**********
"Wewe ni nani mwanangu?" Akamuuliza huku kiganja cha mkono wake kikigusa shavu la Aretha kwa kumjali
Aretha akatafakari swali lile alilomuuliza mama yake. Aljaribu kujitathmini lakini kitu pekee alichokiona ni kujikatia tamaa, "kwa nini niwe hivi, sikuweza kumpata baba, na sasa naelekea kumpoteza Rian kama nitakata tamaa tena"
Mama yake aliendelea kumpa nafasi Aretha aweze kujitafakari, "kitu chema unapokipata unatumia uwezo wako wote kuhakikisha hakuna wakukipokonya mkononi mwako" akamwambia
"Yule kijana anakupenda binti yangu, mazingira yanaweza yasiwe laini kwako lakini unaweza kupambana nayo yasikunyang'anye kitu cha thamani ulichokipata. Haya yote ni_" kabla ya kumaliza, Aretha akainuka na kumuita
"Mama"
Mama akamwangalia kwa mshangao
"Mama ninataka kumuona Rian"
"Eeeeeh! Sasa hivi? Kwa nini?" Mama alijikuta akiuliza maswali mfululizo
"Mama, ninafikiri kuondokana na hizi lawama, nitatumia kiasi cha fedha kwenye akaunti aliyonifungulia Rian, nitaandaa onesho kama lile kwa ajili ya Beruya" Aretha akasema kwa matumaini huku akisimama mbele ya kioo cha kabati lake.
"Retha hebu kula kwanza kabla ya hiyo ratiba" mama akamsihi ale baada ya kuona msimamo ukibadilika ghafla kwa binti yake
"Nitakula mama, nahitaji niongee na Derrick mara moja kwanza kabla sijaelekea ofisini kwa Rian" akachukua simu yake na kumpigia Derrick
Mama akabaki akimuangalia Aretha aliyekuwa akiongea na simu sasa, "Mungu hata sijui nimeongea nini na ameelewa nini huyu binti." Akainuka taratibu na kuweka kitanda cha Aretha vizuri huku akisikiliza binti yake akimshawishi Derrick kuandaa onesho, lakini liwe maalum kwa ajili ya Beruya.
Alipomaliza kuongea na Derrick, Aretha akaketi kula chakula huku mama yake akiketi pembeni yake akimtafakari binti yake.
Alipomaliza kula, Aretha akatoa vyombo na kuvipelekea jikoni, akarudi haraka na kuingia kabatini kwake akitafuta nguo.
"Mama naenda kumuona Rian ofisini kwake kisha nataka kufuatilia hali ya Beruya hapo hospitali ninaweza kuchelewa lakini sio sana. Usihofu" Aretha akamwambia mama yake wakati akipiga pasi nguo
"Retha una uhakika unataka kupambania ndoto zako na Simunge kwa wakati mmoja binti yangu?"
"Hmmmm....ndio Mama. Ni aidha nikose ndoto lakini sitaki kumpoteza Rian. Sikuweza kumpata baba wakati wote niliomtafuta nivune mapenzi yake." Akashusha pumzi ambazo mama yake alizielewa kuwa ni hisia za upweke ambazo zimekuwa mzigo mzito kwenye moyo wa binti yake.
"Siku moja ataelewa naamini. Na atanisamehe" mama akawaza moyoni
"Sitaki kumpoteza Rian mama. Na niko tayari kuwa kama dubu kulinda ndoto zangu" Aretha akamwambia mama yake
"Sawa binti yangu. Kila la kheri " mama akainuka na kumpisha Aretha akijiandaa kuondoka.
"Naamini nguo hii itanikaa vyema" akawaza wakati akivaa, alipomaliza akajitazama kwenye kioo, kisha akafunga nywele zake
"I am coming Rian" akatabasamu na kuchukua mkoba wake kisha akatoka chumbani na kumuaga mama yake sebuleni.
************
"Loy unasema ukweli au unanitaabisha?" Akauliza Allan baada ya kupewa jibu na Loy kuwa bosi wake hana nafasi kwa sasa kuonana na mtu mwingine..
"Bosi wangu Allan siwezi kuleta utani kwenye majukumu yangu ya kiofisi" Loy akajibu huku akitabasamu..
"Ratiba yake ilikuwa hivyo au imekuwa ghafla?" Allan akauliza akishangaa
"Hahahahha imekuwa hivyo tena, wewe mara zote huniambia mimi napenda umbea sasa nikikwambia utakuwa umejiunga na timu yangu"
"Loyce" Allan akamuita kwa ukali
"Oh samahani nimevuka mpaka" Loy akamjibu na kuweka sura ya kazi zaidi kisha akaendelea
"Bosi anazungumza na mgeni ameomba asisumbuliwe"
"Mama Simunge amekuja?" Allan akauliza akijua mtu pekee Edrian anaweza kumpa nafasi ya kuingilia ratiba yake ni mama yake pekee!
"Samahani bosi sio mama. Ni mtu mwingine" Loy akamjibu akijaribu kutunza maadili yake ya kazi.
"Oooh basi sawa Loy. Najua hutaki kuniambia ni nani. Uko sahihi. Nimekubana kiofisi hahahaha" Allan akageuka kuelekea ofisini kwake
"Umenibana bosi. Sawa tu" Loy akajibu huku akitabasamu kwa kuwa alimuacha Allan pasipo kujua mgeni huyo ni nani.
*****************