Chapter 90 - AHADI

Busu la taratibu lililoanza kwenye midomo ya Aretha likageuka na kuwa busu zito mfano wa watu wawili ambao walikuwa wamekaa mbali kwa muda mrefu pasipo kuonana. Ed hakumpa sekunde Aretha alimbusu kwa pumzi yake yote hata alipohisi hawezi kuendelea bila kupumua akamuachia..

"Ammh Rian" Aretha alihema kwa nguvu baada ya Ed kumpa nafasi ya kupumua. Macho yake yakiangalia chini Aretha akataka kusema kitu lakini Ed akamkumbatia...

"Tule kwanza Retha mchana sasa" Ed akamwambia kisha akamsogeza pembeni taratibu. Mahali walipokuwa wamekaa kulikuwa na mti mdogo uliovuta kivuli kiasi cha kuwatoshea kukimbia jua la mchana huu.

Ed akachukua mfuko na kutoa chakula wakati huo hakuna aliyeongea kitu kati yao. Aretha akaendelea kuangalia mandhari ya ziwa huku akifinya vidole vyake. Ed akaweka chakula kwenye kitambaa ambacho walikalia.

"Karibu unawe princess" Ed akampa ishara ya kumnawisha kwa maji yaliyobaki kwenye chupa. Aretha akatabasamu na kuweka mikono yake pembeni ili aweze kumtririshia maji. Wakala chakula kimya huku mara zote Ed akijizuia kumuangalia Aretha ambaye alishindwa kula vizuri alipokutana na macho ya aliyekaa pembeni yake.

Walipomaliza, Ed akaweka mabaki yaliyobaki na vifungashio vilivyobeba chakula kwenye mfuko. Akatoa juisi ndogo mbili za boksi akampa Aretha moja. Wakarudi kukaa.

"Retha"

"Abee" akaitika Aretha

"Nina jambo la kukwambia pia" Ed akaongea taratibu akivuta juisi kwenye mrija akaiweka pembeni. Akaangalia mbele akaendelea baada ya kuona Aretha akimgeukia kumsikiliza

"Nitakwambia kuhusu Joselyn, lakini nakuomba ujue kuna wakati maamuzi sahihi yanaweza kukubaliana na moyo na wakati mwingine yakapingana na moyo."

"Ahmmm" Aretha akaitikia kumpa nafasi Ed aendelee. Edrian akamsimulia Aretha alipokutana na Lyn mpaka alipogundua kuhusika kwa baba yake kuharibu kampuni yake. Hakujua kwa nini alikuwa huru kumwambia Aretha kila kitu lakini aliamini mtu aliyemuona akilia ameshuhudia sehemu ya siri ya maisha yake. Mama yake pekee ndie alijua nyakati kama hizo kwa Ed.

Akaendelea kumsimulia matukio ya hivi karibuni na akamwambia sababu ya yeye kutoendelea na Lyn.

"Retha, I am a man of my word, imenigharimu nguvu nyingi kuvunja kile nilichoamini kwa Lyn. Kile ninachojisikia kwako ni zaidi ya hisia, moyo wangu ni kama ulikuficha sehemu fulani hivi, tangu nilipokuona ulinipa hisia za kutaka umilele nawe" Ed akageuka na macho yake yakamfumania Aretha ambaye alikuwa akimwangalia na kumfanya aangalie pembeni kwa aibu!

Akatabasamu na kuinuka, akinyoosha mkono kumwelekea Aretha. Wakasimama wakiangalia maji yaliyong'arishwa na jua, mawimbi yaliyosafiri kuelekea chini ya ule mwamba.

"Ninakuomba uniruhusu tuanze hatua kwa hatua nikupende unipende. Sina shaka na hisia zako. Nakuomba usiwe na shaka na uamuzi wangu kuwa na wewe. Sikuahidi urahisi lakini nakuahidi uthabiti wa maamuzi yangu kwako." Ed akamgeuza Aretha wakaangaliana, wakipishana urefu kidogo.

Akaishika mikono miwili ya Aretha akamuuliza "Tunaweza kuanza hii safari pamoja, mimi nawe, Retha?

Aretha akainua macho yake na kumuangalia usoni Ed, "Tunaweza Rian"

Mikono ya Ed ilipita kwa haraka kiunoni kwa Aretha akamvuta na kumkumbatia huku akimshukuru "Asante Retha"

Wakakaa hivyo kwa sekunde kadhaa hadi alipomuachia.. akainama na kumbusu Aretha ambaye alimpokea huku machozi yakitiririka taratibu usoni kwa furaha akambusu sana.

Walipoachiana kila mmoja alihema kwa nguvu, Ed akayaona machozi usoni kwa Aretha akayafuta kwa kidole gumba.

"Nina sehemu nami nataka twende Retha" Ed akamwambia tayari akiinama na kutoa kitambaa akakikunja na kisha akachukua mfuko uliokuwa na uchafu. Aretha akamfuata kwa nyuma.

Ed akafungua sehemu ya buti la gari akaweka ule uchafu na kurejea kuingia kwenye gari. Aretha tayari alikuwa ndani ya gari.

"Retha, nimesahau kukuuliza, ulijificha wapi siku ile hata sikukuona?"

"Aaahhmmmm" Retha akashtuka na kugeuka kumwangalia Ed ambaye alimpa tabasamu na kuinua jicho

"Pale tulipokaa nyuma ya jiwe" Aretha akamuelekeza..

"Haaaa mbona niliangalia sikukuona" Ed akajibu huku kicheko chepesi kikimtoka akaondoa gari....