"Retha, kuna mahali unataka twende?" Ed akamuuliza Aretha mara tu walipokaribia kwenye taa za kuongozea magari ili kuingia barabara kuu.
"Ahmmm" Aretha akashtuka na kumuangalia Ed kisha akarudisha macho pembeni.."aaah k..kama unapo pengine twende __"
"Hapana.. tunaweza kwenda popote utakapo, ninajua una sehemu Retha kama sivyo usingeniambia niwahi" Ed akamsihi
"Ahh.. nina..a, aam kuna mahali natamani twende sipajui jina ila naweza kukupa maelekezo" Aretha akamwambia
Ed ambaye sasa alisimama kusubiri taa kuwaruhusu kuingia barabara kuu, akageuka kumsikiliza Aretha, "Nielekeze"
Aretha akatabasamu, "tuelekee barabara inayoenda Pacific Villa Beach"
Ed akashtuka aliposikia maelekezo ya Aretha, "unapafahamu huko Retha?"
Aretha akageuka na kujitetea kwa kudhani Ed alimshangaa kuwa anapajua Pacific Villa kwa kuwa ni moja ya fukwe za starehe zinazojulikana kwa ufisadi.
"Aaah hapana Rian, ninafahamu njia hiyo ila tunapoenda ni mbele zaidi"
Kabla ya Ed kuendelea taa zikawaruhusu kuingia barabara kuu. Kwa kuwa Ed ni mwenyeji wa barabara akanyoosha na kuingia barabara kuu kisha mbele akakata kushoto na kuingia barabara ya Dzama, safari yao ikaendelea.
"Retha, am sorry" maneno yaliyomfanya Aretha kugeuka na kumwangalia Ed kwa uso wenye mshangao
"Am sorry kwani jana sikujua kama aa Joselyn angekuwa nyumbani kwa mama"
"It's okay... limepita hilo Rian" akasema kwa sauti ya upole hata kumfanya Ed ageuze macho kutoka barabarani amwangalie usoni
"Limepita lakini ninatakiwa kukwambia kile__"
"Rian" Kabla Ed hajamalizia Aretha akamuita
"Naam" kaitika
"Aaaammh..Tunapoenda hakuna sehemu ya chakula wala vinywaji unaonaje tukichukua kabisa?" Aretha akapendekeza
"Ooooh tutapitia hapo Pacific huwa wana chakula kizuri"
Wakaendelea na safari, walipofika PVB wakachukua chakula na vinywaji, Ed alifurahi namna ambavyo walionekana pamoja. Hakutaka kujificha tena hata Aretha alipotaka aende mwenyewe kuchukua chakula hakumruhusu akamwambia waende wote. Wakiwa kwenye mgahawa mhudumu alipompa mfuko Aretha, Ed akauchukua na kuubeba yeye.
"Rian, lete nibebe" Aretha akamsihi lakini Ed badala ya kumjibu akamvuta mabegani kitendo kilichomfanya ajikute ubavuni kwake. Mikono ya Ed ikakamata vyema bega la kushoto la Aretha.
"Nitabeba mimi princess" akainama na kumnong'oneza
Baadhi ya watu waliokuwa kwenye mgahawa ule wakawaangalia hatua kwa hatua. Ed hakutaka kusalimiana na yoyote aliwapungia mkono watu wachache aliowafahamu.
Wakaingia kwenye gari, uso wa Aretha ulijaa aibu na alishindwa kumwangalia Ed usoni mara walipoketi. Akatumia simu yake kuyaondoa mawazo yaliyoanza kuumbika kichwani kwake.
Ed ambaye alijua matokeo ya kile alichofanya kwa Aretha uso wake haukuondoka tabasamu tangu walipoondoka PVB.
Lakini tabasamu hilo halikudumu muda mrefu mara Ed alipoelekezwa na Aretha mahali ambapo wangeenda kukaa. Akaendesha gari kwa mwendo wa kawaida kwa kuwa njia hiyo ilikuwa haijatengenezwa kwa kiwango cha lami.
"Retha una hakika na tunakoelekea" Ed akauliza huku akimwangalia kwa wasi wasi, Aretha ambaye hakujali ule wasi wasi aliokuwa nao akatabasamu na kumwambia
"Nina uhakika Rian, it's my suprise for you"
Wakaendelea na kisha wakakata kushoto ambapo palionesha ni mwisho wa njia ya gari.. Aretha akamwambia washuke kwenye gari, Ed akafanya kama alivyoambiwa huku bado maswali yakiwa wazi akilini kwake
"Retha ulipajuaje huku?" Ed akamuuliza aliposhindwa kuvumilia maana sasa walisimama mwisho wa mwamba mahali ambapo walitazama ziwa Manir, fujo za mawimbi yake vilileta msisimko wa furaha.
"Rian tukae pale kwanza" Retha akamuelekeza mahali palipokuwa na majani mafupi ya kufaa kukaa. Retha akatoa kwenye begi lake dogo alilobeba mgongoni na kutoa kitambaa safi kikubwa na kukitandika chini.
Ed muda huu wote alikuwa kama mtu atembeaye ndotoni. Akamfuata Aretha ambaye alichukua mfuko mkononi mwake na kumuonesha kwa mkono aweze kukaa. Ed akafanya hivyo, akamuangalia Retha usoni akatikisa kichwa, alijiuliza ikiwa ni bahati kuwa Aretha anapajua hapa au kuna mtu alimwambia kuhusu eneo hili hata akamleta. Akabaki mshangaoni.