"Karibu ujifunze binti yangu" mama alichukua glovu na kumpatia Aretha ambaye alizipokea na kuvaa. Akaongezewa na aproni ili asiweze kuchafuka
Wakaendelea kuweka vipande vya kuku katika vifungashio. Aretha alimuangalia jinsi huyu mama alikuwa akiweka naye akafanya hivyo hivyo. Mara kadhaa mama alimuuliza maswali ya familia yake lakini kwa sababu ya kelele hawakuweza kuelewana vyema. Mashine zikazimwa baada ya oda kukamilika, kazi iliyobaki ikawa ni kuziweka tu kwenye vifungashio..
Aretha alifurahia maana hakuwahi kuona kuku wengi hivi na shughuli yake ya uandaaji.
"Huyu binti yangu sijui kaelekea wapi, anapenda kula nyama lakini hataki kuiandaa" mama alilalamika na moja kwa moja Aretha akajua anamuongelea Coletha.
Akatabasamu huku akiendelea kuweka kuku,
"Aretha mwanangu unaishi na wazazi wako wote?" Akauliza mama yake Ed.
"Hammm..hapana. mama ndio yuko hai ila baba yangu alishafariki" Aretha alisema maneno haya pasipo kuonesha huzuni ya aina yoyote.
"Oooh pole sana" mama akampa pole.
"Asante" mama yake Ed alishangaa maneno yake hayakuonesha hisia yoyote. Akaamua kuendelea na maongezi
"Uliwahi kuwafahamu vijana wangu kabla?"
"Aaahm" akashangaa kwa kuwa hakujua anamaanisha wanae wote au Derrick na Ed. Kabla hajaonekana kushangaa zaidi mama akamuwahi..
"Ulimfahamu Derrick kwanza au Ed?"
"Oooh..Ria.ah Edrian kwanza na ndio nikamfahamu Derrick" kidogo angetaja Rian, aaah Aretha akainama kwa aibu kwa namna alitaka kumrejea Edrian
"Nikajua ulimfahamu Derrick mjanja mjanja sana yule"
"Hapana mama"
"Mpaka hapa panatosha mwanangu. Watamalizia wengine." Mama akamshukuru Aretha, kisha akainuka na kumuita mmoja kati ya vijana waliokuwa wakisafisha mashine.
"Lex, hebu niitie Ann na Joy wamalizie hapa, naingia na mgeni ndani"
Aretha akainuka na akatoa aproni na glovu alizovaa, akielekezwa na mama kuziacha pale pale. Wakasafisha mikono yao na kuingia kwenye nyumba ile kubwa. Jikoni wakamkuta Coletha akiendelea na mapishi yake..
"Ona ulivyo mvivu, kuwashughulikia kuku hutaki ila kupika na kula asssshhh." Akamsema Coletha
"Mama" aliita kwa kulalamika.
Aretha akainama na kutabasamu akiwafurahia mama na binti yake.
"Aretha karibu hapo mezani upate walau chakula kidogo...Mama ashakunyonya damu na hao kuku" Coletha akamkaribisha Aretha kwenye meza ndogo ya chakula iliyokuwapo pembeni ya jiko lao.
"Mwanangu usiogope kaa hapo uonje mapishi ya mwenzio, yakikushinda achana nayo...anapika pika vitu sivielewi kila akija" mama akamwelekeza Aretha huku yeye akiingia kwenye friji na kutoa chupa ya maji akaelekea kukaa kwenye meza ile ile. .
"Coletha, Ann ameenda wapi aje asaidizane na Joy?"
Kabla hajajibu, kengele ya mlangoni ikaita,
Coletha akapunguza moto wa jiko "Sijui nani aargh mwisho niharibu kuku wangu....Ann amepeleka maziwa kwa Mpeta walipiga simu wakati uko huko" Coletha akaenda mpaka sebuleni kabla hajafungua mlango sura yake ikajikunja
"Wooooi huyu naye kafata nini hapa tena"
Wakati kasimama pale kengele ikaita tena,
Coletha akasogea na kufungua mlango,
"Wifi yangu, habari ya siku" Lyn akaachia tabasamu akimsalimia Coletha ambaye ni wazi alikerwa na kumuona pale...
Coletha nae akaweka tabasamu feki, "karibu Lyn"
"Asante" Lyn akasogea na kumfanya Coletha aliyeganda mlangoni kusogea kumpisha aingie. Akafunga mlango na kumfuata nyuma Lyn ambaye hakusubiri akaribishwe kukaa, akaketi kwenye kochi taratibu huku akiangaza macho yake..
"Mama yuko wapi wifi" ile wifi alivyoisema Lyn ilikuwa na msisitizo kumkera Coletha
"Yuko jikoni, anaongea na mgeni" Coletha nae akaweka msisitizo wa mgeni kuonesha huyo mgeni alivyokuwa wa muhimu
Lyn akainuka na kumwambia Coletha "nipeleke nimsalimie na mimi ni mgeni wake"
"Subiri amalize una haraka ya nini" Coletha akamjibu. Mlango wa kuingia jikoni ukafunguliwa na mama akasimama lakini kabla hajasema chochote akamuona Lyn
"Oooh binti yangu karibu" akamkaribisha kisha macho yake yakarudi kwa Coletha
"Huko jikoni ni mimi napika au wewe?" Akauliza kisha akamgeukia Lyn ambaye uso wake ulionesha unyenyekevu
"Karibu huku mwanangu" mama akamkaribisha