Mimi hapa" akaitika Aretha.
"Ooooh...karibu." alimkaribisha yule dada
"Naitwa Victoria lakini waweza niita V, na wewe utakuwa ni Coletha" akajitambulisha yule dada
"Yes, dada V, Coletha na huyu ni Aretha" Coletha akaitikia bila kuficha shauku ya wazi iliyokuwa usoni kwake kumuona Victoria. Dada huyu si tu alikuwa amependeza katika vazi alilovaa lakini kulikuwa na mvuto wa kipekee kwa uzuri aliokuwa nao.
"Coletha najua umeshavaa moja ya 'collections' zetu eeh" akamkumbusha Coletha wakati wakielekea kwenye safu ya magauni iliyokuwa upande wa kulia.
"Ndio da V, nilipendeza sana" Coletha akamjibu
"Oooh asante hiyo ni kwa kaka yako, Ed anajua kuchagua naweza kusema" akajibu wakati huo wakasimama.
"Aretha, Ed kanipa vipimo vyako kiufasaha nadhani hapa tutapata kitu kizuri cha kukufaa" V akamwambia Aretha huku akimwangalia juu hadi chini kisha akaanza kuchukua magauni. Akabeba rangi ya kijivu, bluu, pinki, njano na kijani ya jeshi, alipomaliza akaja mhudumu akazichukua na kupeleka kwenye chumba maalum cha kupimia.
Wakitoka wakaenda kwenye viatu, "Aretha unapendelea viatu virefu" akamuuliza baada ya kuwa wamefika kwenye safu ya viatu
"Haas..Dada Victoria_"
"Niite V tu wala usipate shida." Akamshika bega kumpa uhakika hakujali kuitwa hivyo
"V, sijawahi kuvaa virefu, ila naweza kujaribu kujifunza" akajibu Aretha
"Kweli unaweza kujifunza" akaongeza Coletha
V akatabasamu kisha akamwambia Aretha, "Kwenye tukio lako huwezi kuvaa kitu ambacho hujazoea, utajifunza kweli. Ila kwa leo tutachukua kile unachoweza kustahimili nacho. Na tutaongeza cha kuanza kujifunza. Sawa Aretha" V akamuelekeza, naye Aretha akaitikia kwa kichwa akifurahia namna ambavyo alikuwa mkarimu..
"Okay, sasa tuchague kwenye viatu. Coletha hapa kuna oda yako, chagua" akaendelea na Aretha katika kuchagua wakimuacha Coletha akiangalia naye nini angechagua.
Baada ya kuchagua wakaelekea kwenye chumba cha kujipima. Na hapo kulikuwa na wahudumu wawili ambao walikuwapo kusaidia.
"Aretha unajua unapendeza na kila gauni unalopima aisee" V aliyekuwa amekaa kwenye kochi akimwangalia Aretha.
"Hahaha umeona dada V ana damu ya nguo huyo" Coletha akachangia huku akitabasamu macho yake yakimwangalia Aretha.
Katika magauni yote V akachagua rangi ya bluu na njano huku Aretha mwenyewe akichagua rangi ya njano na kijani jeshi. V akawaambia wahudumu wafunge kile alichochagua Aretha. Wakapita kwenye urembo na hapa V ndie alichagua kila kitu hadi pochi ambayo ingeendana na magauni yote mawili.
Kwa upande wa Coletha, alichagua viatu na urembo. Wakiwa wanamalizia kwenye manukato sauti ilimuita V ambaye alikuwa akimsaidia Aretha kufanya uchaguzi wa manukato yenye kufaa usiku...
"Victoria, naona umepata wateja adimu sana"
V akageuka nyuma kuona nani aliyemuita
"Oooh Joselyn karibu sana" V akamkaribisha huku akiomba samahani kwa Aretha amuone Joselyn kwa dakika chache
"Asante, naona umeamua kuwahudumia wateja wako mwenyewe" Lyn ambaye alisimama hatua chache kutoka waliposimama kina Aretha.
"Ni sehemu ya majukumu yako Lyn, vipi utahitaji mhudumu wa kukusaidia?" Akauliza V huku akiangalia huku na kule na akamuona mhudumu mmoja ambaye alimuita...
"Hahaha hapana Victoria, nafikiri nami naweza kupata heshima ya kuhudumiwa na wewe" akasema Lyn huku akiinua jicho kumuangalia V ambaye kidogo uso wake ulibadilika...
"Kama utataka hivyo utabidi unisubiri nimalizane na hawa nilionao" V akamwambia huku akimuelekeza lilipo kochi, lakini Joselyn akatikisa kichwa kukataa
"Tsk. .tsk. .tsk..hapana V, hawa wanaweza kumalizana na mhudumu. Usisahau mimi ni VIP" Lyn akaongea huku akiweka tabasamu
"Lyn, acha drama, kila mteja ana haki sawa ya huduma. Na hata hawa wanatumia kadi ya VIP, siwezi kuwaacha wakati wamekuja kabla yako" V akamwambia Lyn akaendelea
"Unataka nikuhudumie nisubiri hapo kwenye sofa, ila kama una haraka nitafurahi kukuitia meneja aje akupe usaidizi" alipomaliza V akageuka na kurudi walipokuwa akina Aretha. Coletha alimwangalia Lyn kwa tabasamu la dhihaka
Joselyn akasonya "Hivi Aretha unadhani utakaa na Ed, atakuacha 'soon', furahia hivyo vinguo unapata"