"Nisingekuja Retha eeeh?" Edrian akageuka na kumwangalia Retha kabla ya kurudisha macho barabarani.
"No, simaanishi hivyo, Rian huwezi kuwa unakatisha ratiba zako kwa ajili yangu"
"Nimekukera kuja Retha?, au nimewaingilia ratiba na mwenzio?" Edrian akauliza kwa sauti ya upole
"Hapana Rian, mwenzangu yupi tena? Aretha akashtuka na kugeuka upande aliokuwa Ed lakini kabla hajapata majibu taa ya uelewa iliwaka akilini kwake akamuuliza
"Unamaanisha yule Charlz aliyenipokonya simu?"
Edrian akashtuka naye na kuuliza, "Yule ni Charlz?"
"Unamfahamu Charlz, Rian?" Aretha akauliza
Ndipo Edrian akajua amejiingiza kwenye kona ngumu itakayomhitaji atoe maelezo ya kumfahamu Charlz.
"Charlz simfahamu sana ila ninajua kuwa Derrick ana rafiki yake hapo chuoni anayeitwa kuna hilo hilo"
"Umejuaje kuwa huyu ni Charlz rafiki yake Derrick, au mmempa kazi ya kunifuatilia Rian?"
"Hapana, hapana Retha, ila nipe dakika chache nikufikishe nyumbani nitakwambia ukweli wote?"
Aretha ambaye alianza kuhuzunika moyoni alipohisi kuwa Charlz hakuwa rafiki aliyekuja kwake bali aliwekwa na Rian kumfuatilia,
"Sawa Rian. Nitataka nijue unawezaje kumuweka mtu anifuatilie" akasema kwa huzuni
"Ooooh tafadhali Retha usijisikie vibaya. Nitakwambia. Remember I love you"
Kimya kifupi kikafuata kati yao kila mtu akiwaza ya kwake. Aretha aliona anaingiliwa maisha yake, wakati Edrian aliwaza atajinasuaje kwenye maelezo ya Charlz.
Muda mfupi baadae walisimama nje ya geti la nyumbani kwao Aretha. Giza jepesi lilitawala, Ed akatumia mwanga wa taa ya nje iliyomulika upande waliosimama, akamwangalia Aretha na kugundua hakuwa na furaha yake ya wakati wote. Akakohoa kidogo kisha akaushika mkono wa Aretha na kuuweka kifuani.
"Retha, naomba uamini kuwa kila ninachofanya ni kwa ajili ya kukuweka salama." Akashusha pumzi na macho yake hayakutoka usoni kwa Aretha ambaye alikuwa makini kumsikiliza
"Ninao maadui Retha. Shughuli ninazohusiana nazo zinazalisha maadui na marafiki wengi. Kuna wakati ninawafahamu maadui zangu lakini kuna wakati siwajui na mbaya zaidi ni pale adui anakuwa mtu wa karibu na wewe. Hapa ndipo suala la usalama wako linakuja kichwani?"
"Unamaanisha siko salama Rian?" Akauliza Aretha
"Retha sitaki kusema hauko salama lakini hebu fikiria kama Joselyn anaamua kukuwinda ili akufanyie kitu kibaya, unadhani nitakuwa na hali gani?"
"Kwa hiyo umemweka Charlz ili anilinde au anifuatilie?" Aretha akauliza
"Hapana Retha, bali namhitaji aweze kuangalia mazingira yanayokuzunguka iwapo yataonesha dalili za hatari."
"Huamini mimi naweza kujilinda Rian hadi niwe na mtu anayeigiza kuwa rafiki kumbe la?" Aretha aliongea kwa huzuni kiasi cha kumfanya Rian ashtuke na kumvuta karibu kisha akamkumbatia..
"Retha sio hivyo. Tafadhali nielewe. Sikumuweka Charlz akufanye rafiki. Nilipojua Charlz yupo karibu nawe ndipo nilimuomba Derrick anisaidie kuongea nae ili awe tayari kunijulisha vitu au watu wa hatari wanaoweza kukuzunguka." Akamsogeza kwa nyuma ili kuangalia uso wake
"Retha siwezi nikakaa kama mtu asiyejua mazingira yangu. Huwezi jua ni mara ngapi nimeepuka mazingira hatari. Kulinda kile kilicho cha thamani kwangu ni kawaida siko tayari kusubiri hadi mambo yaharibike ndio nichukue hatua"
Aretha akashusha pumzi na kumwangalia Edrian usoni, "unadhani Joselyn anataka kunidhuru?"
"Huyo ni mmoja ninayemjua lakini wapo wengine siwajui na inawezekana wasitake kukudhuru bali watumie ukaribu wako kwangu kunitega. Kukwambia tu kuwa mwangalifu haitoshi Retha. Nahitaji mtu ambaye anaweza kugundua watu wabaya wanaojaribu kukusogelea"
"Na mtu huyo ni Charlz, Rian?" Akainua jicho lake na kumuuliza
"Retha, Charlz ni mwanafunzi kama wewe, ana ratiba zake pia. Kwa sasa nimemuomba ajaribu kuangalia iwapo kuna vihatarishi vyovyote lakini mbeleni nitampata mtu atakayefanya kazi hiyo na nakuomba usinizuie Retha"
Aretha aliyemsikiliza kwa makini akainama huku akikuna kichwa chake, na kabla ya kusema chochote Ed akaendelea
"Unakumbuka siku ile nakurudisha nyumbani tukapata ajali ndogo?"
Aretha akashtuka na kuinua uso kumwangalia Edrian ili aendelee