Wakati Aretha akijiweka vyema kwemye maliwato ya ofisini kwake, Edrian akasogea ilipo kompyuta yake, akaketi kwenye kiti na kuandika mambo kadhaa kisha akatuma. Akachukua simu akatafuta namba ya Tobby na kumpigia. Lakini kabla ya simu kuunganishwa Aretha akaingia akiwa amejiweka vyema...
"Hellow Bro" Edrian akaita wakati macho yake yakikaza kumuangalia Aretha ambaye kwa aibu akataka kuelekea kwenye kochi ili akae lakini akampa ishara aende kukaa kwenye kiti kilichotazamana nae.
Aretha akafanya kama alivyomwambia huku akitabasamu akaketi na kuanza kucheza na vidole vyake..
"Kwa hiyo hakuna dalili za mtu kutoka nje?" Akauliza Ed baada ya muda kupita akimsikiliza Tobby upande wa pili.
"Basi sawa. Asante sana bro" alipomaliza akakata na simu huku akiendelea kumtazama Aretha aliyekuwa akilamba midomo yake huku macho yake yakitazama nje kupitia dirisha lililokuwa pembeni ya meza ya Edrian.
"Retha, tutaenda kwa mama kisha tutaenda kuonana na Yassin na Derrick, samahani kwa hii ratiba_"
"Hapana shida Rian nimekupa ratiba yangu leo" Aretha akasema huku akitabasamu
"Ratiba yote Retha?" Ed akauliza huku akiinua nyusi zake kisha akaegama kwenye kiti akizungusha kalamu mkononi mwake
"Ndio, una mashaka?" Aretha akajibu akijaribu kujionesha kumzoea Ed
"Uuhhhm kwa kusema hivyo tukimaliza na Yassin tutaelekea kwangu."
"Aah!" Aretha akashtuka
"Ndio maana ya kunipa ratiba yako Retha. Ratiba yangu baada ya hapo ni kwenda nyumbani!" Edrian akamtania tena kwa msisitizo
"Laki__" akataka kujitetea
"Hakuna lakini Retha, umesema na_" simu yake ya mezani ikamkatisha
"Yes Loy" sauti ya kukerwa ya Ed iliitika na kumfanya Aretha kutabasamu
"Bosi, kuna chochote unahitaji muda wa kutoka umekaribia"
Edrian akashtuka, akaangalia saa akatabasamu maana hakuelewa muda uliendaje endaje haraka "ooooh.. no Loy. Sina nachohitaji. Andaa ratiba ya kesho vizuri kuna mabadiliko nakutumia kwa barua pepe naweza kuchelewa" akamalizia kwa kumwangalia Aretha ambaye alishtuka kusikia atachelewa
Mapigo ya moyo ya Aretha yakaongezeka, "Hivi anamaanisha kweli sitaenda nyumbani?" Akawaza Aretha
Vidole vilivyogongwa usoni kwa Aretha vilimshtua kutoka kwenye mawazo
"Unaogopa kumalizia ratiba uliyonipa?" Akauliza Ed nusu ya mdomo wake ukitabasamu
"Ha..hapana hapana Rian...nitakwenda" Aretha akamalizia maneno yake kwa sauti ya chini
Edrian akacheka taratibu na kisha akazima kompyuta yake "Hahahahha najua unajaribu kuwa jasiri lakini usiwaze maana nitafuata ratiba yako nitakapomaliza yangu." Akakusanya vitu vyake vilivyotakiwa kuingia kwenye begi lake na wakati akifanya hivyo Aretha akainuka kutoa zile glasi kwa aibu ya kuona Edrian amejua alikuwa akiwaza nini
Alipohakikisha kila kitu kimekaa sawa, Ed akamshika mkono Aretha ili watoke baada ya kumuona anabeba mkoba wake, lakini akasikia kuvutwa kurudi nyuma akageuka
"Rian..aaa. .m..mikono, nafikiri si_"
"Ssshhh" akamwekea kidole mdomoni asiendelee kisha akainama na kumwambia sikioni
"Nafurahi nikitembea nimekushika, inakusumbua?"
"Aah..no aah hapana Rian ni__"
"Basi usiwaze kingine zaidi ya furaha yangu kutembea nimeshika mkono wako" Ed akamwambia na kuendelea hadi alipofungua mlango
Bado Loy alikuwepo akimalizia kazi aliyopewa, Edrian alikuwa na uhakika Allan alikuwepo muda ule ofisini, lakini hakutaka kumshtua, kumbe hakujua masikio yake yaliegemea mlango na mara sauti ya mlango wa ofisi yake ukifunguliwa ikasikika.
Edrian na Aretha wakageuka kwa pamoja na kukutana na macho ya Allan ambayo yaliganda kwenye mikono iliyoshikana..
"Allan, unamkumbuka Aretha? " Ed akamuuliza huku mkono wake ukimvuta karibu Aretha
"Oooh namkumbuka bro. Habari yako Aretha" Allan akapiga hatua kumsogelea Aretha huku mkono wake ukiwa umenyooshwa,
Aretha akanyoosha mkono wa kuume ambao ulikuwa huru akamsalimia Allan, "salama Allan"
Bado Ed hakuachia mkono wa kushoto aliomshika Aretha, "Kuna maelekezo nimempa Loy atayatuma kwako. Natoka"
"Sawa bro, Aretha karibu sana" Allan akaonesha ukarimu kwa Aretha ambaye alishukuru. Wakatoka wakiwaacha Loy na Allan wakiwaangalia, mshangao ukiwa wazi usoni.