Chapter 151 - USALAMA

Baada ya usingizi wa masaa matatu, Edrian aliamka na kujiandaa, na sasa alikuwa barabarani kuelekea nyumbani kwao Aretha.

Simu yake iliita, akaangalia ilikuwa namba aliyoihifadhi kwa jina la "Intel" akapokea

"Hellow" akapokea

"Taarifa aliyopewa upande wa pili na huyo mtu aliyepiga ilifanya sura ya Edrian ijikunje ghafla, akashusha pumzi akaendelea kumsikiliza

"Na Beruya aliamua nini?" Akauliza

Akasikiliza majibu kutoka upande wa pili, akaendelea,

"Basi sawa, Asante kunitaarifu na endelea kunisaidia hapo"

Akakata simu na kisha akapiga simu na kuongea na mtu ambaye hakumtaja kwa jina

"Brother samahani nimekusumbua mida hii, nahitaji msaada wako.. inahusu hapo Southern Pole" akanyamaza kumruhusu mtu wa upande wa pili kumjibu kisha akaendelea

"Nina mtu nataka asiruhusiwe kuingia, nitakutumia taarifa zake mapema"

"Asante sana bro. Mapumziko mema"

Akakata simu. Akaendelea kuendesha gari mpaka alipofika nyumbani kwao Aretha. Akaegesha gari pembeni na kuingia ndani baada ya Frans kufungua geti dogo.

Akapokelewa na mama yake Aretha,

"Umefika wakati mzuri mwanangu, fikia mezani kabisa" akamkaribisha mezani ambapo chakula kilikuwa tayari kimeandaliwa

"Asante mama" Edrian alimjibu huku macho yake yakiangaza huku na kule

Mama akatabasamu maana alijua wazi alikuwa akitafuta kumuona Aretha ambaye alielekea chumbani baada ya kurudishwa na mama yake alipotaka kwenda kumfungulia Edrian.

"Frans hebu muite hiyo binti yangu atajizungusha kama hana mpango wa kula"

Frans akarejea akiongozana na dada yake.

"Karibu Rian" Aretha akamkaribisha Edrian huku akijaribu kuficha aibu nyingi alizokuwa nazo usoni..

Edrian akatabasamu na kumsalimia Aretha. Kwa pamoja wakaelekea mezani na kula chakula kwa pamoja.

Walipomaliza kupata chakula, Edrian alibaki akiongea na mama wakati Aretha alipoenda kujiandaa ili waweze kuondoka.

"Sasa mwanangu huo usiku mtakuwa salama kweli?" Akauliza mama aliyekuwa na wasi wasi uliokuwa wazi usoni kwake

"Mama tutakuwa salama usiwe na shaka na_" Kabla hajamaliza mama akamsogelea na kumwambia kwa sauti ya chini

"Mwanangu uwe muangalifu maana maadui wengi huwa na sura ya kondoo lakini ni mbwa mwitu"

Edrian ambaye hakuwahi kuwa katika ukaribu kama huu alionao sasa na mama yake Aretha alishtuka na kumwangalia mama usoni. Akaona msisitizo mkubwa katika maneno yake na muonekano wa sura yake.

"Sawa mama nitakuwa muangalifu zaidi kuanzia sasa" Edrian akamuondoa mashaka mama lakini akaamua kuuliza

"Mama, samahani lakini kwani kuna mtu ana shida na Retha?"

Mama akashtuka, akarudi kukaa vizuri, "aaah hapana mwanangu, Aretha alivyokuwa mbinafsi huyu, hana marafiki, yeye na picha zake tu unadhani atatoa wapi maadui!"

"Ooooh basi sawa, nilipata wasi wasi nikadhani labda kuna watu unawafahamu wanamuwinda Retha" Edrian akafurahi kusikia hivyo lakini alishangaa mama bado alikuwa na wasi wasi ndipo akatumia ajili yake kutambua

"Aahm mama, una wasi wasi sababu ya maadui wangu na sio wa Retha eeehm"

Mama akamuangalia kwa huruma Edrian kiasi cha kumfanya Edrian ashangae,

"Mwanangu, wewe ni mmoja kati ya watu maarufu hapa A-Town. Kuna watu wanatamani kukuona ukianguka na kuna wengine wanatamani kukupokonya ulichonacho. Najua unajilinda, ila sasa uko na Retha nawaza unahitaji kujilinda zaidi."

"Sawa mama, nimekuelewa, usiwe na wasi wasi sana, nakuomba uamini kuwa najali sana usalama wa watu wanaonizunguka na hasa Retha" akashusha pumzi lakini anatamani kujua hasa nini kilimsukuma mama kuona hivyo

"Mama, unawaza Retha anaweza kuwa mtego wa wao kuutumia na__"

"Shhhhhh" mama akampa ishara anyamaze baada ya kusikia hatua za Aretha aliyekuwa akija pale sebuleni

Aretha akafika sebuleni, Edrian akatabasamu kiasi cha kusahau maongezi yaliyoendelea na mama yake Aretha..

Akainuka ishara ya kuanza safari, "mama sisi tunaenda" akamuaga mama ambaye naye alisimama ili kuwasindikiza

"Sawa mwanangu...ukumbuke tulivyoongea"

"Sawa mama. Nitakumbuka kila kitu" akaongea huku akimuangalia Aretha machoni ambaye sasa alikuwa kwenye kushangaa nini kiliongelewa kati ya mama yake na Edrian ambaye alitabasamu sasa.