Baada ya kumaliza kikao cha alasiri, Edrian alirudi ofisini kwake, akasimama pembeni ya meza yake akajinyoosha mwili wake kabla ya kuketi kwenye kiti chake. Akaangalia simu yake, alitamani akutane na ujumbe kutoka kwa Aretha lakini la! Akabofya namba ya Aretha lakini kabla ya simu kuunganishwa akakata,
"Aaaaarhg!!, niliahidi kumuacha apumzike. I should be patient" akaweka simu pembeni na kuchukua nakala aliyopokea kutoka kwa Renatha na kuanza kuisoma huku akiandika maoni yake pale alipoona panafaa.
Dakika chache baadae alishtuliwa na simu ya Loy ambaye alimjulisha kuwa ana mgeni.
"Mruhusu aingie na tafadhali nitakuwa 'busy', clear my timetable please!"
Sekunde tano zilizofuata Edrian alisimama ofisini huku akitabasamu, akapiga hatua kwenda mlangoni kwa furaha akisubiri kuingia kwa mgeni huyo. Mlango ukafunguliwa taratibu
"Retha, what a suprise!" Edrian akasema mara alipomuona Aretha akiingia ofisini kwake!
Aretha alisimama akimwangalia Edrian ambaye hakuweza kuificha furaha yake,
"Rian samah___"
Kabla ya kumaliza maneno yake, Edrian akamkumbatia huku akisema maneno ya kumshukuru kwa kuja kwake..
"Rian tuko ofisini" akaongelea kifuani kwa Ed
"Ni ofisi yangu Retha na wewe ni mgeni wangu" akajibu huku akitabasamu kidevu chake kikiegemea kichwa cha Aretha..
"Oooh so sweet to have you here" akasema moyoni mwake kisha akamwachia Aretha. Akamshika mkono hadi kwenye kochi la watu wawili lililokuwa ofisini kwake. Akamketisha halafu akaelekea lilipo jokofu, akatoa boksi la juisi ya matunda, akachukua glasi mbili na kumimina.
Akarudi akiwa ameshika glasi mbili za kiosk mkononi mwake, akaweka moja mezani na nyingine akamkabidhi Aretha..
"Karibu princess"
"Asante" akapokea Aretha
Kimya cha sekunde kadhaa kikapita kati yao, shauku ya Edrian kujua sababu ya ujio wa Aretha ilizidi ndani yake. Alipofungua kinywa chake ili aanze kwa swali, Aretha naye akaanza kusema na wote wakagongana
"Haha tafadhali endelea princess" Edrian akampa nafasi Aretha ya kuzungumza
"Asante Rian" Aretha akashukuru kisha akachukua glasi ya juisi akanywa kidogo akageuka upande ili aongee akimtazama usoni Ed, kitendo ambacho kilimfanya Edrian ashangae ndani ya moyo wake. Namna alivyogeuka Aretha alionesha ujasiri na kujiamini tofauti na mara kadhaa ambazo Ed alipata kuwa karibu naye.
"Rian, samahani kwa kuja pasipo kukutaarifu, nimehitaji kukuona kwa sababu kuna mambo nahitaji maongozi yako ya karibu." Aretha akatoa simu kwenye pochi ndogo aliyobeba akagusa kioo chake na kisha akamkabidhi Edrian
"Naomba usome meseji kwenye simu zimetoka kwa Beruya, japokuwa nahisi sio yeye aliyeandika."
Edrian akapokea simu, akamwangalia Aretha machoni kisha akarudi kuangalia meseji kama alivyoelekezwa. Akapandisha juu na kusoma akashangaa kwa nini Beruya alimlaumu Aretha kwa jambo ambalo hakuna ambaye aliyetarajia. Akamuangalia tena Aretha usoni kuona dalili za huzuni lakini alikutana na tabasamu
"Rian, nimekuja hapa nina mambo mawili naomba unisaidie"
"Retha mpenzi, nakusikiliza" Edrian akamuitikia halafu akaweka simu mezani kisha akaushika mkono wa Aretha
Aretha akaangalia mikono ya Ed iliyompa faraja,
"Rian, naomba unisaidie kujua nani chanzo cha tukio lile lililoharibu onesho la Beruya" akamwangalia Edrian ambaye alimuitikia kwa kutikisa kichwa
"Aaahm na jambo la pili...aah_" akasita kidogo akainua macho yake yakakutana na yale ya Ed yaliyompa uhakika
"Niambie jambo la pili" Edrian akamsihi
"Naomba niandae onesho kama lile kwa gharama zangu lakini maalum kwa ajili ya Beruya."
Aretha hakujua maneno yake yalichofanya kwa Edrian, alisikia raha kuwa amepewa nafasi ya kuchunguza suala lile kutoa mrejesho. Edrian akamvuta Aretha na kumkumbatia kwa furaha
"Nakuhakikishia Retha nitamjua aliyehusika bila shaka. Asante sana mpenzi"
Akamwachia Aretha, akamuangalia "Retha, umenifurahisha sana kuja ofisini, lakini nini kimetokea kwa ghafla ukataka kuniona?"
Aretha akalamba midomo yake na kisha akainua macho kumwangalia Edrian
"Nataka kuwa jasiri. Najua mambo mengi siyafahamu lakini natamani kupambana pamoja nawe sababu nakupenda mno"