na kuegama kwenye kiti. Akampigia Derrick ambaye alipokea na kumuomba ampe dakika chache atamtafuta kwani walikuwa na mazungumzo na Beruya
Edrian aliposikia hivyo akashukuru na kisha akarudisha simu lakini kabla ya kutulia meseji ikaingia
"Una nafasi tuongee Rian" ilitoka kwa Aretha
Edrian akatabasamu, akakumbuka tangu walipoongea asubuhi hakuwa amemtafuta tena. Akafurahi kuona Aretha anataka kuongea nae. Akampigia kisha akaacha mazungumzo yao yawe wazi
"Princess, umenikumbuka eeeh" Edrian akamwambia huku akiegama kwenye kiti
"Rian, Habari ya mchana!" Aretha akamsalimia shauku ikiwa wazi kwenye sauti yake.
"Salama mpenzi, umepumzika eeeh?" Edrian akauliza akiwa amejituliza kwenye kiti
"Nimepumzika, lakini nimechoka kukaa tu Rian" Aretha akalalamika
Edrian akashtuka "unahisi kuchoka tu au unajisikia vibaya Retha?"
Aretha alipohisi wasiwasi wa Ed akawahi kumjibu "Ah niko sawa ila nachoka kukaa nyumbani tu"
"Aaaaah leo hauna picha ya kuchora" akauliza Edrian baada ya kushusha pumzi
"Ninataka kuchora ila sijui nichore nini, Rian?" Akamuita
"Mmm" Edrian akaitika huku akitafakari kitu
"Tunaongea ukiwa unafanya nini? Isije ikawa ni_"
"No. Nina nafasi ya kuongea nawe. Umekula lakini?"Edrian akamkatisha huku akitabasamu
"Ndio nimeshakula"
Edrian akafumba macho kuonesha kukata tamaa ya kile alitaka kukifanya, lakini papo hapo akatabasamu kisha akaendelea "Retha, unakumbuka ulipapenda sana huku juu ya jengo letu!"
"Ndio nakumbuka, kule juu ni pazuri sana" sauti ya Aretha ilidhihirisha furaha kwenye kumbukumbu ile
"Unaonaje ukija ukatulia huko juu naamini wazo litakuja" Edrian kwa sauti yakujali akamshawishi Aretha
"Rian, uko kazini sio vizuri nikufanye uache ratiba yako" Aretha akamjibu kwa kujali sana
"Sawa Retha basi sitakuja kukaa nawe lakini nitakuwa ofisini hadi muda wa kutoka" Edrian akajitetea
Kimya kifupi cha sekunde kikapita, huku Edrian akimpa nafasi Aretha aamue mwenyewe
"Sawa, nitakuja Rian" Aretha akajibu huku shauku ikiwa dhahiri kwenye sauti yake..
"Mmmhhhh" akashusha pumzi kwa furaha baada ya kusikia jibu la Aretha kisha akaaendelea
"Ukija tutafanya ile kazi ya kujaza fomu ya uhamiaji, beba vielelezo vyote mpenzi"
"Aaaah Sawa. Ila mama hajaniruhusu kasema anaendelea kutafakari atanipa jibu. Kwani safari ni lini?" Akauliza Aretha
"Jumatatu" Edrian akamjibu
"Haaaaa una hakika ni sawa kufanya hayo yote?"
Edrian akacheka "Retha hilo niachie mimi. Jiandae namuagiza mtu akuchukue"
"Nooo.. usifanye hivyo nitakuja mwenyewe" Aretha akahamaki
"Hahaha hutaki nije Retha" akamtania
"Rian baadae najiandaa." Aretha akamuaga na akakata simu
Edrian akacheka "nimempigia mwenyewe lakini amekata simu kabla sijamaliza. Ananifurahisha"
Akabofya kwenye simu yake ya mezani na sauti ya Loy ikasikika "Hello boss"
"Naomba uandae mtu afanye usafi kule juu" akatoa maagizo
"Jana walifanya usafi bosi" Loy akajibu
"Mmmmm" Edrian akaguna
"Sawa bosi nitamuagiza sasa hivi" Loy akajibu kwa adabu
"Ukimaliza kuna ujumbe nakutumia kwenye simu yako. Kanunue hivyo vitu ukaviweke huko juu." Edrian akakata simu kisha akachukua simu yake ya mkononi akaingia kwenye ujumbe akaagiza biskuti aina tatu tofauti, juisi boksi mbili na matunda tofauti. Akamtumia Loy. Akaendelea na kazi lakini akiwa na shauku kubwa