Chapter 148 - MKUTANO

Edrian aliamka asubuhi na mapema kama ilivyo kawaida yake japokuwa alichelewa kulala. Baada ya mazoezi ya asubuhi, akaingia bafuni na dakika chache baadae alikuwa akishuka kuelekea kwenye ukumbi wa chakula ambapo aliungana na Li.

"Vipi umeamka salama?" Edrian akamsalimia Li ambaye alishaanza kupata kifungua kinywa

"Salama bro, karibu" Li akaitikia salamu

Wakaendelea kupata kifungua kinywa pamoja. Mara kwa mara waligusia mambo yaliyohusiana na Mkutano wa bodi.

"Mama kasema tusimfuate Steve atamleta" Edrian akamwambia Li

"Okay" akaitikia Li.

Baada ya kumaliza kupata kifungua kinywa ndugu hawa wakasimama na kuelekea mlangoni tayari kuondoka lakini Coletha aliwaita kabla ya kutoka. Wakasalimiana

"Kaka nimewaombea usiku, naamini mtatoka na ushindi" Coletha akawaambia huku akiwaacha wenye tabasamu la furaha

"Asante baby sisy...worry not it's goin to be okay" Edrian akamjibu huku akimshika begani

Kama kawaida utani mfupi ulimtoka Li kabla hawajaondoka.

Mkutano ulitarajiwa kuanza saa nne asubuhi ya siku ile. Edrian na Li waliwasili saa moja kabla ya muda wa kuanza. Sehemu kubwa ya wafanyakazi katika jengo hili la Ashanti walikuwa mapumziko jumamosi hii.

"Kuna taarifa nyingine kuhusu Martinez na Mjinja?" Akauliza Edrian baada ya kumpigia simu Captain mara tu alipoingia ofisini kwake.

"Hapana bro, ila ninadhani kuna kitu kimejificha kuhusu Martinez, ni aidha kuna kitu anakitafuta au kuna mtu anamtumia"

"Mmmmmm" Edrian akaguna

"Tunaendelea kujaribu kudukua akaunti zake kuona mtiririko wa mapato yake" Captain akamueleza Ed

"Mmmhm basi sawa, nitasubiri taarifa. Tunaingia kwenye Mkutano muda mfupi ujao" baada ya kumaliza mazungumzo akakata simu na kutafuta namba ya Aretha kisha kumpigia

"Hellow princess bado umelala?" Akamuuliza

Sauti ya Aretha ilikuwa ya mtu atokaye usingizini. Edrian akatabasamu

"Tumia muda mrefu kupumzika Retha, kesho ni siku ndefu kwako" Edrian akamwambia lakini kabla ya kuendelea na mazungumzo mlango wa ofisini kwake ukagongwa na kufunguliwa, mama yake akaingia huku akiongozana na Li.

"Mama...karibu" Edrian akamkaribisha

"Asante mwanangu" mama akamshukuru huku akiketi kwa kulalamika kwenye kochi, kisha akaendelea

"Kwa hiyo mmekubaliana na uwepo wa Bwana Kussah kwenye bodi?" Akauliza mama

"Ndio mama. Vigezo vyetu vinamlinda Mjinja kuuza hisa zake kwa Kussah. Ila tuna mkakati tumeandaa, tutaanza kuzungumza kwanza na Felix kuhusu kununua hisa zake ili kuhakikisha "majority" zinaendelea kubaki kwetu"

Wakazungumza kwa ufupi kabla ya wote kuinuka na kuelekea kwenye ukumbi wa Mkutano, Loy aliwataarifu kuwa kila kitu kilikuwa sawa, ikiwemo kuweka nakala za ajenda za mkutano kwa kila mshiriki.

Baada ya kufika na kuhakikisha kila mmoja yupo, mkutano ukafunguliwa na mapitio ya ripoti mbalimbali za SGC ikawa ajenda ya kwanza. Kwa kuwa kila mshiriki alipokea ripoti mapema siku tatu kabla ya Mkutano, ilikuwa rahisi kujadili.

Edrian akiwa ni mwenyekiti wa Mkutano huo aliketi kwa utulivu kabisa, akijibu maswali na kupangua hoja zilizoonekana kumshtumu isivyo halali.

Mkutano huu ulibeba sura ya tofauti na mingine ambayo ilifanyika hapo nyuma. Kulikuwa na mvutano mkubwa kila mara ambao ulihoji mambo ya uendeshaji wa miradi wakitumia tatizo la G-Town kama kigezo cha Edrian kushindwa kusimamia vyema kampuni.

Lakini kwa kutumia taarifa alizojikusanyia mapema aliweza kuwajibu pasipo shaka.

Mrejesho wa mapato na matumizi yalielezewa vyema kipindi cha mchana baada ya wajumbe kupata chakula cha mchana. Walipoelekea mwishoni kama Edrian alivyopata taarifa, Benard Mjinja alitangaza kuuza rasmi hisa zake.

Edrian hakushangazwa hata kuonesha mshtuko wowote. Akatoa muda wa siku 30 kama makubaliano yao yalivyokaa kumleta mmiliki mpya wa hizo hisa.

Majira ya alasiri, Mkutano ulimalizika na kuwaruhusu wajumbe kuondoka mahali pale. Lakini Edrian alibaki na familia yake akiwemo Allan, Ganeteu ambaye ni mwanasheria wa SGC na Beno.

Wakafanya tathmini fupi ya matukio ya Mkutano ule, na kwa pamoja walikubaliana kuboresha mfumo wa uendeshaji.

Wengine wakaaga na kuondoka wakimuacha Edrian na Li ofisini.