Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 185 - NAWEZAJE KUKUSAIDIA

Chapter 185 - NAWEZAJE KUKUSAIDIA

Njiani aliendesha gari akimtazama Charlz kwenye kioo, kichwani alitamani kutaka kujua imekuwaje. Picha ya ile damu ilipogonga kwenye fikra zake mwendo wa gari uliongezeka. Alipofika mahali kwenye taa za barabarani kwa mchana ule Edrian alipita pasipo kusubiri taa zilizomruhusu yeye kupita.

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwake kufanya hivi ukiacha ile ambayo alifanya mara alipotoka hospitali akiwa amethibitishiwa na daktari kuwa baba yake hakuwa hai tena. Na wakati ule alipewa adhabu ya kutoendesha gari kwa miezi mitatu. Sasa leo alifanya hivyo tena na tayari akiwa na tiketi mbili za makosa. Hakujali.

Alipoingia City hospitali hakuingia chumba cha dharura (ER) aliendesha mpaka nyuma ya jengo ambalo lilikuwa na ofisi ya Dr Brianna. Alipofika tayari Dr Brianna alikuwa na madaktari wanne wamesimama wakimsubiri.

Alipoegesha gari, hakushuka akafungua vitasa vya milango ya gari na kisha akashusha pumzi na kuegemea kwenye usukani. Dr Brianna akafungua mlango na wale madaktari wakafanya kazi ya kuwachukua Aretha na Charlz. Walipomaliza kuwatoa wakaelekea ndani huku wakimuacha Dr Brianna nyuma.

Dokta akafunga mlango na kuelekea mahali mlango wa Edrian akauvuta

"Ninawezaje kukusaidia" akauliza Dr Brianna akimgusa Ed begani

Alipoinua uso Dokta akafumba macho na kumeza mate kisha akatabasamu

"Unahitaji matibabu haraka rafiki yangu"

Akamvuta kidogo ili ashuke kwenye gari ambapo Edrian alifanya hivyo huku Dokta Brianna akizima gari na kisha akachomoa funguo na kurudishia mlango. Macho ya Ed yalikuwa mekundu huku mishipa ikionekana wazi usoni.

Wakapiga hatua huku Dokta Brianna akiwa amemshika mkono. Wakaingia kwenye lifti na moja kwa moja wakelekea ghorofa ya nne. Wakaingia ofisini kwa dokta, Edrian akaelekea kwenye kitanda kilichokuwa pembeni ya meza ya daktari akafungua vifungo vya shati na kifua chake kikawa wazi. Akapanda na kulala chali, huku Dokta Brianna akachukua kidonge kwenye droo iliyokuwa pembeni na maji akamsogelea. Edrian akakichukua kidonge kile na maji akanywa.

"Tulia Edrian halafu nitarudi kujua nini kinaendelea, kwa sasa naenda kumuona Aretha." Akatoka na kumuacha Edrian mle ndani, akafumba macho.

Baada ya nusu saa Dokta Brianna akarudi, Ed alikuwa sasa ameketi kwenye kiti kilichoangaliana na kile cha dokta. Alikuwa amepiga simu kadhaa na kuongea na Derrick. Lakini hasa aliwasiliana na 4D na kuhakikisha wanamsaidia kumpata yule aliyefanya kitendo kile. Bado aliingia kwenye duka la mtandaoni la Victoria akawa akichagua nguo na kisha akaziagiza

"Uko sawa sasa rafiki yangu unaweza kuniambia eeeh?" Dokta Brianna akamwambia mara tu alipoketi

"Unanifahamu vyema Brianna" akajibu Ed akijaribu kutabasamu ambapo Dokta naye alitabasamu, akaendelea

"Kabla sijakusimulia nataka nijue kwa nini Aretha anatokwa na damu?"

Dokta Brianna akaitikia, akainua simu iliyokuwa pembeni yake "Dr can you please check why she is bleeding and let me know?"

Akarudisha simu na kumwangalia Edrian ambaye alianza kumsimulia kila kitu. Mara kadhaa machozi yalionekana machoni pa Ed lakini akafanya kila awezalo kuyazuia.

Kama kuna watu wanajua kusikiliza basi Dr Brianna ni mmoja kati yao. Hakumkatisha hata mara moja na tena alipohitaji kushusha pumzi alimpa nafasi.

Simu ikaita naye Dokta akapokea na hakuongea sana zaidi ya kukubali kile alichoambiwa. Akamwangalia Ed

"Ni damu ya mzunguko wake wa kawaida. Mwili wake umepitia mambo yakushtua kwa siku hizi chache ndio maana amepata muingiliano ghafla" dokta Brianna akamwambia

"Mhhhhh, Brianna Tafadhali ukachunguze chochote ki___"

"Nakuelewa sana Edrian. Relax. Nitakujulisha. Kwa sasa anaweza kuamka muda wowote itakuwa vyema ukakae nae"

Edrian akainuka akamshukuru Dokta Brianna,

"Utanipeleka au ninaweza kwenda mwenyewe?" Akauliza Ed alipofika mlangoni.

"Hahaha, usijali yuko chumba kile kile alicholala jana. Na Charlz yuko ghorofa inayofuata. Derrick yuko nae na marafiki wengine"

"Asante Brianna."

Akatoka ofisini kwa dokta na kuelekea kilipo chumba alicholazwa Aretha.

******

Alipomuona Aretha akikimbia chooni akatabasamu na kurudisha macho yake kwenye simu.

"I love her"