Geti dogo lilifunguliwa na mlinzi, Ed akashusha kioo akamsalimia, kisha akamjulisha kuwa hatoingia ndani, bali akamuomba ampeleke Aretha ndani kwa mama yake.
"Retha, relax. Enjoy the moment!" Ed akamhakikishia Aretha.
Aretha akaachia tabasamu "Asante" akageuka ili kushuka
"Asante nani Retha" Ed aliuliza huku akimwangalia na tabasamu lake
"Hmm" Retha akageuka kumwangalia, akakwepesha macho na kugeuka ili kushuka akasema "Asante Rian"
"Sawa Retha, nitakuja baada ya masaa matatu."
"Sawa"
Aretha akaingia na mlinzi kwenye geti akimwacha Ed aliyekuwa aligeuka gari tayari kuondoka. Hakutaka kubaki kwa kuwa alimjua mama yake angemuuliza kwa nini amekuja.
Akaamua kuelekea kwa Brian wakati akimsubiri Aretha.
******************
Aretha alipofikishwa na mlinzi kabla hawajabonyeza kengele tayari Coletha alifungua mlango na kumkaribisha ndani Aretha.
"Hatujaonana tangu birthday ya mama!..unaendeleaje Aretha?" Coletha akamsalimia wakati akimuelekeza mahali pa kukaa..
"N..niko salama, sijui wewe?" Akajibu na kukaa kwenye kochi
"Niko poa. .nilisahau kuchukua namna yako ya simu na huyu 'hopeless twin of mine' akaninyima. Anyway leo nitaichukua mwenyewe" maneno haya yalimfanya Aretha atabasamu.
Sawa...aah samahani ..ni Coletha eeeh? Akauliza Aretha macho yake ya upole yakimwangalia Coletha..
"Ndio dear, Coletha pacha wa Derrick rafiki yako"
"Aaaah nashukuru kukuona aah tena" Aretha hakuficha uso wake ambao ulionekana kumfurahia Coletha..
"Mimi zaidi, ngoja nimshtue mama, kaamka na oda ya kuku basi hawapi kupumua watu.. sasa hivi atakuja" Coletha akamjulisha huku akielekea kwenye mlango ulionekana kuelekea jikoni. Lakini kabla hajasukuma mlango, Aretha akamuita
"Coletha"
Akageuka na kukutana macho na Aretha ambaye alisimama
"Niambie dear" Coletha akamuitikia
"Ah. .unaonaje usimuite aa. .mama kama yuko na kazi nyingi ..nitaenda kumsalimia" Aretha aliongea huku akipangusa mikono kwenye gauni lake kwa wasi wasi...
"Aaaah. ..hapana huko mimi mwenyewe pananichosha, damu damu tu..Aretha kaa atakuja___" Kabla ya kuendelea kumshawishi kubaki Aretha akawa amepiga hatua kumkaribia Coletha
"Please usimtoe nipeleke nitamsalimia huko"
Coletha akamwangalia usoni Aretha kisha akamshika mkono
"Haya twende, ila usinilaumu usipojisikia vizuri dear"
"Usijali" Aretha akashukuru. Ndani ya moyo wake aliona vyema kukutana na huyu mama akiwa na shughuli zake, akiamini atakuwa na muda mchache wa kumuuliza uliza maswali.
Wakapita kwenye ule mlango uliowapeleka kwenye sehemu kubwa ya jiko. Wakaelekea kwenye korido iliyowatoa mlango wa nyuma. Na wakaingia kwenye baraza kubwa na kuelekea nyumba nyingine iliyokuwa nyuma. Walipishana na wasichana wawili ambao walibeba mifuko mikubwa. Wakaingia kwenye ule nyumba, ulikuwa ni ukumbi mdogo ambapo kilikuwa na watu wachache ambao walikuwa na kazi waliyokuwa wakifanya huku mashine tatu zilikuwa mbele yao.
Baada ya kuingia Aretha alielewa kwa nini Coletha alikataa asije, kwa kuhofia namna gani angeweza kustahimili harufu ya nyama za kuku zilizokuwa zikiandaliwa kwa msaada wa mashine ..
"Wewe Coletha mbona umemleta mgeni huku" akaongea mama yake kwa sauti kutokana na mlio wa mashine zilizokuwa zikiendelea kuchinja, kunyonyoa na kukata vipande.
"Mama ametaka kuja kuona unachofanya" akajibu kwa sauti na yeye.
Aretha akabaki mdomo wazi kwa jibu la Coletha, akajiuliza ni kwa namna gani watasikilizana. Akafurahi kuwa kama watakuwa kwenye hizi kelele basi watafanya kazi zaidi ya maswali.
"Njoo mwanangu, Coletha leta kiti hapo akae mgeni wangu" akamuita Aretha na wakati huo Coletha akaleta kiti na kumkaribisha Aretha akae. Mahali alipokaa mama huku kulikuwa na meza ya chuma ambapo viliwekwa vipande vya kuku na yeye alikuwa na kazi ya kuviweka kwenye mifuko maalum.
Aretha akamsalimia mama yule ambaye aliitikia huku akiendelea na kupanga vipande vya kuku.
"Mwanangu samahani umenikuta na ubize huu lakini usijisikie vibaya"
"Hapana mama, nimefurahi kuona shughuli yako" Aretha alijitahidi kuongea kwa sauti asikike
"Karibu ujifunze binti yangu" mama alichukua glovu na kumpatia Aretha.