Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 181 - SORRY PRINCESS

Chapter 181 - SORRY PRINCESS

"Polisi tayari wamefika, wanataka kuzungumza na Aretha. Kwa sasa wanamalizia kuchukua maelezo ya Charlz" Dokta Brianna akamwambia Edrian

"Ni sawa. Na...vipi aaah kuhusu n_" dokta Brianna akaamua kumketisha baada ya kumuona Edrian akipatwa na kigugumizi kuuliza swali lile

"Edrian, She is okay. Hakuna chochote kilichofanyika kwenye mwili wake"

Akafumba macho kisha akafumbua, uso wake walau ulionesha mwanga baada ya maneno haya kutoka kwa dokta Brianna.

"Sawa, wajulishe tunawasubiri kabla hatujaondoka hapa" Ed akamwambia dokta

"Kabla hawajafika jaribu kumwelezea taratibu nini kilitokea kwa upande wako" dokta akamwambia huku akipiga hatua kuelekea upande wa pili wa wodi ambako Charlz alilazwa.

Edrian akafungua mlango na kuingia ndani, akamkuta Aretha akiwa ameketi pembezoni mwa kitanda huku kichwa chake kikiegemea meza iliyokuwa pale.

Aliposikia mlango ukifunguka akainua macho yake na kumuangalia aliyeingia, macho yao yalipogongana hakuna aliyesema neno lakini mengi yalizungumzwa tayari.

Edrian akavuta kiti na kuketi mbele ya Aretha akashika mikono yake kisha akamwambia

"Naomba usiwaze sana Retha, hebu nielezee nini kilitokea kabla ya kupoteza fahamu" macho ya Edrian yalimtazama kwa upendo mwingi hata Aretha akahisi utulivu mkubwa na amani

Akaanza kumsimulia mara walipofika darasani nini kiliendelea na namna Charlz alivyojaribu kumnusuru na fujo za Bruno. Alipomwambia kuhusu mtu aliyemshika puani na kitambaa, Edrian akasimama ghafla akamvuta Aretha na kumkumbatia..

"Am so sorry princess" Edrian akamwambia huku akijaribu kuutuliza moyo wake binafsi kwa maumivu ambayo yaliongezeka aliposikia maelezo ya Aretha

Aretha alitulia mikononi mwa Edrian, akihisi faraja kubwa. Baada ya sekunde kadhaa, Edrian akamuachia Aretha kisha akakaa pembeni yake akikilaza kichwa chake kifuani.

"Rian nini kilitokea hata nikaletwa hospitali?" Aretha akauliza kwa sauti ya chini

Edrian akashusha pumzi ndefu na akafumba macho kisha akayafumbua na kuanza kumsimulia,

"Nilijaribu mara kadhaa kuipiga simu yako lakini haikupokelewa, nikapiga kwa mama akaniambia umeenda chuo. Nikamtafuta Charlz kujua kama kuna shida yoyote lakini naye simu yake iliiita bila kupokelewa. Nikaomba msaada wa mtu mmoja aweze kuiangalia namba yako mahali ulipo. Wakati huo nilikuwa tayari njiani kuja huko chuoni. Nikamjulisha Derrick amtafute Charlz.

Nilipofika eneo ambalo simu yako ilisoma nikakukuta kwenye hiyo nyumba wewe pamoja na Charlz" akajaribu kuyakwepa macho ya Aretha akaangalia pembeni huku akikunja viganja vya mikono yake kwa nguvu

"Halafu ikawaje?" Aretha akauliza taratibu huku akikumbatia viganja vya Ed kwa vile vya kwake

"Mmgh" akakohoa kidogo kisha akaendelea

"Nilipoingia ndani sikukuona lakini nilimkuta dada mwingine amefungwa kwenye stoo ya nyumba ile. Jana usiku nilipigiwa na namba ambayo sikuwa naifahamu nikasikia sauti ya dada ambaye alikuwa akilia akiomba msaada wangu. Nilipomkuta yule dada pale stoo nilishtuka baada ya kugundua ni sauti ile ile niliyoisikia jana. Nikaendelea kukutafuta hadi nilipoona simu yako kwenye sebule na gari pamoja na simu ya Charlz. Wakati huo Derrick alikuja kuungana nami kuwatafuta. Ndipo nilipoona mlango mwingine." Akashusha pumzi kisha akataka kuinuka lakini mikono ya Aretha ikambana kwa chini abaki huku macho yake yakimwangalia kutaka kujua kilichotokea

Wakati wakitazamana mlango ukagongwa, Ed akamwangalia Aretha kisha akamwambia

"Polisi wamekuja kuchukua maelezo yake. Usiogope Retha, waambie kile ambacho unaniambia." Akamkumbatia na kumbusu kwenye paji la uso kisha akainuka

Mlango ukagongwa tena mara ya pili, Edrian akaufungua. Wakaingia polisi wawili wakiume wakiwa wamevalia mavazi nadhifu ya Jeshi la Polisi

"Inspekta karibu" Edrian akawakaribisha mara baada ya kumwangalia begani kwake yule aliyetangulia

Wale polisi wakamsalimia Edrian na kisha wakamuangalia Aretha ambaye aliketi kitandani.

"Aretha Thomas?" Akauliza Inspekta huku akipiga hatua kuelekea kilipo kitanda ambacho aliketi Aretha ambaye alimuitikia kwa kichwa.

"Unaendeleaje kwa sasa?" Akauliza huku akiketi kwenye kiti