Aretha muda huu alichukua chupa ya maji akampa Ed huku naye akibaki na moja. Macho ya Ed hayakutaka kuangalia mbele ambapo kulikuwa na muonekano wa kuvutia wa ziwa Manir, zaidi alimuangalia Aretha usoni pasipo kuchoka na kumfanya.
Akanywa maji kidogo na kurudi kusubiri maelezo ya Aretha alipajuaje hapa. Aretha alikunywa maji taratibu huku akiangalia mandhari nzuri iliyokuwa mbele yake..
"Retha" Ed akamuita alipoona amenyamaza kwa muda lakini kabla hajaendelea Aretha akafungua kinywa na kusema..
"Rian..ni muda mrefu umepita tangu mimi nikuone mahali hapa" akameza mate huku macho yake yakibaki mbele
Ed akashtuka na kutaka kusema kitu lakini Aretha akamuwahi na kuendelea..
"Nilipotimiza umri wa miaka 21 nilimsumbua sana mama kuhusu baba yangu ambaye hatukuwa tukiishi naye tangu nikiwa mdogo" Ed aliposikia maneno haya akakaa kimya kumsikiliza mikono yake ilitamani kumkumbatia lakini akatulia tuli
"Katika harakati za kumtafuta, siku moja nikaambiwa anapatikana hasa PVB, niliazimu kumfuata. Nikafanya hivyo lakini sikumpata na hakukuwa na mtu aliyenitaka kunisaidia. Niliondoka nikiwa nimekata tamaa kabisa na sikuona raha yoyote ya kuishi..." hakukuwa na hisia yoyote usoni kwa Aretha ya huzuni lakini aliendelea kumwambia Ed
"Nikatembea huku machozi yakinitoka hata nikajikuta nimeacha njia niliyopaswa kurudi nayo, nikatokezea hapa" akanywa maji na kuendelea..
"Ndani yangu kusudi la kuishi sikuliona tena, nilipoangalia taabu na masumbufu niliyopata wakati nasoma nilikata tamaa. Niliookaribia hapa nikaona gari imepaki pembeni. Mwanzoni niliogopa nikadhani wanaweza kuwa watu wabaya, nikajificha"
Ed sasa akayarudisha macho kuangalia mandhari ambayo Aretha aliikazia macho.
"Ndipo nikakuona kwa mbele ukiwa umeinama, najua ulikuwa ukilia na kisha ukapiga magoti huku ukipiga mikono yako chini. Nilikaogopa na kuhisi utaumia, kwa kuwa nilikuwa na maji na kitambaa nikasogea na kuviweka pembeni yako. Ukiwa umeinama___" kabla Aretha hajamaliza maneno maneno yale mikono ya Ed ilimvuta kifuani kwake na hakuweza kuendelea kumwambia
"Retha...Retha...ulikuwepo siku ile..it was you" Ed akajitahidi kusema japokuwa alihema kwa shida na sehemu ya macho yake ilijaa machozi....
"Rian" sauti ya Aretha ikamshtua Ed ambaye alimkumbatia kama mtu ambaye hakutaka hata unywele wake uwe mbali naye..
Akalegeza mikono yake lakini hakuacha kumkumbatia mikono yake ikachezea nywele za Aretha
"Uliniletea maji nioshe michubuko niliyopata nami nikashangaa ni malaika gani alitumwa kunisaidia wakati nilipokuwa na huzuni kubwa" Ed akasema kwa sauti iliyojaa mikwaruzo..
"Rian..uliniokoa na maamuzi mabaya niliyotaka kufanya" Aretha akamshtua kwa hili
"Eehmm" Ed akamwachia huku akimuangalia usoni kwa mshangao..
Aretha akaangalia pembeni na kusema "maneno yako uliyosema baada ya kuosha mikono ndio yamenipa kuishi hata leo"
Edrian akashangaa kwa kuwa hakukumbuka nini alisema lakini anakumbuka alikuwa hapa miaka saba iliyopita baada ya kutoka hospitali ambapo madaktari walithibitisha kifo cha baba yake.
Alipenda kuja mahali hapa wakati wote alipojisikia na huzuni. Alipafahamu baada ya siku moja kwenda na marafiki zake PVB, kwa kuwa yeye hakuwa mtu wa starehe sana, kelele zilipomshinda akaamua kuendesha ili kupoteza muda kabla ya kuwapitia rafiki zake warudi nyumbani. Na ndipo alipotokea mahali hapa.
Tangu wakati huo mara zote hupakumbuka na kuja kutuliza mawazo hasa anapokuwa ahitaji usumbufu kutoka kwa watu.
"Nilisema nini Retha" akamuuliza akimuangalia usoni huku tabasamu lake lilionekana...
Aretha akamuangalia na akafumba macho akikumbuka maneno aliyosema Ed
**********************
Edrian akiwa na miaka 28 akainama moyo wake ukiwa mzito baada ya kutoka hospitali mchana huo ambapo taarifa za kifo cha baba yake zilisikika kwenye vyombo cha habari. Simu yake iliita mara zote kumpatia pole hivyo alipokuja hapa aliiacha ndani gari.
Akapiga kifua chake, akapaza sauti na kulia "Babaaaa....why now!" Akauliza katikati ya kilio chake.
Akapiga magoti na kuinama uso wake akauficha katika magoti yake, mikono yale ikagonga chini kwa nguvu hata kusababisha mchubuko wa ngozi.