Aliposimama kwenye geti la nyumbani kwake, Edrian akageuka na kumwambia Coletha,
"Coletha tangulia nawapeleka nyumbani"
Aretha akageuka na kumwangalia Coletha huku akijaribu kutabasamu!
"Asante Coletha"
Coletha akamjibu kwa uchangamfu "Asante pia na karibu nyumbani"
akamuaga Frans na akashuka. Baada ya Coletha kushuka, Ed akaondoka gari kuwapeleka Aretha na Frans.
Njiani hakuna aliyeongea kila mmoja aliruhusu mawazo yake kumtawala hadi walipofika nyumbani kwao Aretha. Frans akamshukuru Ed kisha akashuka kwenye gari huku akipiga simu kwa mama yake ili awafungulie
Walipobaki wawili, Ed akamgeukia Aretha na kumwambia, "Retha unaniamini?"
Aretha akaitikia "Mmhm"
"BM sio mtu mwema" Ed akamwambia kwa ufupi
"Rian..ninajua una maadui hata kama huniambii ni kina nani...lakini sio kila mtu anaweza kuwa adui yako" Aretha aliongea huku sauti yake ikibeba dalili zote za kutaka kulia. Picha ya kule ukumbini ilipita akilini mwake na kukumbuka kilichomtokea Beruya.
"Retha, naomba uniamini katika hili ninalokwambia, mtu amekufahamu jina lako, ghafla yuko kwenye tukio linalokuhusu na amejitolea kununua picha zilizoharibika? Bado__"
Edrian akakatishwa na sauti ya geti lililofunguliwa, mama akatokeza na kuangalia mahali gari iliposimama. Akatabasamu na kuingia ndani akiongozana na Frans. Aliamini huenda kuna kitu cha msingi binti yake anaongea na Edrian.
Ndani ya gari Aretha alipoona mama yake kafungua geti, akataka kushuka lakini Ed akamuwahi na kumshika mkono,
"Retha please listen to me"
"Rian, naomba niende kupumzika, nimechoka" Aretha akamjibu Ed sauti yake ikionesha dalili zote za kukasirika
"Tutaenda wote Retha, nitaenda kumwambia mama nini kilichotokea"
"Nitamwambia mwenyewe, unaweza kuru__" kabla ya kumaliza sentensi yake Ed akafungua mlango na kushuka kitendo kilichosababisha Aretha naye kushuka kwa haraka. Edrian alipofika upande wa Aretha akamkuta ameshashuka
"Retha kwani kuna shida yoyote ikiwa ninataka kumwambia mama kilichotokea?" Edrian akamuuliza Aretha mara aliposimama mbele yake
Aretha akavuta pumzi akamuangalia Ed usoni, akakutana na macho yake ambayo yalionesha ustahimilivu na kujali, lakini ghafla ile picha ya Beruya ilipomjia kichwani uchungu ukapanda kifuani kwake,
"Nitamwambia mwenyewe Rian, naomba uende" akamjibu huku akijaribu kumpita lakini mkono wa Ed ukamuwahi na kumshika mabegani,
"Retha, una nini?" Akamsihi kwa sauti ya upole
"Naomba uniachie tafadhali Rian" kulikuwa na dalili za kilio kwenye sauti ya Aretha ambacho hakuweza tena kukizuia huku akijaribu kujitoa mikononi mwa Edrian
Edrian akaamua kumkumbatia kwa nguvu, Aretha akashindwa kujizuia tena akalia kwa uchungu huku akimlaumua. Ed hakutaka kubishana nae akaamua kumuacha amlaumu tu ikiwa angepata nafuu ya kusikilizwa.
Akiwa amemkumbatia ghafla Aretha akashusha pumzi kwa nguvu na mwili wake ukalegea, kama asingekuwa amemkumbatia kwa nguvu huenda angeanguka.
"Retha, Retha" akamuita lakini hakupata mwitikio wowote kwake. Edrian akamshika kwenye mshipa wa shingoni akagundua mapigo ya moyo yaligonga kwa mbali. Kwa sekunde hiyo kengele ya hatari ikagonga kichwani kwa Ed akamuinua Aretha haraka akamuingiza kwenye gari. Akawasha gari na kuondoka kwa mwendo mkali ambao uliwashtua waliokuwa tayari wameingia getini. Akashusha vioo vya gari kuruhusu hewa kupita vyema. Akaamuru simu yake ipige kwa mama yake Aretha
"Mwanangu mbona_"
"Mama, naomba niongee na Frans kama yupo hapo" Ed akamuomba, baada ya Frans kupokea simu, akampa taarifa na akamuomba amwambie mama pia. Akamsihi sana amwambie kilichotokea lakini amwambie kuwa wamerudi hospitali kumuona Beruya.
Ed alipokata simu akageuka kumwangalia Aretha ambaye alilala kwenye viti vya nyuma kwa utulivu
Akarudisha macho barabarani na kuongeza mwendo, akaamuru tena simu yake impigie daktari
"Hello Dr, ninakuja hapo tafadhali nikukute ER" akaongea na kuendelea kuyakwepa magari yaliyoonekana kumchelewesha.
Moyoni Ed aliwaza sana kama ni yeye ndio chanzo cha haya yote, akajisikia hatia na kujilaumu.
"Nisamehe Retha" akasema taratibu huku akipiga kona kuingia hospitali.