Chapter 86 - PRINCESS?

Saa tano na dakika arobaini, Edrian aliegesha gari nje ya geti la nyumbani kwao Aretha. Akashuka taratibu kwenye gari akajiangalia na kuachia tabasamu

Alivaa suruali nyeusi aina ya jeans, na shati yenye maua yaliyofifia sana rangi ya njano na nyeusi. Mguuni alivaa raba nyeusi, muonekano wake ulimpa sifa ya mtanashati. Alinyoa vizuri nywele zake na ndefu zake chache kidevuni zilipunguzwa sana.

Kwa hatua chache akasimama getini pembeni akisubiri, maana alimpigia Aretha kumwambia amefika na angetamani kumuona mama kabla hawajaondoka.

Sauti ya kufunguliwa kwa kitasa cha geti kulifanya moyo wa Ed kupata furaha zaidi. Geti lilipofunguliwa mbele yake alisimama kijana mdogo wa kiume wa takribani miaka kumi na nane.

Huku akimwangalia Ed alifungua kinywa kumsalimia lakini akakatishwa na salamu iliyomtoka kwanza kijana huyu ambaye aliachia tabasamu

"Karibu ndani, shikamoo"

"Marhabaa, asante" Ed akapiga hatua kuingia ndani baada ya kijana kurudi nyuma kumpisha. Alipoinua macho akamuona mama yake Aretha amesimama pembeni ya mlango akimsubiri.

Alipomkaribia alimsalimu kwa heshima huku mama yake Aretha akicheka..

"Mwanangu karibu, nisikusumbue kuingia ndani maana kuna mtu atanikaripia kutumia muda wake hehehhe"

Ed akachia kicheko chepesi huku akimsikiliza ambaye alimsogelea kidogo na kumwambia kwa sauti ya chini "ni binti yangu mwanangu nakuomba umtunze na utunze heshima yake" baada ya kusema maneno haya akaita "Retha"

Ed akitabasamu kufuatia maneno ya mama huyu, akafurahi zaidi alipoona mama akamuita Aretha hii kwake ilibeba maana moja kuwa mama yake Aretha amemuamini kuwa na ukaribu wa kimapenzi na mwanae. Huyu mama alimshangaza Ed maana ni kama alijua kuisoma mioyo yao.

Mlango ulipofunguliwa, Ed akainua kichwa chake kumtazama huyo aliyetoka ndani, macho yao yalipokutana Aretha aliwahi kuangalia pembeni huku akiinama chini kwa aibu

"Retha unapoteza muda wa mwenzio, au unataka kurudi ndani" mama alimshtua Aretha aliyekuwa amesimama akitafuta kitu cha kusema kwa Ed

"Umeamkaje Retha!" Ed akamsalimia pasipo kuondoa macho yake kwenye uso wa Aretha.

"Umm.. salama" akajibu na kupiga hatua kuelekea kwenye ngazi ambapo Ed alisimama.

Ed akayarudisha macho yake kwa mama akasema. "Asante mama, naomba tuondoke sasa"

"Haya mwanangu.....oooh nilisahau" mama akshtuka na kugeuka "huyu Frans kaenda wapi" akasema huku akionekana kumtafuta yule kijana aliyemfungulia geti Ed. Akaita "Frans"

Ed wakati huo alimpa nafasi Aretha apite na alisimama sasa pembeni yake. Macho yake yalifanya ziara kumwangalia binti huyu ambaye alivaa suruali nyeusi iliyomkaa vyema na blauzi ya rangi ya njano iliyokolea. Miguuni alivaa raba nyeupe. Alikuwa na muonekano wa kawaida lakini kwa Ed harufu ya upendo iliyomzunguka binti huyu ilimfanya kutaka kumkumbatia sana wakati huu.

"Ed, huyu ni kijana wangu anaitwa Frans, mdogo wake Retha. Usije ukampita siku moja ha ha" mama alimtambulisha kijana yule ambaye alitabasamu na kunyoosha mkono kumwelekea Ed

"Karibu sana"

"Asante sana" Ed akarudisha kwa furaha kwa kuwa alishangaa kijana yule alivyo na haiba njema ya kiutu uzima katika umri huo mdogo.

"Haya nendeni wanangu" mama akasema na kumfanya Aretha aliyekuwa kimya muda huu kumwangalia mama yake usoni kisha akaanza kuondoka huku nyuma akifuatiwa na Ed.

Walipoingia kwenye gari Ed akamwangalia Aretha aliyejaribu kuyakwepa macho yake

"Umependeza Retha"

"Umh...aa. asante Rian.. nawe pia" kajibu huku akimwangalia na kurudisha macho mbele.

Ed akasogea karibu na Aretha huku mkono wake ukielekea begani kwake. Mapigo ya moyo ya Aretha yakapata ghasia za haraka kiasi kwamba hakuweza kupumua kupumua vizuri. Ed akavuta mkanda uliokuwa pembeni ya kiti akaufunga huku akisema taratibu "Your safety is my priority princess"

"Ahmm" alishtuka Aretha na kumuangalia Ed kama mtu aliyetaka maneno yale ayarudie tena..

Ed akainua macho yake na kumtazama Aretha huku akitabasamu kumuashiria alichosema alimaanisha hata asiporudia..

Aretha akaangalia nje uso wake ukijawa na soni kwa kufikiria alichokisikia

Edrian akawasha gari na kuondoka, tabasamu likiwa usoni...