Chapter 142 - MAMA

Siku zilikimbia haraka, kwa upande wa Edrian ratiba yake ya kazi ilimfanya atoke usiku akihakikisha kila ripoti imekaa vyema. Hakutaka kuwe na makosa yoyote katika ripoti zote zilizohusisha Simunge Group of Companies. Kwa kuwa wao ndio walimiliki hisa nyingi za kampuni alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha hawatoki kwenye nafasi yao, na alitafuta namna zote za kununua hisa kutoka kwa wamiliki wenye hisa chache. Mpaka sasa asilimia 62 ya hisa ilimilikiwa na Edrian Simunge kama mrithi wa Elvis Simunge.

Ijumaa hii alimaliza kikao cha kwanza na wafanyakazi wa SGC kwa upande wa Biashara ya Fedha ambayo ilikuwa chini ya Mkurugenzi Mtendaji Linus Simunge. Sasa alikuwa njiani akirudi ofisini kwake akitokea Exchange Tower.

"Hellow Captain" akapokea simu mara moja baada ya kuita

Uso wake kidogo ukabadilika kutokana na taarifa aliyopewa na Captain.

"Basi sawa. Nitaona cha kufanya" akamjibu na kukata simu.

Akaimuru simu yake iweze kumpigia mama yake. Baada ya sekunde chache simu ilipokelewa.

"Habari mama" akamsalimia

"Salama mwanangu, eeeh mbona umenipigia mida hii"

Usihofu mama, nimekupigia ili usije ukashangaa maana nimepata taarifa Mjinja ana mpango wa kuuza hisa zake" akamwambia mama yake ambaye alishangaa kwa kuwa Mjinja alikuwa rafiki wa karibu na marehemu mume wake. Haikuwa rahisi kuamini kama angefanya maamuzi kama hayo bila kumshirikisha wakati yeye alikuwa mtu wa pili ambaye alimiliki asilimia 15 ya hisa katika kampuni ya SGC

"Mama, nimekwambia mapema maana si tu kwamba anaziuza hisa bali ana mtu ambaye ameshaamua kumuuzia hizo hisa." Edrian akanyamaza kidogo na kabla ya kuendelea akasikia mama yake akihema taratibu

"Mmmhm nani huyo?" Akauliza mama yake

"Martinez Kussah" Edrian akamjibu mama yake huku sauti yake ikibeba hisia za kutofurahishwa na jambo hilo

"Eeeh Kussah ndio mnunuzi?" Mama akashangaa

"Ndio mama, na inaonekana anashawishi na wengine waweze kumuuzia hisa zao. Lakini usihofu nina mpango juu ya hilo" Edrian akamuondoa wasi wasi mama yake

"Sawa mwanangu. Najua jumamosi umejiandaa vyema." Mama yake akamtia moyo

"Sawa mama. Baadae" akakata simu na kuendelea kuendesha.

*************

Kwa Aretha alikuwa katika changamoto ya kuchagua picha gani itafaa kwenda kwenye onesho. "Eewhhhu yaani hakuna kazi nyepesi duniani" akalalama Aretha.

Akafanikiwa kuzipata ambazo aliamini kabisa zingefaa. Tangu kulipokucha mawazo yake yalikuwa kwenye picha. Alipokuwa akiziweka, macho yake yakakutana na picha mojawapo ya zile zilizobaki, akatabasamu!

"Siku moja nitakuonesha hii picha Rian" akawaza

Mlango ukagongwa na mama yake akaingia,

"Umemaliza?" Akauliza mama yake

"Nimemaliza mama" akajibu na kuendelea kupanga vifaa vyake mezani..

"Retha" akamuita

"Abee" akaitika

"Hebu acha kwanza unisikilize" akamuomba Aretha ambaye baada ya kusikia ombi la mama yake akasimama na kuegemea meza akimsikiliza mama yake..

"Aretha mwanangu unajua nafurahi kukuona unajitahidi kuishi ndoto yako. Namshukuru sana Edrian kwa msaada wake" mama akaanza kuongea taratibu huku akimwangalia usoni Aretha

Aretha alimwangalia kwa makini mama yake maana kwa kipindi hiki cha siku tatu alionekana kuwa na mawazo. Pamoja na Aretha kujaribu kumshawishi afunue kinachoendelea ndani yake lakini jitihada zake ziligonga mwamba. Sasa alihisi huenda mama yake yuko tayari kusema kinachoendelea

"Retha,.mh unaonaje kama ukienda Town M kumalizia masomo yako na ukaendeleza ndoto yako huko..naamini kule kuna fursa nyingi sana" mama akamwambia Aretha ambaye alimwangalia kwa mshangao mkubwa kwa sababu hata sauti ya mama yake iliyosema maneno hayo ilisikika ikiwa na majuto.

"Kwa nini mama?" Aretha akauliza huku akimkazia mama yake macho

Aaaah. .Retha, hapa naona kama utakuwa na changamoto nyingi za kupambana nazo na hasa yule binti ambaye anadhani umempokonya Edrian, bado mazingira ya hapa yana__"

"Mama" Aretha akamkatisha mama yake kwa kumuita, mwili wa mama yake ukakamaa baada ya kusikia kwa mara ya kwanza Aretha akimuita kwa sauti ya ukali

"Retha mbona_"

"Nini kinaendelea mama mbona huniambii" akamuuliza mama yake kwa huzuni