Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 245 - MKONO WAKO UMEFANYA HAYA

Chapter 245 - MKONO WAKO UMEFANYA HAYA

"Retha, samahani nilipata simu ya dharura ofisini na sasa niko njiani naelekea huko" Edrian akaongea na simu mara tu alipoingia kwenye gari...

"Kuna tatizo kubwa?" Akauliza Aretha kwa wasiwasi

"Sijui, lakini mfumo wa mawasiliano umezima ghafla wakati ambao kuna ndogo uko safarini. Naomba unipe muda nitakutafuta nitakapomaliza."

"Sawa." Aretha akajibu na kukata simu.

Akaamuru simu impigie Captain, "Vipi umefikiwa wapi?"

"Sio jambo la kawaida mfumo kuzima pasipo kutoa onyo. Nafanyia kazi kaka"

"Niko njiani nakuja, tafuta namna nyingine ya kuwapata walioko njiani na mzigo" Ed akajibu huku uso wake ukijikunja. Kwanza alichoshwa na kuvurugiwa ratiba yake ya mapumziko. Ratiba yake na Aretha siku za mwisho pale Singapore iliwapa nafasi kidogo ya kupumzika. Alihitaji muda huu ili kujiweka sawa kabla ya kurejea katika majukumu yake ya kuja siku.

'Nini kinaendelea hapa?' Akawaza.

**********

"Habari ya mchana Loy" Ed akamsalimia Loyce ambaye aliinama kwenye kompyuta akifuata maelekezo ya Captain ambaye alikuwa ofisini kwa Alphonce

"S-salama bosi, nikulet____" Loy akataka kusimama lakini kabla ya kufanya hivyo Ed alikuwa ameingia ofisini kwake

"Mhhh leo siku itakuwa ndefu" Loy akasema huku akiketi kwenye kiti

Ed akaelekea kwenye kabati lake lililokuwa karibu na mlango wa kuingia kwenye maliwato. Akafungua mlango wa upande wa kushoto kisha akabonyeza kitufe kwa juu ya mbao. Kukafunguka sehemu ndogo kama kisanduku cha hazina, akaweka kidole chake na kisha akaingiza namba, kikafunguka. Akatoa kifaa kidogo kama kitunza taarifa akakiingiza mfukoni. Akafunga na kisha akatoka ofisini kuelekea ofisini kwa Alphonce huku njiani akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa SGC ambao walifurahi kumuona..

"Habari zenu!" Akasalimia mara alipoingia

"Salama kaka" wakajibu huku Alphonce na Allan wakiinua nyuso zao kumtazama, lakini Captain hakutoa macho yake kwenye kompyuta.

"Tumepata nini hadi sasa?" Akauliza Ed huku akitamani aambiwe limeishamalizika..

"Inaonesha tumetembelewa na kirusi mpya ambaye nina uhakika amepandwa na mtu makusudi ya kuharibu mfumo wa mawasiliano" Captain alijibu huku akiendelea kubonyeza vitufe kwenye kompyuta.

"Unaweza kuangalia alipandwa kutokea wapi?" Akauliza Alphonce

"Nafikiri itakuwa vizuri" akajibu Ed

Captain akainua kichwa na kumtazama Allan kisha akaendelea na kuchapa namba kwenye kompyuta ambazo kwa mtu mwingine angedhani hajui alichofanya.

Baada ya dakika kumi, Captain akaachia tabasamu na kubonyeza kitufe cha kuingia mara kompyuta ikazima na kisha sekunde thelathini ikawaka tena..

"Tumerudi" akamwambia Edrian ambaye aliketi kwenye kiti karibu na mlango..

"Allan fuatilia na watu wa G-Town"

Allan aliposikia maelekezo ya Ed akawa kama mtu aliyezinduka usingizini, akainuka kiunyonge na kuelekea ofisini kwake

Akabaki Alphonce, Captain, Silvia na Edrian.

"Umefanikiwa kupata chanzo cha huyo kirusi?" Akauliza

"Nafanyia kazi bro, ila nipe dakika chache nitamaliza kazi" Captain akamjibu

Allan alipoingia ofisini kwake akachukua simu yake na kumpigia Renatha,

"Salama Renatha, naomba uniambie ukweli kama hauhusiki na kupanda hicho kirusi?"

"Kirusi gani?" Akauliza Renatha kwa mshangao.

"Usiniigizie tafadhali nakuomba, hujui kirusi kilichofunga mawasiliano na ofisi za G-Town" sasa sauti ya Allan ilibeba hisia za hasira

"Allan, nimeomba ruhusa nipumzike, sio kuanza kushtakiwa kwa makosa nisiyofahamu" Renatha naye akajibu kwa hasira

"Naomba isiwe ni mkono wako umefanya haya Renatha." Allan alipomaliza akakata simu na kushusha pumzi kwa nguvu. Akaegemea kwenye kiti lakini akakumbuka maagizo ya Ed.

Akaingia kwenye mfumo wa mawasiliano na kisha akawatafuta watu wa mgodi wa SGC G-Town.

Baada ya dakika tano Allan alipata taarifa mbaya zaidi juu ya ndege iliyobeba mzigo kupoteza mawasiliano na kutojulikana ilipo.

Allan sasa alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa akijaribu kuwasiliana na watu ambao aliamini wanaweza kusaidia kufuatilia taarifa za awali za ndege.

Akampigia akampigia Ed ambaye bado alikuwa ofisini kwa Alphonce. Wakakutana ofisini kwa Ed,

"Tunatakiwa kuondoka sasa hivi"