Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 72 - MARA YA KWANZA

Chapter 72 - MARA YA KWANZA

Saa nane kamili mchana Edrian akaegesha gari yake nyumbani kwao Aretha. Pale getini aliwaza kama itakuwa sawa kwa yeye kuingia ndani ili aweze kumsalimia mama yake... akapiga simu ya Aretha na kumjulisha kuwa yuko getini na angetamani kumsalimia mama yake. Aretha akamjulisha kuwa mama yake ametoka yupo yeye na mdogo wake.

Dakika mbili baadae geti dogo lilifunguliwa na Aretha akatoka. Edrian alimuangalia kwa uso wa furaha Aretha ambaye alivaa gauni ya rangi ya bluu ambayo haikuwa ndefu sana na chini alivaa raba nyeupe. Nywele zake alizifunga nyuma na kufanya uso wake kuonekana vizuri sana.

Akafungua mlango wa nyuma ili aingie lakini Edrian akamuwahi

"Naomba unipe kampani hapa mbele" Ed alimuomba Aretha kabla hajaingia kiti cha nyuma. Aretha akarudisha mlango na wakati huo Ed alimfungulia mlango kwa ndani, Aretha akapanda na kuketi. Ed akawasha gari na kuondoka kuelekea USA Estate kwa mama yake.

Ed alimuibia jicho mara kwa mara Aretha ambaye ule ujasiri wake wa kwenye simu haukuwepo tena. Mikono yake ilikuwa bize ikichezea vidole vyake mwenyewe na macho yake hayakuangalia mbele bali pembeni.

"Retha" Edrian alimuita taratibu

"Mm" Aretha aliitika pasipo kugeuza shingo yake kumuangalia Ed.

"Unaogopa?" Akamuuliza

"Eeeh. .. aaa. .kuogopa nini?" Aretha akageuka kumuangalia kwa haraka Ed kisha akarudisha shingo yake dirishani

"Usiogope, mama yangu hang'ati watu" Ed akasema huku akitabasamu

"Aahh" Aretha akaitikia, alitamani amwambie Ed yeye ndio sababu kuu ya vile anavyojisikia maana hisia zake huvurugika pale anapokuwa karibu nae.

"Relax, uwe huru kabisa. Muone kama mama yako alivyo" Ed akaendelea kumsaidia Aretha ajisikie vyema, ambacho hakujua ni kuwa yeye ndie alikuwa chachu ya hali ile ya Aretha. Alishangaa ujasiri wa kwenye simu hakuwa anauona ndani ya binti huyu ambaye aliyakwepa macho yake wakati huu wote..

"Ooh okay Eee..d.. Rian" alikwama kwama Aretha.

"Rian ni zuri zaidi" Ed alijibu huku macho yake yakiwa barabarani na usoni kwa Aretha

"Eeeh" Aretha alishtuka na kumwangalia machoni kwa mshangao kabla ya kuyapeleka mbele macho yake..

"Yes..Retha. Niite Rian. Nitafurahi" Ed alimwangalia Aretha na akarudisha macho barabarani...

"Kwa nini?" Aretha aliuliza mara

Ed aliyekuwa amekazana kuangalia barabarani baada ya taa kuruhusu magari kuondoka, akageuza macho na kumwangalia Aretha.

"Kwa sababu ni mara ya kwanza nimeitwa hivyo na wewe. Huoni sababu kwa nini nisifurahi"

"Oooh, sawa aah a ...Rian" Aretha hakuwa na namna zaidi ya kukubaliana na Ed. Hata yeye anayo sababu ya kumfupisha hivyo...

"Safi. Asante Retha" Ed akaweka msisitizo kwenye jina lake huku akitabasamu

Aretha akaliona tabasamu lile, mikono yake akaikunja huku akigeuka kuficha tabasamu ambalo lilikuwa wazi mdomoni mwake.

Kimya kifupi kikapita kati yao, kila mmoja mawazo yakipita huku na kule wasijue mwisho wa mawazo yao ni mmoja ikiwa wangeongea.

Aretha alitamani kuanzisha mazungumzo ya nini Edrian aliongea na mama yake maana aligundua kuna tofauti kidogo katika namna mama yake amekuwa akihusiana naye siku hizi

Edrian naye alitamani kumwambia Aretha namna ambavyo anatamani ajue hisia zake zinayoenda vururu vururu kila mara anapomuona. Mwili wake ulitaka kumkumbatia wakati huo lakini alijizuia.

Kimya kilipozidi Ed akaamua kuongea, "Retha"

"Amhmm" aliitika Aretha na kugeuza macho yake kumwangalia Ed

"Kesho uliniahidi tutakutana, unakumbuka?"

"Oooh nakumbuka" akajibu, akaongeza "au utakuwa na ratiba nying____"

"La hasha" Ed kwa haraka akamkatisha Aretha ambaye aliachia tabasamu

"Nakumbuka ni kesho Rian" Aretha akamhakikishia..

"Utapenda tukae ufukweni au sehemu ya ndani?"

"Ufukweni" Aretha akajibu mara

"Basi sawa, unapenda kula nini?"

"Chochote... Rian" Aretha akajibu lakini wakati huo huo akageuka huku tabasamu lake halikumpita Ed bila kuliona.

"Okay.. nitashukuru sana nikiiona na picha iliyokuchelewesha kulala jana." Ed akasema haya wakati tabasamu lake likiwa wazi usoni kwake..

"Eeh" Aretha alishtuka na kumwangalia usoni Ed ambaye wakati huu alikuwa bize akipiga honi mbele ya geti la nyumbani kwa mama yake.