Masaa mawili yaliisha Edrian na mdogo wake Linus wakiwa wamekaa kwenye benchi dogo nje ya chumba ambacho alilazwa Lyn. Ndani alibaki Martinez na mama yake Lyn wakimsubiri binti yao arudishe fahamu zake kama Dokta alivyowapa mrejesho kuwa atazinduka muda sio mrefu.
Ed aliyekuwa kainama akiangalia simu yake alishtuliwa na mlango ulipofunguliwa na Martinez ambaye alimgusa bega...
"Tunaweza kuongea kidogo pembeni?" Uso wake ulionesha msisitizo na hakuacha tabasamu lake usoni.
"Okay" Ed alijibu na kuinuka akimpa ishara Li amsubiri pale pale. Akamfuata Martinez ambaye alikuwa mwenyeji kwenye hospitali hii. Wakaelekea mpaka kwenye mgahawa wa hospitali ambapo kwa muda huo wa usiku kulikuwa na watu wachache sana.
Wakakaa kwenye meza iliyokuwa pembezoni kabisa mwa ukumbi ule. Mhudumu alipowasogelea kuchukua oda zao, walimuashiria hawatatumia chochote zaidi ya maji. Baada ya kuletewa maji kimya kiliendelea kati yao kwa dakika chache mpaka Martinez alipokohoa kidogo kujiweka sawa sauti yake akaanza,
"Mr Simunge... naamini mambo tunayozungumza hapa hayahusiani na biashara zetu. Nazungumza kama baba wa mpenzi wako"
"Mmmmm" Ed aliguna
"Tumeongea na Dokta, anasema Lyn yuko katika hali hiyo kutokana na mfadhaiko wa muda mrefu (Depression). Dokta katuuliza kitu gani kinachomfadhaisha binti yetu, hatukuwa na jibu. Tukamuomba Dokta tuzungumze na mpenzi wake ambaye alilala kwake."
Sura ya Edrian ilipata mikunjo ya ghafla na mikono yake iliyokuwa juu ya meza akaishusha na kuikunja kwa nguvu.
"Mr Simunge what's happening to my daughter is caused by you, can you explain to me?" Martinez akamalizia kwa swali ambalo Edrian hakujua hasa nini ajibu. Akajiweka vyema na kutuliza vurugu za hasira ambazo ziliusukuma moyo wake kwa kasi..
"Mr Kussah, naamini kwamba wewe mzazi wa Lyn umemlea binti yako vyema kuweza kukabiliana na changamoto za maisha. Na kama inafikia wakati hawezi kukabiliana nazo ni wazi kuna sehemu hukufanya vyema."
"Wait, unayageuza mambo kwangu Mr Simunge?" Akauliza Martinez bila kuficha tabasamu la dhihaka usoni pake. ..
"Mr Kussah, am sorry lakini nimevumilia mambo mengi kwa binti yako na upande huu unachangiwa na ambition yako kutaka kuniharibia kampuni yangu. Ikiwa binti yako ana mfadhaiko ni matokeo ya mambo unayoyafanya" Ed alimaliza na kunyanyua chupa ya maji kunywa, alipoishusha chini ilikuwa imebaki na maji kidogo sana
"Mr Simunge una maadui wengi kuliko hesabu unayoijua...na taarifa yoyote unayoipokea kuhusu mimi na shughuli zangu huwezi jua, kuna mtu anatenda kazi kutuchonganisha" Ed akajaribu kuongea lakini Martinez akampa ishara anyamaze kwanza
Jana tumelumbana na Lyn wangu sababu ya tuhuma zako juu yangu, ambazo hazina mashiko yoyote. Asubuhi mama yake ananiambia Lyn hayupo nyumbani. Anampigia simu mama yake kuwa anahamia kwa mchumba wake, mama yake kajaribu kumshawishi arudi lakini kasema wewe umempokea na hatarudi. Jioni unanipigia simu binti yangu kazirai, hivi Mr Simunge nani napaswa nimtuhumu kwa matatizo ya binti yangu ee!" Macho ya Martinez yakawa makali kwa Ed
"Hawa wananichezea" Ed akawaza, "Lyn ni copy ya baba yake" akashusha pumzi
"Mr Kussah hii yote ni 'misunderstanding' na sitegemei utajenga tuhuma yoyote kwangu. Subiri aki____" muito wa simu ya Martinez ulimkatisha Ed aliyekuwa ajieleza.
"Aahm" ndivyo Mr Kussah aliitikia mara baada ya kupokea simu yake
"Tunakuja sasa hivi" akajibu na kukata simu
Akainuka.."Lyn ameamka tunatakiwa kwenda"
Edrian hakuinuka "Mr Kussah nadhani nafasi yangu inaishia hapa. Ameshaamka tuwaache na yaliyosalia."
Mr Simunge, she is calling you. Please" Mr Kussah alimuangalia Ed kuonesha msisitizo
Edrian akainuka na kumfuata Martinez wakirudi kwenye chumba alicholazwa Lyn.
Uso wa Ed ulionesha kuchoka, hadi muda huu wa saa sita usiku alikuwa hajapumzika tangu alipoamka alifajiri.
Walipofika Ed alimuona Li amesimama pembeni ya mlango akiwa na mama yake Lyn. Edrian tangu amfahamu Martinez Kussah hakuwahi kumfahamu mkewe mpaka leo walipokutana nae hospitali. Alipowaona alifungua mlango wakaingia wote ndani, walipokelewa na Lyn ambaye alikaa kitandani....