Mpenzi msomaji wangu, naomba uniwie radhi kwa kuwa kimya kwa muda bila kukuwekea mfululizo wa hadithi hii. Sababu za kimajukumu zilinikamata. Nimerejea na nitaendelea kukuletea vipande vizuri vinavyoendelea. Asante kunivumilia
*******************************
Asubuhi ya jumapili hii Edrian hakuamka mapema, hata kumfanya Li kuwa na wasi wasi kwa kuwa si kawaida yake.
Li akasimama kwenye mlango wa kaka yake ikiwa saa tatu asubuhi akaamua kugonga huku akimuita "brother"
Baada ya dakika kadhaa za kugonga kitasa cha mlango kilifunguliwa, Edrian akafungua mlango kumruhusu Li kuingia, lakini hakuingia zaidi ya kumuuliza kaka yake kama alikuwa salama,
"Niko salama Li, nimelala kwa uchovu mwingi na nilihitaji huu usingzi" akajibu Ed huku akipiga miayo kuonesha bado alikuwa kitandani
"Basi, ngoja nikuache.. umenishtua tu" Li akageuka na kumuacha Ed ambaye alirudi chumbani, mara alipoangalia saa yake akatabasamu, "muda unakuja haraka sana Retha, leo sitouacha moyo wangu ubaki katika giza, nitasema" akawaza moyoni. Akachukua simu na kuangalia mazungumzo yake na Aretha mara aliporejea nyumbani. Akaangalia jumbe mbili za mwisho uso wake ukang'aa kwa furaha iliyokuwa wazi machoni pake.
"Rian, nawe ulale sasa na usiamke mapema kama ulivyozoea. Pumzika mara moja kwa wiki" haya maneno aliyaandika Aretha mara tu Ed alipoingia bafuni usiku ule aliporejea.
Ujumbe wa pili ulimfanya Ed acheke mwenyewe
"Rian I love you"
Hakuamini mara alipotoka bafuni usiku ule na kusoma ujumbe huu. Alijitupia kitandani huku akirudia kusoma mara kadhaa. "I love you too Retha" alisema taratibu kwa sauti ya chini lakini hakujibu wala kuandika chochote kwa Aretha. Akaamua kufanya kama alivyoelekezwa, kulala wakati huo na kutoamka mapema.
Kama mtoto mchanga alilala, na kama asingekuwa Li angeendelea kulala. Pamoja na kuwa mama yake Ed alikuwa akimsisitiza mara zote kuwa na muda wa kumpumzika lakini hakuwahi kulala kama alivyolala leo.
Alipomaliza kurudia maneno yaliyoandikwa kwenye ujumbe wa Aretha, Ed akainua simu na kumpigia mama yake kama ambavyo hufanya wakati wote anapokuwa kapumzika nyumbani. Wakaongea na mama yake akiahidi kwenda jioni ya siku iliyofuata ili kumuelezea hali ilivyo katika maamuzi yake. Alipomaliza akamtafuta Coletha na kisha mdogo wake Derrick. Mwisho akampigia mama yake Aretha
"Oh mwanangu umenikumbuka?"
Ed akasalimu "ndio mama, shikamoo"
Baada ya mazungumzo mepesi, Ed akamtaarifu kuwa ataenda na Aretha sehemu, hivyo alihitaji ruhusa kwa ajili ya binti yake..
"Hakuna shida mwanangu, kumbuka mambo mawili niliyokuomba uyazingatie"
"Sawa, nitazingatia mama. Retha atakuwa salama." Ed akamhakikishia. Wakaongea machache na mama yake Aretha kisha akakata simu na kushusha pumzi. Akaandika ujumbe mfupi kwa Aretha...
"Nimefuata maelekezo yako Ritha. Nimeamka muda si mrefu." Akatuma huku kidole chake akipapasa sehemu ya ujumbe wa "I love you" alioandika Aretha. Akaongeza na ujumbe mwingine kabla ya kusubiri ule wa kwanza upate mrejesho.
"Uwe tayari dakika 15 kabla. Nitawahi kuja Ritha"
Akaelekea bafuni sasa akitabasamu, "nitakwambia Retha, leo nitajaribu safari mpya ya mapenzi, kama moyo wangu ulivyokuridhia"
********************
Aretha alipoona kimya baada ya kutuma ujumbe wa mwisho kwa Ed akajisikia vibaya akihisi huenda amekosea kumwambia kuwa anampenda. Maneno ya Li ndio yalimpa ujasiri wa kumwambia Ed kile ambacho kiliujaa moyo wake. Furaha yake ikaingiwa na wasi wasi akifikiri hayumkini maneno ya Li aliyaongea tu kumpoza hali ya hasira aliyekuwa na nayo..
"Aaargggh" akagugumia huku akiinuka. Akaelekea kwenye chumba chake cha kuchora. Akakaa humo mpaka usiku sana aliposhtuliwa na mama yake ambaye aliinuka usiku huo na kumtoa mbele ya picha aliyokuwa akichora.
"Retha angalia afya yako kwanza, kalale"
Mama yake akamsukuma. Akaondoka na kuelekea chumbani kwake.
"Usingemwambia, umefurahi kiasi cha kushindwa kujizuia" akajilaumu baada ya kupanda kitandani. Alihisi kukata tamaa kwa kuwa Ed hakuwa amejibu ujumbe wake ulioeleza hisia za moyo wake.
Hakujua kuwa maneno yake yalipokelewa kwa furaha.
Na asubuhi ya leo hakutoka kitandani mapema sababu alihisi uchovu kwenye mwili wake. Lakini ujumbe wa Ed aliotuma akimwambia amefanya kama alivyomwambia, ulimpa tumaini lililomfanya kutoka kitandani na hasa baada ya kuona anatakiwa kuwa tayari dakika 15 kabla ya muda waliokubaliana.