Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 108 - NIMEPATA NDUGU

Chapter 108 - NIMEPATA NDUGU

Edrian akatafakari sana maneno yale ya Aretha, akajua ni kweli jambo hilo ni gumu kwa wote. Yeye kuwa mbali na Aretha wakati ndio penzi lao limeanza kumea. Lakini kumrudia Joselyn ilikuwa kama mbwa kurudia matapishi yake mwenyewe.

Pamoja na yeye kuona na kufikiri hivyo bado alijua kwa Aretha ni mateso makubwa. Akashusha pumzi

"Retha.... nitakusikiliza wewe unataka nifanye nini kwenye hili"

Aretha akaangalia uso wa Ed ambao ulionesha kuwa katika mchanganyiko wa hisia. Akafikiri kwa sekunde kisha akafungua kinywa chake na kusema...

"Najua kwa hili utakuwa matatani zaidi lakini nakuomba Rian usijaribu kuruhusu ule ukaribu uliokuwa nao mwanzo, aweza kutumia mbinu nyingine na ukaingia mtegoni zaidi. Mimi nitatuhusu muendelee na huo mpango wa mama lakini mambo mawili nitayaomba kwako." Aretha akanyamaza kidogo na kumwangalia Edrian

Ed akatikisa kichwa kumuonesha kuwa anamsikiliza,

"Rian, naomba asije kuishi hapa, kitu kingine utatafuta namna ya kuonana nami walau mara mbili au moja kwa wiki." Alipomaliza Aretha akataka kuinuka lakini Ed akamuwahi akamvuta na kumkumbatia

"Retha, mbona kama hutaki" akahuzunika Ed

"Rian, najua nafanya kwa sababu nakupenda, na hii inajumuisha pamoja na kufanya yale nisiyokubaliana nayo lakini yatakulinda na kukupa furaha"

Ed akamkumbatia kwa nguvu zake zote akambusu sana kichwani na kwenye paji la uso mpaka aliposikia sauti ya Aretha ikimuita akamuachia na kumsogeza mbele...

"Asante Retha. Asante sana" akamshukuru sana

Akamuinua, wakasimama tayari kuondoka, wakafungua mlango na kutoka.

Coletha hakutoka sebuleni, alikaa macho yake yakitazama ngazi zilizoelekea juu. Aliposikia hatua kwenye ngazi akayapeleka macho yake kwenye runinga kuonesha alikuwa akifuatilia kipindi kilichoendelea.

Walipokaribia chini, Coletha akasimama

"Aretha karibu chakula tayari mezani" tabasamu lake likamkwamisha Aretha asijue nini afanye akatamani Ed amtetee lakini alipomwangalia alipigwa na butwaa kuona Ed akakubaliana na mdogo wake...

"Aaah... Coletha nafikiri nita__" Kabla ya kumaliza alishangaa mkono wa Coletha ukiwa umemshika tayari huku akimkokota taratibu kuelekea kwenye meza ya chakula. Edrian akawafuata kwa nyuma akitabasamu.

Mezani waliendelea kupata chakula kwa furaha huku zaidi Coletha akionesha dalili zote za kufurahia uwepo wa Aretha.

"Aretha uwe unakuja sasa umepafahamu, nitafurahi sana tuna mengi ya kuzungumza"

"Aah sawa nitakuja mara hizo nyingi" Aretha akajibu

Edrian alikula taratibu na mara kadhaa alimuongezea Aretha vipande vya samaki kwenye sahani yake. Aretha alitaka kukataa lakini umoja wa kaka na dada ulidhoofisha hoja zake..

Walipomaliza kula, Ed akaelekea mlangoni kuandaa gari kwa kuondoka akiwaacha nyuma Aretha na Coletha ambao maongezi yaliendelea huku wakitoka nje.

Ghafla wazo likamjia Coletha na kumfanya achukue hatua haraka huku akimvuta Aretha amfuate taratibu. Walipofika kwenye gari, Coletha akaelekea kwenye kioo cha mlango wa dereva ambapo alikaa kaka yake,

"Big brother, naomba tumsindikize wote Aretha"

Ed akamuangalia mdogo wake kwa mshangao kwa nini anaingilia nafasi ya yeye kuwa pekee na Aretha kabla hajatoa jibu, sauti ya Aretha ikamshtua

"Rian...ni sawa itakuwa vizuri apaone ninapoishi"

Coletha akataka kusema kitu lakini mdomo wake ukafunguka na kufunga akishangaa mambo yalivyoenda haraka kaka yake amekuwa Rian.

Ed naye alimwangalia Aretha aliyekuwa pembeni kwa mdogo wake akijiuliza imekuwaje hata Coletha kamshawishi akubali. Akahisi kuonewa na mdogo wake lakini hakuwa na namna nyingine ya kukataa akakubali yaishe. Alimfahamu mdogo wake akiwa na shauku na jambo anavyokuwa..

Coletha alipoona kaka yake kamkubalia akamvuta Aretha wakaingia viti vya nyuma wakimuacha Ed ambaye aliketi peke yake mbele.

"Aaaarrrgh" akalaumu kwa sauti ya chini kisha akawasha gari na kuondoka huku akisikia stori za mdogo wake alipokuwa akiongea na Aretha. Akatabasamu kwa namna ambavyo furaha ilikuwa wazi usoni kwa mdogo wake.

Coletha kwa uchangamfu wake mara kadhaa likifanya kicheko cha Aretha kusikika..

"Nitafurahi tukitembeleana Aretha, nitakuwa nimepata ndugu"