"Edrian" sauti dhaifu ya Lyn ilimuita baada ya kuingia ndani ya kile chumba alichokuwa amelazwa. Martinez na mkewe wakasogea pembeni kumwachia nafasi aweze kupita wao wakibaki kusimama kando.
Ed hakuwa na namna zaidi ya kusogea kilipokuwa kitanda, "unaendeleaje". Akajikaza kumuuliza huku akiwa amesimama karibu na kitanda.
"Sitaendelea vyema kama unamsikiliza Retha kuliko mimi" machozi yalitiririka pembeni ya macho ya Lyn taratibu
Ed akiwa katika mshtuko wa kutojua ajibu nini, Martinez akamuwahi
"My sweet daughter, usiseme hivyo, Ed si mtu wa hovyo, anakujali na atakusikiliza" wakati akisema haya maneno Martinez akasogea ili kumfariji binti yake. Lyn akamzuia kwa ishara baba yake, akainua mkono kumuonesha Ed akae pembeni yake.
Ed uso wake ulikuwa hauna hisia yoyote ambayo ungeweza kuielezea, huzuni, huruma au nyingineyo. Akakaa pembeni ya kitanda kama Lyn alivyomwelekeza. Mara alipokaa Lyn aliachanisha mikono yake kuonesha kutaka kumbatio kutoka kwa Ed ambaye alikakamaa akitamani kutofanya hivyo lakini akaamini ubinadamu kwa sasa ulihitajika zaidi ya hasira alizokuwa nazo. Akasogea akamkumbatia Lyn kwa haraka, lakini Lyn hakumpa nafasi ya kumwachia, akaendelea kumkumbatia huku akisema kwa sauti ya chini
"Niamini Edrian, hatutaachana mpaka niamue. I love you." Kwa maneno yale Edrian alirudi nyuma kwa nguvu lakini Lyn alikuwa kashalegeza mikono yake, akamwangalia usoni kumuona aliyesema maneno yale, akakutana na uso wenye muonekano dhaifu wa Lyn.
Ed akainuka na kulainisha koo lake kisha akasema "nadhani itakuwa vyema nikapumzike kwa kuwa mama na baba wako hapa Lyn. Take care of yourself. "I'll be ready for you" maneno ya mwisho akayasema kwa msisitizo lakini kabla hajaondoka, mama yake Lyn akamgusa bega,
"Asante mwanangu, pole kwa usumbufu wote wa kumleta mwenzio hapa. Kapumzike.. uwe mwangalifu njiani usiku umeenda sana" mama huyu aliongea kwa unyenyekevu kiasi kwamba Ed akabaki akimkagua kama maneno yake hayana unafiki. "How I wish walau Lyn akachukua unyenyekevu huu" akawaza.
"Asante mama nitajitahidi." Akajibu kwa heshima lakini alipogeuka akagundua Martinez na Lyn walimwangalia yule mama kwa jicho la ukali. Akapiga hatua kutoka nje moyoni akikusudia kutorudi. Martinez akamfuata kwa nyuma.
Alipotoka nje akamkuta Li akiwa pale kwenye benchi akimsubiri.
"Mr Simunge" Martinez akamuita.
"Mmmmmm" Ed akaguna, kisha akasimama
"Naomba usijaribu kumuumiza binti yangu kama ulivyofanya leo, hujui maumivu ya kupoteza mtoto" Martinez akaongea kwa taratibu akimwangalia huku tabasamu la kibabe lilikionekana usoni mwake...
"Sijui maumivu ya kupoteza mtoto ila najua maumivu ya kupoteza baba. Mr Kussah unajaribu kunitisha au?" Ed akauliza na sauti yake ilionesha wazi kukerwa...
"Ha ha ha hapana Mr Simunge, Joselyn ni binti yangu pekee, sitataka kumuona akiwa na huzuni na mateso kwa sababu ya kukosa kwako uaminifu"
Li aliyekuwa amesimama akamsogelea kaka yake na kumpa ishara waondoke, Ed akamwangalia Martinez akamwambia
"Kitu pekee ambacho hujui kuhusu mimi ni kuwa vitu vya hovyo huwa sivipatii muda. Mlee binti yako, acha kumrubuni na maisha ya filamu. Usiku mwema Mr Kussah"
Edrian akaondoka akiambatana na Li ambaye hakuongea chochote akijua kaka yake sasa ni mchungu kumkabili. Walipofika kwenye gari bado kimya kiliendelea kutanda kati yao, Li hakuthubutu kuongea zaidi ya kuendesha gari huku akimwangalia kaka yake ambaye alikaa nyuma kichwa amekiegemeza na macho yake yakiwa yamefumbwa.
"Li" akaita kizembe
"Naam bro"
"Nataka kujua kila anachofanya Martinez, anayekutana nae, anapolala, na kila taarifa kumhusu yeye na Lyn.... Ongea na Captain."
Li hakukataa alijua kwa sasa 4D itakuwa zaidi ya busy.
"Sawa bro"
"Kitu kingine" Ed akashusha pumzi akaendelea " nisaidie mtu wa kuangalia usalama wa Aretha"
Li aliposikia akaamua kuuliza maana hakujua kule ndani ya chumba alicholazwa Lyn nini kiliongelewa..
"Una wasi wasi na usalama wa Aretha bro"
"Lyn ni kinyonga, tangu asubuhi anataja jina lake, nina mashaka na ujinga anaoweza kuufanya kuhakikisha anamtoa karibu yangu" Ed aliongea kwa uchovu.