Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 150 - SITAYASALITI

Chapter 150 - SITAYASALITI

Beruya alishangazwa na wageni wa ghafla waliomtembelea pale ukumbini, alikuwa ni Melissa rafiki yake ambaye aliongozana na dada mwingine ambaye alivalia nguo nadhifu na za thamani pamoja na mwanaume mmoja ambaye naye alivaa vyema na kuonekana kuwa mtanashati

Baada ya kusalimiana, Beruya akawakaribisha kwenye meza iliyokuwa na viti vinne, ambayo juu yake kulijaa karatasi. Wakaketi.

"Samahani Bei, najua uko kwenye "Final touches" za onesho, Huyu anaitwa Joselyn ni rafiki wa Mr Simunge anahitaji msaada wako" Melissa akamwambia Beruya

Beruya akamgeukia Joselyn kwa uso wa mashaka akamwambia "Karibu sana, msaada gani naweza kutoa kwako"

Joselyn ambaye muda wote alinyamaza akimuangalia Beruya kwa dharau akatabasamu kisha akasema,

"Nimeambiwa utafanya onesho lako na Aretha, si ndio?" Akauliza

Beruya akatikisa kichwa kukubali huku akiendelea kumsikiliza Joselyn

"Mfukuze!" Joselyn akaongea kama mtu atoaye amri.

Beruya akashtuka akihamisha macho kutoka kwa Joselyn kwenda kwa Melissa ambaye alimpa mrejesho kwa kuitikia kwa kichwa. Alipozinduka kutoka kwenye mshtuko wa kile alichosema Joselyn, uso wake ghafla unapata mikunjo na akamgeukia Joselyn

"Kwa nini nimfukuze?, Na wewe ni nani hata uniamrishe"

Melissa alipoona Beruya amebadilika kimazungumzo akaamua kuingilia kati, huku akimshika mkono na kumvuta aende pembeni

"Bei sikiliza huyo dada ndiye mchumba halisi wa Mr Simunge, yule dada mwingine sio. Nasikia anatumia kila nafasi ili aonewe huruma. Mpango wake ni kumuibia Edrian na anatumia picha ili asaidiwe." Melissa akamwambia Beruya kwa sauti ya chini

"Kwani Melissa kuna sehemu yoyote ulimsikia Edrian akitutambulisha kuwa yule dada ni mchumba wake?" Beruya akamuuliza

"Bei acha utoto basi, sote tunamfahamu Edrian hawezi tu kuongozana na mtu mwingine namna ile. Josely ameniambia huyo dada hampi nafasi hata kidogo Edrian anamfuata hadi kazini, nyumbani kwao na kila sehemu anayoenda, sasa bado hufikirii anachotaka huyo dada?"

"Melissa sikubaliani na hiki unachoniambia na kama huyo Joselyn anataka kumsaidia Edrian akamwambie mwenyewe. Ila mimi sitayasaliti maneno yangu mwenyewe" Beruya hakusubiri Melissa aendelee kumwambia chochote, akageuka na kuelekea alipokuwa Joselyn

"Samahani Joselyn, siwezi kufanya kile unachokitaka" Beruya akamwambia akiwa amesimama huku akimuangalia Joselyn ambaye alikuwa akiangalia kucha zake akainua macho juu na kumwangalia ...

"Huwezi kumfukuza eeeh" akaongea kizembe sana Joselyn

Beruya alikerwa na tabia ile ya majivuno ambayo Joselyn aliionesha.

"Nina mambo mengi yakufanya samahani Melissa" akamwambia Joselyn kisha akamgeukia rafiki yake ambaye alionesha huzuni

"Lakini Bei_?" Kabla ya Melissa kumaliza Beruya akamkatisha

"Chochote utakachosema Melissa kuhusu hilo sitakusikiliza."

Joselyn akainuka na kumsogelea Beruya,

"Najua hunifahamu, na unaongea kwa sababu hujui hasara utakayopata ukiendelea kumkumbatia yule mwanamke" akashusha pumzi na kuendelea

"Tumia akili Beruya, wewe ndio unachipukia kwenye hii sanaa, hasara kidogo utapotea kwenye 'game'. Ningekuwa mimi nisingeruhusu onesho langu liingiliwe na mtu mwenye nia ovu kama ya Aretha hata_" Beruya akamkatisha kwa kuinua mkono wake

"Tafadhali Melissa ondoka na wageni wako, sina muda wa kusikiliza zaidi" akageuka na kuelekea kwenye shughuli zilizokuwa zikiendelea na kuwaacha Melissa na wageni wake wakimshangaa...

"Anakwenda kupoteza mtsssk" Joselyn akasonya na kuondoka huku nyuma akifuatiwa na Melissa ambaye alijaribu kumpoza Joselyn

Beruya akafikiri nini kinaendelea kati ya yule dada na Aretha.

"Aretha anaweza kuwa kweli ni mchumba wa Edrian au wanajaribu kunichanganya" akawaza amuulize Aretha au Edrian ikiwa angekuja kwenye onesho..

Akaamua kuliacha mpaka, amalize onesho lake lililotegemewa kufanyika siku iliyofuata. Wakati hayo yakiendelea pembeni mmoja kati ya waandaaji aliongea na simu yake akimpa mtu wa upande wa pili taarifa ya kile kilichotokea.

"Sawa boss, nitaendelea kuangalia na kukujulisha kila kinachoendelea" akaongea kwa sauti ya chini huku akiwa amejibanza kwenye kona moja iliyokuwa karibu ukumbi ule.